Na Mwandishi wetu,JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema kuna uwezekano wa kutokea kwa Kimbunga kamili hadi kufikia kesho tarehe 2 Mei 2024 kutokana na uwepo wa mgandamizo mdogo wa hewa katika Bahari ya Hindi mashariki mwa pwani ya Mtwara.

Kupitia taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo leo Mei 1, 2024 imesema Wakati mgandamizo huo mdogo wa hewa ukiendelea kuimarika, unatarajiwa pia kusogea kuelekea baadhi ya maeneo ya pwani ya nchi kuanzia usiku wa kuamkia siku ya Ijumaa tarehe 3 Mei 2024.

Aidha taarifa hiyo imedai Mgandamizo huo mdogo wa hewa unatarajiwa kuendelea kuwepo katika maeneo ya ukanda wa pwani ya nchi hadi tarehe 6 Mei 2024.

LHata hivyo, mgandamizo huo mdogo wa hewa unatarajiwa kupungua nguvu baada ya tarehe 6 Mei 2024.

TMA imewataka Wananchi kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri
kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.

Uwepo wa mgandamizo huo mdogo wa hewa unatarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Morogoro, Dar es Salaam na maeneo ya jirani.