Na Suzy Butondo,JamhuriMedia, Shinyanga

Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Magharibi Walter Christopher amesema uchakachuaji wa mafuta umepungua kutoka asilimia 80 hadi asilimia 4 mwaka 2022.

Hayo ameyasema leo Alhamisi Mei 2,2024 wakati akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Shinyanga juu ya shughuli za udhibiti wa huduma za nishati na maji kwa lengo la kuimarisha uelewa.

Christopher amesema awali mafuta yalikuwa yanachakachuliwa kwa asilimia 80 lakini kwa sasa wameweza kudhibiti hadi kufikia asilimia 4 kwa mwaka 2022, na hivyo kwa sasa mafuta yapo salama hivyo wateja wasiogope vituo vya mafuta kwamba sehemu furani yamechakachuliwa.

Meneja wa mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati na maji EWURA kanda ya magharibi akizungumza kwenye mafunzo ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga

“Niwaombe wananchi msiogope vituo vya mafuta kwamba mafuta yamechakachuliwa hapana kwa sasa tumeshadhibiti vituo vyote vina mafuta safi kabisa kwa sababu tunayaona na kwenye vituo vyote tunatembelea na wengine tayari tulishawachukulia hatua kali za kisheria kwa sasa usalama upo vizuri,”amesema Christopher.

Afisa mwandamizi idara ya mafuta kutoka EWURA muhandisi Ibrahimu Kajugusi amesema Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ndiyo mdhibiti mkuu inayoa kibali kwa wauzaji mafuta na inatoa kibali kwa wafanyabiashara wanaohitaji kuanzisha kituo cha mafuta, ikiwa ni pamoja na kushauri ni eneo gani kijengwe kituo chamafuta.

Afisa mwandamizi uhusiano kwa umma kutoka EWURA Thobietha Makafu amewashauri watumiaji wa gesi kwamba wanapotumia gesi wasiiweke kwenye sehemu ya joto na watakaposikia harufu wakague inawezekana jiko likawa linavuja,na ikitokea hali hiyo waweze kufungua madilisha na wasiwe na simu za mkononi au wasiwashe taa, wahakikishe wanafungua madirisha ili kuepuka ajali ya gesi.

Afisa Mwandamizi huduma kwa wateja kutoka EWURA kanda ya magharibi Getruda Mbilinyi akizungumzia utaratibu wa kuwasilisha malalamiko, ambapo amesema malalamiko ni moja ya kazi ambazo wanapaswa kuzifanya, ambapo pia amesema wajibu wa Tanesco unaishia kwenye mita, mambo mengine ni mteja na mkandarasi.

‘”Mtumiaji yeyote anaweza akalalamika, mtu binafsi, kikundi unaweza kutumia mwanasheria kwa ajili ya kuweza kushughulikia lalamiko lako, pia niwakumbushe kwamba ukinunua nyumbaunatskiwa uhakiki kuwa nyumba hiyo haikuwa na deni, kwani wengine wamekuwa wakinunua na kukutana na madeni makubwa yakiwemo ya umeme hivyo niwaombe tuwe makini,”amesema Mbilinyi.

Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Shinyanga, Patrick Mabula, ameishukuru EWURA kwa kutoa semina hiyo na kuahidi elimu watakayoipata wataitumia kuelimisha wananchi kupitia Kalamu zao.

Baadhi ya waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga akiwemo Stella Ibengwe ameshukuru kupatiwa mafunzo hayo hivyo ameelewa kazi nyingi zinazofanywa na EWURA hivyo ataendelea kuelimisha jamii kwa kutumia kalamu yake iki iweze kuwa na uelewa.

Afisa mwandamizi idara ya mafuta kutoka EWURA Mhandisi Ibrahimu Kajugusi
Afisa mwandamizi uhusiano kwa umma kutoka EWURA Thobietha Makafu akizungumza