Na Joe Beda Rupia

Nimewahi kuhoji katika safu hii miezi kadhaa iliyopita iwapo kilimo bado ni uti wa mgongo wa taifa letu. Hakukuwa na majibu ya moja kwa moja.

Kilimo. Kilimo. Kilimo. Kimekuwa kikiambatana na kaulimbiu mbalimbali, lakini kwa hakika kimetelekezwa

kwa miaka mingi na kuendelea kuwa cha kujikimu.

Kilimo cha ujima. Kilimo tulichorithi kutoka kwa mababu zetu, kikavurugwa na wakoloni na sasa kimeshindwa

‘kurejeshwa kwenye reli’ na watawala wakati huu wa utandawazi.

Mwaka hadi mwaka ile kaulimbiu tuliyoisikia utotoni ya ‘kilimo cha kufa na kupona’, imekuwa ikijidhihirisha kuwa

ni ‘kilimo cha kufa tu’; hakuna kupona.

‘Farmer’ na ‘peasant’ ni maneno mawili ya Kiingereza yanayomzungumzia mtu mmoja anayefahamika kwa Kiswahili kama ‘mkulima’. Je, mkulima wa Tanzania ni farmer au peasant?

Ukweli mchungu ni kwamba, mkulima wa Tanzania ni ‘peasant’. Hana haki. Anasikiliza uamuzi wa watu walioko

Dodoma. Hana nafasi ya kujidaia uhuru wake.

Anaendeshwa tu. Huyu si sawa na farmer hata kidogo! Na hili si sula la jana au juzi, ni la miaka mingi. Serikali

zinarithishana na maofisa wake kumtumia mkulima kujitajirisha bila haya wala soni.

Kuna miaka wakulima wa pamba waliuziwa mbegu feki. Samahani, walikopeshwa mbegu feki. Wakapanda kwenye mashamba yao na hazikuota. Hatua gani ilichukuliwa? Mungu ndiye anayejua.

Wakulima wa kahawa nao walipoona ukulima wao umegeuzwa uzwazwa, wakaamua kukata miti ya kahawa. Hakuna aliyejali.

Wakulima Mpanda na Tabora wamewahi kuvushwa msimu mzima bila tumbaku yao kununuliwa na hakuna aliyejali kwamba kilimo cha tumbaku ndiyo maisha yao.

Kwamba hulima kwa kuzunguka mwaka hadi mwaka. Julai na Agosti wanafulia mbegu kwenye vitalu; Septemba na Oktoba wanaandaa mashamba; Novemba na Desemba wanapandikiza miche mashambani; Januari na Februari wanapalilia; Machi na Aprili wanavuna na kukausha tumbaku kwenye mabani; Mei, Juni na Julai wanaingiza tumbaku sokoni na kuuza.

Fedha inayopatikana hapo ndiyo hutumika kuandaa mashamba kwa ajili ya msimu unaofuata. Sasa asipolipwa, anaandaaje mashamba?

Wafanyakazi na wasomi wao wanapambana kuongezewa mishahara, vyeo na madaraja na kweli wanaongezewa.

Mkulima yupo yupo tu. Hana wa kupambana naye ili apatiwe haki zake.

Madhira kwa wakulima yamekuwa yakibadilika mwaka hadi mwaka. Ya mwaka huu si sawa na ya mwaka juzi.

Lakini yapo tu. Hayaishi!

Wakulima wa mihogo na mbaazi wanaahidiwa soko la uhakika Uchina. Wanaingiza fedha nyingi kwenye kilimo.

Wanavuna. Mara, mnunuzi haonekani! Hasara. Hakuna kwa kulalamika na serikali ipo tu.

Wakulima wa mahindi nao ndio kabisaaaaa! Wamewahi kuzuiwa kuuza nje ya nchi. Mahindi ya msimu mmoja

yakakutana na ya msimu mwingine. Bungeni wakaambiwa ni rahisi kuagiza mahindi Marekani kuliko kuyatoa Sumbawanga. Miaka inakwenda. Mwaka jana bei ya mbolea imeruka kuliko ilivyowahi kutokea wakati wowote na hakuna anayejali. Mfuko mmoja umetoka wastani wa Sh 50,000 hadi kufikia Sh 120,000!

Hakuna anayejali. Hiki ni kilimo cha kufa tu, hakuna kupona. Wakulima wafanyeje? Wengi wamelima bila mbolea. Yaani karne ya 21 unalima bila kutia mbolea kweli?

Kwa nini mbolea ikapanda bei kwa kiwango kile? Nani ana majibu sahihi? Wizara ya Kilimo inasema nini? Kampuni (Shirika la) ya Mbolea (TFC) iko wapi? Inafanya nini? Ina majibu gani kuhusu kupanda bei kwa mbolea?

Ukitazama kwa jicho makini utagundua kuwapo kwa ‘cartels’ kushinikiza upandaji wa bei ya mbolea.

Hili linapaswa kuchunguzwa na kutafutiwa dawa kwa kuwa haiwezekani hali ile ikatokea halafu wakubwa wote

wakae kimya tu. Mkulima aende wapi? Wakati wa Waziri Mkuu alipokuwa akifunga Bunge Novemba/Desemba mwaka jana, alisema TFC ingeingiza nchini maaelfuya tani za mbolea ili kudhibiti kupanda kwa bei.

Je, kwa nini hilo halikufanyika? Ni nani aliyezuia TFC isilete mbole nchini? Kuna nini hapo?

Jibu ni moja tu. Kuna watu, tena wakubwa sana tu, wanaonufaika na ukubwa wa bei ya mbolea na hawataki

TFC ilete mbolea.

TFC ikiingiza mbolea, ni wazi hawatapata asilimia kadhaa wanazopewa na jamaa fulani hivi. Hili halihitaji PhD

kuliona! Linaonekana wazi kabisa.

Kiwanda cha TFC Tanga kimekufa, kimeoza na kusahaulika kana kwamba watu wameacha kulima! Jamani!

Je, katika hali hii, ‘mapinduzi ya kilimo’ yaliyomo kwenye bajeti ya 2022/23 yatawezekana?

Muda utaongea.

0679 336 491

By Jamhuri