NA BASHIR YAKUB

Hauna haja ya kuvutana na mtu kuhusu iwapo wewe ni baba wa mtoto au hapana. Nimesema baba kwa sababu wasiwasi wa aina hii mara zote upo kwa wanaume. Kuwa fulani ni mama wa fulani karibia mara zote hapana utata.

Basi wapo wanaopenda au ambao wangependa kufanya vipimo vya vinasaba (DNA) kuthibitisha kama ni wazazi kweli au hapana. Nitaeleza utaratibu mzima hapa kutokana na Sheria ya Usimamizi wa Vinasaba vya Binadamu ya 2009, Sura ya 73.

1. Nani anaweza kupimwa DNA?

Yeyote ambaye anahitaji kujua kuhusu uhalali wa uzazi wake anaweza kupima DNA. Upimaji huu hauna umri. Hata hivyo DNA si kwa jili ya masuala ya kuthibitisha uzazi tu, bali hutumika hata katika masuala ya ushahidi na upelelezi.

2. Nani ana mamlaka ya kuomba DNA kupimwa?

Si kila mtu anaweza kuomba kupima DNA. Hata kama mwenye uhitaji ni wewe lakini bado hauna mamlaka ya kuomba kupima DNA.

Kifungu cha 25(2) cha sheria niliyotaja hapo juu kinawataja wafuatao kuwa na mamlaka ya kuomba DNA kupimwa.

Kinamtaja hakimu ambapo kuna kesi/shauri fulani linaendelea, wakili, ofisa ustawi wa jamii, ofisa wa polisi mwenye cheo zaidi ya mkaguzi (inspector), daktari na mkuu wa wilaya.

Hawa ndio wenye mamlaka (Requesting Authority). Kwa hiyo wewe ukiwa na shida ya DNA unaweza kumuona

mmoja miongoni mwa hawa ili aandae maombi ya kupima DNA na kuyapeleka kunakostahili.

3. Maombi ya DNA yanapelekwa wapi?

Kifungu cha 24 cha Sheria ya Usimamizi wa Vinasaba kinataja maabara ya vinasaba vya binadamu ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa na mamlaka ya kupima DNA. Pia kinazitaja maabara nyingine ambazo zitakuwa na leseni maalumu ya kupima DNA kuwa na mamlaka hayo.

Kwa hiyo maombi ya DNA yatapelekwa moja kati ya sehemu hizo.

4. Nani anapeleka maombi na kufuatilia majibu?

Wahusika waliopimwa DNA hawaruhusiwi kupeleka wala kufuatilia majibu. Maombi na majibu ya DNA yatapelekwa na kufuatiliwa na hao niliowataja hapo juu katika namba 2, ambao ndio wenye mamlaka ya kuomba DNA kupimwa.

Hawa ndio watapeleka maombi na ndio watachukua majibu na kuwasomea wahusika.

5. Maombi ya kupima DNA yanakuwaje?

Kifungu cha 26(1) cha sheria hiyo kinasema maombi ya kuomba DNA kupimwa yatakuwa katika mfumo maalumu wa maandishi.

Yataeleza mwombaji na cheo chake, yataeleza wanaotakiwa kupimwa DNA na sahihi zao, yataeleza DNA ipimwe katika nini na nini, yataeleza sababu za kupima DNA, yatakuwa na kiapo kuwa majibu hayatatumika kwa shughuli nyingine tofauti na iliyoombwa, na yatasainiwa na muombaji ambaye ni wale niliowataja katika namba 2 juu.

6. Ada ya kupima DNA ni kiasi gani?

Malipo yapo. Na mpaka Desemba 2018 ilikuwa ni Sh 100,000 tu kwa kila mtu. Kawaida DNA ya kutambua uzazi hupimwa watu watatu. Mama, baba na mtoto. Kwa hiyo kila mmoja ni Sh laki moja, hivyo watatu ni Sh laki tatu.

Nani anatoa hizo fedha, anaweza kuwa yule anayehitaji kuthibitisha kwamba yeye ni mzazi halali, au yakawa ni

maelewano ya wahusika, au kutokana na maelekezo ya mahakama.

7. DNA inapimwa katika nini na nini?

Kifungu cha 29(1) cha sheria hiyo kinaeleza maeneo ambayo DNA inaweza kupimwa kuwa ni kwenye mate, damu, mkojo, ute ute wa sehemu za siri, nywele, haja kubwa, ngozi, mifupa, meno, mbegu za kiume, unyayo na sehemu nyingine ambayo mhusika atakuwa amegusa, kukanyaga au kuwapo au alama yoyote ya uwepo wake.

Basi yatutoshe haya kwa leo kuhusu DNA ya kutambua iwapo u-mzazi wa fulani ama hapana.

By Jamhuri