Na Edward Kondela, JamhuriMedia, Mbeya

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa namna inavyotekeleza Programu ya Kielelezo “Jenga Kesho Iliyo Bora” (BBT – LIFE) na kuwataka vijana waliopo kwenye programu hiyo kutumia vyema fursa hiyo.

Rais Samia amesema hayo leo Agosti 8, 2023 wakati alipotembelea mabanda ya wizara hiyo, kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima (Nanenane) yakiwa yanaelekea kuhitimishwa

Ameongeza kuwa amepata faraja kubwa kuona namna wizara hiyo ikiongozwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) pamoja na watendaji wa wizara wanavyosimamia vyema programu ya BBT – LIFE katika sekta za mifugo na uvuvi kwa kuwapatia vijana mafunzo ya vitendo ya unenepeshaji wa ng’ombe, kaa, jongoo bahari, pamoja na kilimo cha mwani.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwapatia ng’ombe chakula baada ya kutembelea moja ya mabanda ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima (Nanenane) katika viwanja vya John Mwakangale ijini Mbeya, ambapo ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa namna inavyotekeleza Programu ya Kielelezo “Jenga Kesho Iliyo Bora” (BBT – LIFE) na kuwataka vijana waliopo kwenye programu hiyo kutumia vyema fursa hiyo.

Amesema soko la nyama nje ya nchi ni kubwa hivyo kupitia programu ya BBT – LIFE vijana wanaopatiwa mafunzo ya kunenepesha ng’ombe wanapaswa kutumia fursa hiyo ili kunenepesha ng’ombe kwa wingi na kupata masoko ya kuuza mifugo yao viwandani na hatimaye kuchakatwa na myana kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Akizungumzia juu ya BBT – LIFE Sekta ya Uvuvi, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka vijana kuhakikisha wanatumia vyema fursa ya ufugaji viumbe maji kuelekea uchumi wa buluu kwa kuongeza uzalishaji wa viumbe hivyo wakiwemo samaki.

Ameongeza kuwa amekuwa akitafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha programu mbalimbali zinaanzishwa na kuendelezwa zikiwemo za ufugaji wa samaki ili vijana waweze kuingia katika fursa hizo na kujiongezea kipato hivyo kuwataka wazitumie vyema.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amemuelezea Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan namna wizara ambavyo imejikita kuhakikisha programu ya BBT – LIFE inasambaa maeneo mbalimbali nchini ili vijana wengi zaidi waweze kujiunga na programu hiyo.

Amesema lengo la wizara ni kuona sekta za mifugo na uvuvi zinaongeza uzalishaji na kuinua pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwapatia samaki chakula baada ya kutembelea moja ya mabanda ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima (Nanenane) katika viwanja vya John Mwakangale ijini Mbeya, ambapo ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa namna inavyotekeleza Programu ya Kielelezo “Jenga Kesho Iliyo Bora” (BBT – LIFE) na kuwataka vijana waliopo kwenye programu hiyo kutumia vyema fursa hiyo.

Nao baadhi ya vijana wanaonufaika na programu ya BBT – LIFE wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameanzisha programu hiyo ambayo ina manufaa makubwa kwao kwa kuwa inawaongezea maarifa na kuwaongezea kipato.

Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima (Nanenane) yamekuwa yakifanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya tangu Agosti Mosi mwaka huu.

By Jamhuri