Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Songea

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amewaasa Washereheshaji kutumia lugha ya Kiswahili kwa ufasaha na kuibua misamiati mipya ambayo inaweza kichakatwa na kuwa rasmi katika kukuza lugha hiyo.

Ndumbaro ametoa rai hiyo tarehe 26, 2024 mjini Songea wakati akifungua mafunzo kwa washereheshaji, wasanii, wapambaji, wazalishaji wa kazi za sanaa ambayo yameendeshwa na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA).

“Ushereheshaji ni biashara na ajira, ni wakati sasa wa kurasimisha kazi zenu ili mtambulike rasmi, tasnia ya ushereheshaji inatumika katika kukuza lugha kupitia misamiati mnayotumia ili muendelee kufanya vizuri katika tasnia hii”, amesema Mhe. Ndumbaro.

Amewataka washereheshaji hao kurasimisha biashara zao katika taasisi za Serikali ikiwemo BRELA, kuhakikisha wanapata leseni ya biashara ili waweze kuingiza kwenye soko la ushindani, ambapo pia amewataka kuwa wabunifu katika kazi hiyo.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BAKITA, Bi. Consolatha Mushi amesema mafunzo hayo yana lengo la kufikisha ujumbe kwa wadau mbalimbali wanaotumia lugha ya Kiswahili katika kazi zao kuwa na uelewa wa maneno sahihi ya kutumia kulingana na hadhira na aina ya tukio wanalofanyia kazi pamoja na kukuza lugha ya kiswahili.   

By Jamhuri