Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini Tanzania, EWURA, imetangaza bei mpya za mafuta ambazo zinaonesha, mafuta aina ya Petroli imepanda kwa shilingi 443 na dizeli ikipanda kwa shilingi 391 kwa kila lita moja kwa mafuta yanayouzwa katika jiji kuu la kibiashara Dar es Salaam.

Hivyo bei ya lita moja katika kituo cha mafuta kwa Dar es Salaam ni shilingi 3199 kwa petroli na shilingi 2935 kwa dizeli.

EWURA imesema sababu ya mabadiliko hayo bei ambayo huanza kutumia kila Jumatano ya kwanza ya mwezi ni tatizo la upatikanaji wa dola ya Marekani, mabadiliko ya sera za kikodi, kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani, sababu nyingine ikiwa ongezeko la gharama za mafuta katika soko la dunia na gharama za uagizaji wa bidhaa hiyo.

Ongezeko la zaidi ya shilingi 440 kwa mafuta ya petroli na zaidi ya shilingi 390 kwa mafuta dizeli jijini la Dar es Salaam ndiyo la chini zaidi kulinganisha na maeneo mengine yaliyo mbali na bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara yanakoshushwa mafuta.

Kwa mfano mji wa Bukoba mkoani Kagera ulio ubali wa zaidi ya kilomita 1400 kutoka Dar es Salaam lita moja ya mafuta petroli inauzwa shilingi 3415 kwa lita moja wakati dizeli ni shilingi 3151 kwa lita moja.