Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.
Dkt. Selemani Jafo akimnawisha Mkuu wa Kanda ya Kaskazini TBC Bi.
Anna Kwambaza baada ya kupanda mti wakati wa zoezi lla upandaji wa
miti ililofanyika katika ofisi za Redio Jamii za Shirika la Utangazaji
Tanzania (TBC) mkoani Arusha leo tarehe 27 Aprili, 2024.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.
Dkt. Selemani Jafo akizungumza mara baada ya zoezi la upandaji wa miti
lililofanyika katika ofisi za Redio Jamii za Shirika la Utangazaji Tanzania
(TBC) mkoani Arusha leo tarehe 27 Aprili, 2024.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.
Dkt. Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na watumishi kutoka
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Kanda ya Kaskazini na Baraza la
Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kaskazini
mara baada ya zoezi la upandaji wa miti lililofanyika katika ofisi za Redio
Jamii TBC mkoani Arusha leo tarehe 27 Aprili, 2024.

                                                                          ……………………..

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.
Dkt. Selemani Jafo amezitaka taasisi mbalimbali kuongeza kasi ya
upandaji wa miti katika maeneo yao ili kukabiliana na athari za
mabadiliko ya tabianchi.

Amesema hayo wakati akishiriki zoezi la kupanda miti ya matunda katika
ofisi za Redio Jamii za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) mkoani
Arusha leo tarehe 27 Aprili, 2024.

Amelipongeza shirika hilo kwa kuendesha kampeni ya upandaji miti
katika maeneo mbalimbali nchini ambapo tangu mwaka jana
wamefanikiwa kupanda miti 3,000 ikiwa ni katika kuunga mkono juhudi
za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan.

Waziri Dkt. Jafo amesema kuwa kampeni ya upandaji wa miti
inayoendeshwa na shirika hilo la umma ina mchango mkubwa katika
hifadhi ya mazingira hususan katika maelekezo ya kila halmashauri
kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.

"Niwashukuru TBC kwa sababu mlianza zoezi la Mti wa Mama nawapa
'big up' sana kwasababu mmeonesha mfano na nadhani wengine
wanatakiwa waige mfano kama huu, kila taasisi," amesema Dkt. Jafo
Amesema wananchi wana kila sababu ya kuendelea kushiriki katika zoezi
la kupanda miti na kwamba hadi kufikia hivi sasa tayari takriban 266
imepandwa kati ya 276 ambayo ni malengo ya Serikali kwa kila
halmashauri.

Halikadhalika, ametoa wito kwa wananchi kutumia mvua zinazoendelea
kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini kupanda miti akisisitiza miti
inayopandwa itunzwe na kutoruhusu mifugo kuivamia kwani kufanya
hivyo zoezi la upandaji wa miti litakuwa halkina maana tena.

Kwa upande wake Mkuu wa Kanda ya Kaskazini TBC Bi. Anna Kwambaza
amesema miti iliyopandwa leo ni 25 ikiwemo ya matunda 15 ambayo ni
miembe, miparachichi, michungwa na ya kivuli.

Amesema miti ina faida nyingi na ndio maana mkoani Arusha kuna hali
nzuri ya hewa kutokana na utunzaji wa mazingira na kuwa shirika
linaendesha kampeni hiyo ya kipekee ili kutunza mazingira.

Bi. Anna ameongeza kuwa kwa kupanda miti hiyo wanawaelemisha pia
wananchi hususan majirani wanaozunguka ofisi za shirika hilo kwani
wanajifunza.

Nae Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa Baraza la Taifa la Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bw. Benjamin Doto amesema miti ni
kama mapafu ya dunia ambayo tukiitunza tunaiweka katika hali nzuri.

Tunapoendelea kuiotesha na kuitunza miti tunaifanya dunia kuwa katika
mahali pazuri pa kuishi na hatua hiyo inasaidia kukabiliana na athari za
mabadiliko ya tabianchi.

Pia, meneja huyo amewasisitiza wananchi kutumia mvua zinazoendelea
kunyesha kwa ajili ya kupanda miti kwani ni wakati ambao maji
yanapatikana kwa urahisi

By Jamhuri