Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Serikali imefikia uamuzi wa kutekeleza mradi wa Building a Better Tomorrow (BBT) unaolenga kuongeza ushiriki wa vijana katika kilimo kwa kuwapatia mafunzo, maeneo ya mashamba, mitaji na kuwaunganisha na fursa za masoko.

Ambapo utekelezaji wa mradi huo ni matokeo ya maagizo na maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha vijana wanapata fursa katika sekta mbalimbali za kiuchumi zikiwemo za madini, kilimo na nishati.

Aidha, katika kuhakisha kunakuwa na ustawi na undelevu wa mradi huo Serikali imeanzisha vituo jumuishi vya kutoa huduma za zana za kilimo.

Akizungumza hivi karibuni wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema kuwa katika mwaka 2023/2024, Wizara yake itaanzisha vituo vitatu vya kutoa huduma ya zana za kilimo kwenye mashamba makubwa ya pamoja yatakayoanzishwa kupitia Programu ya BBT.

Aliongeza “Vilevile, itajenga majengo matatu kwa ajili ya kuhifadhi na kuhudumia zana za kilimo kwenye mashamba hayo. Kadhalika, wamiliki na waendeshaji wa mashine na zana za kilimo 50 katika mikoa ya Tabora, Singida na Manyara watapatiwa mafunzo ya matumizi bora ya zana za kilimo”.

Bashe alisisitiza “Wizara itawatambua wasindikaji wadogo na wakati 50 wa zao la alizeti na zabibu katika mikoa ya Dodoma, Singida na Manyara na kuwapatia mafunzo kuhusu usimamizi na utunzaji wa mitambo ya usindikaji”.

Hata hivyo, Wizara ya Kilimo itaendelea kuhamasisha matumizi bora ya zana za kilimo katika mnyororo wa uzalishaji kwa kutoa mafunzo kwa watoa huduma ya zana za kilimo kwenye mashamba makubwa ya pamoja yatakazoanzishwa kupitia Programu ya BBT katika mikoa ya Dodoma, Kagera, Kigoma, Shinyanga, Singida, Pwani, Njombe na Mbeya.

By Jamhuri