Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Mkuranga

Kiwanda cha Sapphire Float Glass (Tanzania) Company Limited, kilichopo Mkiu wilaya ya Mkuranga, Mkoani Pwani kinatarajia kuanza uzalishaji mwezi Septemba mwaka huu na kugharimu USD 311 sawa na fedha za kitanzania sh.bilioni 700.

Aidha kinatarajia kuzalisha tani 700 kwa siku hali itakayowezesha kupunguza uagizaji wa vioo nje ya nchi.

Akitembelea kiwanda hicho, wakati wa mbio za Mwenge, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Abdallah Shaib alieleza kasi kubwa inafanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kutanua wigo wa kidemokrasia na kujenga mahusiano mzuri pamoja na mataifa mengine.

Anasema, mahusiano hayo ndio matokeo ya Wawekezaji hao wa Kichina wameweza kujenga uwekezaji huo mkubwa wenye tija ndani na nje.

“Mwenge huu umetembelea,umepokea taarifa ya mradi na kukagua kwa kina na kujionea maendeleo mbalimbali, nampongeza kwa kipekee Mbunge wa Jimbo hili Abdallah Ulega, Mkuu wa wilaya Hadija Nasri kwa uwajibikaji wenu mkubwa unaonekana “

Shaib anaeleza kuwa, matokeo ya mradi huu mkubwa hapana shaka ni dhamira ya dhati inayotokana na Sera nzuri za uwekezaji zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita.

Nae mbunge wa Jimbo la Mkuranga Abdallah Ulega, alisema katika wilaya inayokwenda kwa kasi nchini katika masuala ya uwekezaji na viwanda ni pamoja na wilaya ya Mkuranga.

Ulega anasema,kadri Rais anavyokwenda nje ya nchi kutafuta fursa za kuinua nchi wilaya hiyo inaongoza kwa fursa hiyo.

“Sisi hapa ni shoo,shoo tunatekeleza sekta ya uwekezaji na viwanda kwa kiasi kikubwa”alisisitiza Ulega.

Ofisa mahusiano na utawala Kiwandani Hapi, Sharifa Chen alifafanua, ujenzi wa kiwanda ulianza mwaka July 2022 na sasa umefikia asilimia 89 .

Sharifa alisema, uzalishaji unaanza mwezi September mwaka huu na utatoa ajira zisizopungua 1,600 .

“Tunaendelea kushirikiana na Serikali na tunaunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuinua sekta ya uwekezaji nchini”alibainisha Sharifa.

Akipokea Mwenge wa Uhuru ukitokea wilaya ya Kibiti, Mkuu wa wilaya ya Mkuranga Hadija Nasri alieleza ,ukiwa wilayani hapo umepitia miradi 12 yenye thamani ya kiasi cha sh.bilioni 500.9 na kukimbizwa katika km.89.5.

Mwenge huo pia umeweka jiwe la msingi kituo cha afya Nyamato ,mradi wa ujenzi wa boksi kalavati, jiwe la ufunguzi wa shule ya Sekondari Kilimahewa ,na kuzindua mradi wa udhibiti shughuli za ufugaji holela kukagua mabanda na mfumo wa utumiaji Bio gesi ikiwa ni manufaa ya ufugaji wa kisasa.

By Jamhuri