Na WAF – Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya afya imedhamiria kuendelea kuboresha huduma za Ukunga sambamba na kuongeza idadi yao ili kupunguza vifo vya watoto wa mchanga.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema hayo leo Mei 5, 2024 kwenye siku ya Mkunga duniani ambapo mgeni rasmi katika Maadhimisho hayo alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.

“Uwepo wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa katika Maadhimisho haya leo ni kielelezo kuwa Serikali ipo tayari kujenga na kuweka mazingira mazuri ya kufanya kazi kwa wakunga ikiwa ni njia moja wapo ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.” Amesema Waziri Ummy

Amesema, sio kila mtu anaweza kufanya kazi ya ukunga, ukunga ni taaluma ambayo tunataka tuendelee kuitambua zaidi na wakati umefika wa kutofautisha Uuguzi na Ukunga.

Aidha, Waziri Ummy amesema wakunga wamekuwa msaada mkubwa kwenye kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga ambapo afua nyingi za afya za uzazi na mtoto zinaendelea kuboreshwa ili kutoa huduma bora za uzazi na afya ya mtoto.

“Serikali imeongeza upatikanaji wa huduma za uzazi salama, huduma za uzazi wa mpango, upimaji wa Virusi vya UKIMWI (VVU) kwa wajawazito, upimaji wa Saratani ya mlango wa kizazi, utoaji wa chanjo kwa rika zote pamoja na utolewaji wa elimu ya afya ya uzazi.” Amefafanua Waziri Ummy

Waziri Ummy amemshukuru Mhe. Rais kwa kuiwezesha Sekta ya Afya katika kuboresha huduma za Afya hususan Afya ya Uzazi mama na mtoto ambapo vifo vya wajawazito vimepungua kwa 80%.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amewataka wakunga hao kuendelea kuwahudumia wateja kwa kutambua wajibu wao wa kuimarisha afya zao ili kufanikisha Dira ya 2025 ya Tanzania na Mendeleo Endelevu yenye malengo kupitia utoaji wa huduma ya afya ya uzazi inayokidhi mahitaji ya afya ya uzazi kwa wanawake na vijana.

“Naomba sana, tuzingatie taaluma zetu, maadili ya kazi, weledi na tufanye kazi kwa kutanguliza utu maana ukunga ni kazi inayohitaji sana kuwa na huruma, sisi wote hapa tumetokana na kazi nzuri ya wakunga.” Amesema Waziri Ummy

Wakunga ni mashujaa wasioimbwa katika utoaji wa huduma za afya hapa nchini, Wakunda ni wataalam tunaowategemea katika huduma bora na muhimu kwa akina mama wajawazito kabla, wakati na baada ya kujifungua.

Siku ya Wakunga duniani huadhimishwa kila ifikapo Mei 05, na kwa mwaka huu hapa nchini Maadhimisho hayo yamefanyika mkoani Dar es Salaam katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere wa Mikutano.