-Atangaza rasmi kampeni ya mbio za hiyari ni ya nchi nzima

-Awataka wakazi wa DSM kuendelea kufanya mazoezi ya hiyari kila Jumamosi kuanzia saa 12:00 Asubuhi hadi saa 3:00 Asubuhi

Na Mwandishi Wetu, JammhuriMedia, Dar es Salaam

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa leo Mei 4, 2024 amezindua mbio za hiyari katika fukwe za Coco beach Kinondoni Jijini Dar es Salaam.

Majaliwa alianza kwa kukimbia mbio za hiyari kuanzia cocobeach, round about ya Aghakan na kurudi tena coco beach akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa Albert Chalamila wananchi,vikundi mbalimbali vya Jogging, waendesha baiskeli, na Viongozi mbalimbali wakiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa huo Dk Toba Nguvila.

Aidha Mhe Waziri amepongeza Mkoa chini ya uongozi wa Mhe Albert Chalamila kwa hamasa kubwa ambayo imewezesha umati wa watu waliokusanyika katika fukwe hizo za cocobeach kufanya mazoezi ambapo ameagiza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuendeleza kampeni hiyo kwa kuhakikisha kila jumamosi wanafanya mazoezi lakini pia kualika Viongozi mbalimbali waje kujumuika nao.

” Barabara hii ya Coco beach hadi Tanzanite kila Jumamosi itakuwa inafungwa kuanzia saa 12:00 Asubuhi hadi saa 3:00 ili kuwafanya watu kuwa huru kufanya mazoezi” Alisema Mhe Majaliwa.

Vilevile Mhe Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa Kinondoni kufanya maboresho eneo la fukwe hiyo upande wa mbele ili liwe na mvuto ambapo amesema Coco beach itaendelea kuwa kwa ajili ya Umma lakini lazima mazingira yawekwe kiutalii.

Mwisho Mhe Majaliwa amesema mazoezi husaidia kwa kiasi kikubwa kujikinga na magonjwa Yasiyoambukiza ambayo kwa sasa ni tishio.

By Jamhuri