Na Isri Mohamed

Klabu ya soka ya Yanga leo inatarajia kushuka dimbani Manungu Complex Turiani mkoani Morogoro kuumana na Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ambao kama wananchi watafanikiwa kuvuna alama tatu basi watatangazwa rasmi kuwa mabingwa kwa mara 30.

Yanga ambao kwa sasa wana alama 68 wakiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, kama atashinda mechi hiyo watafikisha alama 71 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yeyote zinazomfuatia.

Katika msimamo wa ligi, Azam Fc wanashika nafasi ya pili ambapo wakifanikiwa kushinda mechi zote tatu zilizosalia watafikisha pointi 69 sawa na Simba Sc ambao watafikisha pointi 69 wakishinda michezo yao minne iliyobaki.

Mechi ya Yanga na Mtibwa itachezwa majira ya saa 10 jioni, na inatarajiwa kuwa mechi ngumu kwa pande zote mbili, kwani Yanga anahitaji kutangazwa bingwa mapema akiwa na mechi kadhaa mkononi huku Mtibwa wakijipapatua ili kujinusuru kushuka daraja kutokana na nafasi ya chini kabisa aliyopo.