Na Mwandishi Wetu, JakhuriMedia, Songwe

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Daniel Chongolo ameipongeza timu ya wataalamu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kufanya kazi kwa haraka na ufanisi mkubwa kuhakikisha barabara zinapitika mkoani Songwe.

Rc Chongolo ameeleza kuwa changamoto ya uharibifu mkubwa wa miundombinu umefanyiwa kazi kwa haraka na timu ya wataalamu wa TANROADS na TARURA jambo ambalo limerejesha mawasiliano ya pande zote zilizokuwa hazipitiki.

“Kila mmoja kwa barabara zake wamefanya kazi kubwa na wanaendelea kufanya hivyo lengo ni kuhakikisha Wananchi hawakosi huduma ya barabara pale inapotokea changamoto’’ Amekaririwa Mhe Chongolo.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe Mhandisi Suleiman Bishanga akizungumza mara baada ya kukagua sehemu zilizoathirika na mvua za El-Nino wilayani Songwe na Ileje amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 5.7 kwa ajili ya kutatua changamoto na kurejesha miundombinu ya barabara na madaraja ambayo yameharibiwa na mvua kubwa za El- nino zinazoendelea kunyesha Mkoani Songwe.

Amesema kuwa Wilayani Songwe miundombinu imeharibika katika barabara ya Galula – Namkukwe sehemu ya Malangali, daraja la Mpona maji yalifurika juu na kukata mawasiliano kati Kijiji cha Namkukwe na Mpona.

Sehemu nyingine ni Magamba eneo linalounganisha Kijiji cha Mpona na Igalula ambako sasa hivi linajengwa daraja na kuinua tuta la barabara; pia kwenye barabara ya Chang’ombe – Mkwajuni eneo la Zira miaka ya nyuma lilikuwa korofi; lakini mwaka huu halijapata changamoto kwa sababu Serikali kupitia TANROADS ilichukua hatua za mapema kulifanyia matengenezo.

Ameeleza kuwa Wilayani Mbozi Barabara iliyoathirika zaidi ni Mlowo – Kamsamba ambayo inaunganisha Mji wa Songwe kuelekea upande wa Mkoa wa Rukwa ambapo Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni moja kutengeneza maeneo mbalimbali yaliyoharibika.

“Katika Wilaya ya Momba kuna barabara ambayo tumeirithi mwaka jana kutoka TARURA kuja TANROADS na yenyewe ilikuwa katika hali mbaya, Serikali haikusita ikatupa fedha shilingi milioni 500 ambazo zimeenda kushughulikia matatizo ya kule na sasa ile Barabara ya Kwenda Ilonga inapitika’’ ameeleza Mhandisi Bishanga na kuogeza.

“Wilaya ya Mbozi kuelekea Ileje kuna sehemu tunaunganishwa na Daraja la Hezya lile dadaja lilisombwa na maji na Serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 261 kwa ajili ya kujenga daraja hilo na kwa sasa linapitika’’.

Kwa upande wao Afisa Tarafa ya Songwe Godwin Kaunda na Diwani kata ya Magamba Mhe Kapala Chakupewa Makelele wameishukuru serikali kupitia TANROADS kwa urejeshaji wa haraka kwa miundombinu ya barabara na madaraja iliyoathiriwa na mvua za El-Nino zinaendelea kunyesha katika maeneo mengi nchini.

By Jamhuri