Na Mussa Augustine, JamhuriMedia

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imezindua rasmi kampeni inayojulikana kwa jina la ‘Tuwajibike’ yenye lengo la kuwakumbusha na kuwahamasisha wauzaji bidhaa na wanunuzi kutoa na kudai risiti halali za EFD.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati akitambulisha kampeni hiyo Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Richard Kayombo, amesema kampeni ya Tuwajibike ni kampeni yenye malengo makuu matatu ikiwemo kuwakumbusha na kuwahamasisha wauzaji wa bidhaa na watoa huduma nchi nzima kuwajibika kwa kutoa risiti halali ya EFD kila wauzapo bidhaa au kutoa huduma.

Aidha amesema kuwa kampeni hiyo pia imelenga kuwakumbusha na kuwahamasisha wanunuzi wa bidhaa na huduma kote nchini kuwajibika kudai risiti halali za EFD pamoja na kuzikagua ili kujiridhisha kama zinakidhi vigezo vyote muhimu.

Halikadhalika kampeni ya “Tuwajibike”itahusisha kufuatilia utoaji wa risiti halali za EFD pamoja na kuchukua hatua kwa wauzaji wasiofuata sheria katika utoaji wa risiti.

” Risiti halali ya EFD inatakiwa kukidhi vigezo vikuu vinne ambavyo ni jina la biashara,tarehe halisi ya mauzo,kiasi halisi cha pesa kilichonunuliwa bidhaa au TIN ya mnunuzi au vyote kwa pamoja”amesema Kayombo.

Aidha Kayombo amesisitiza kuwa TRA itachukua hatua kwa yeyote atakaebainika kufanya udanganyifu ambapo mfanyabiashara atakayebainika kushindwa kutoa risiti halali ya EFD au kufanya udanganyifu atatozwa faini ya Shilingi milioni tatu (3,000,000) hadi shilingi milioni nne na laki tano ( 4,500,000) au kifungo kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

Amesema kwamba mnunuzi atakaebainika kufanya manunuzi bila kudai risiti halali ya EFD atatozwa faini kuanzia shilingi elfu thelathini ( 30,000) mpaka milioni moja na laki tano( 1,500,000) hivyo amewasihi wananchi kudai risiti kila wanapofanya manunuzi ya bidhaa mbalimbali.

“Tunapenda kutoa wito kwa wafanyabiashara wote kuwajibika kutoa risiti halali za EFD bila kushurutishwa na wanunuzi kudai risiti halali kwa kila manunuzi watakayofanya ili kuepuka usumbufu usio wa lazima na wakati huohuo kuisaidia Serikali kutimiza malengo yake ya kuwaletea wananchi maendeleo na kukuza uchumi wa nchi yetu” amesema.

By Jamhuri