Kwa mara nyingine tena timu ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 17, Serengeti Boys, imeshindwa kupata nafasi ya kushiriki katika fainali za Mataifa ya Afrika zinazotarajiwa kufanyika mwakani nchini Madagascar.

Hii ni historia nyingine mbaya kwa wadau wa soka Tanzania hasa baada ya kaka zao, Taifa Stars, kuchemsha kwenye mbio za kuwania nafasi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwakani nchini Gabon.

Salum Madadi, Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), anasema wapenzi wa soka wanatakiwa kuichukulia hali hiyo kama changamoto na kuendelea kuwatia moyo vijana hao ambao wamepigana vya kutosha.

Anasema ni nia na matamanio ya kila Mtanzania mpenda soka siku moja kuwaona vijana hawa wanakuwa wachezaji wa timu ya Taifa ya wakubwa, na hilo litawezekana tu pale wadau wote wa mpira watakapoungana kuwapa ushirikiano vijana hawa.

Anasema tatizo lililopo ni wadau wa soka kudhani kuwa majukumu yote ya michezo ndani ya nchi yanapaswa kugharamikiwa  na TFF na kusahau kuwa wadau wote wana jukumu la kuhakikisha michezo inasonga mbele.

Anasema mara baada ya Serengeti Boys kushindwa kufuzu katika hatua ifuatayo; kama viongozi watahakikisha vijana hao wanabaki salama bila ya kupotea kama wapenzi wengi wa michezo wanavyodhani.

Anasema wadau wote wa mchezo wa soka wanapaswa kuunganisha nguvu kuhakikisha vijana hawa wanaendelea kuwapo kwa manufaa ya timu ya Taifa ijayo kwa manufaa ya soka letu.

“Hebu tuchukulie  mfano wa nchini Uganda ambako kuna mashindano ya shule za sekondari na vyuo ambayo ndiyo yamekuwa yakitumika kuzalisha wachezaji kama Erisa Ssekisambu (Sports Club Villa), Farouk Miya (Vipers/Bunamwaya) Juuko Mursheed (Simba) na Khalid Aucho (Gor Mahia) ambao wametoa mchango mkubwa kwenye timu ya taifa ya nchi yao,” anasema Madadi.

Anasema wachezaji hao wamepatikana katika mashindano ya shule na vyuo lakini ingawa nasi tuna mashindano yetu ya namna hiyo, siku hizi hatuvuni tena wachezaji kama tulivyokuwa tunavuna mwanzoni mwa miaka ya 2000, katika sekondari  kama za Jitegemee na Makongo, ambazo zilitoa nyota wengi wa soka nchini.

“Ni ndoto kwetu kuwafikia mafanikio endapo mzigo wa kuendeleza michezo nchini utabaki mikononi mwa chama cha mpira cha nchi ni lazima wadau wote kuunganisha nguvu zetu kwa pamoja kama tunahitaji kufikia mafanikio ya kweli,” anasema Madadi.

Charles Boniface Mkwasa, kocha wa timu ya Taifa, Taifa Stars, anasema vijana hao bado wana safari ndefu katika soka kiasi cha kutakiwa kuwa na juhudi za ziada za kuhakikisha wanaendelea kuwapo katika ramani ya soka.

Anasema kuna mambo mengi ya kuangalia pale tunapoipa Taifa Stars kipaumbele cha kufanya vizuri katika mechi za kimataifa; kwanza ni lazima kukubali kuwa soka la Tanzania limegubikwa na changamoto nyingi zinazopaswa kushughulikiwa ndipo Taifa liweze kupiga hatua na kujiamini katika soka la kimataifa.

Kuhusu Serengeti Boys anasema vijana hawa bado wadogo ila wameonesha kuwa katika miaka michache ijayo endapo wataendelea kuwa pamoja, Tanzania itakuja kuwa tishio katika soka la ukanda huu.

“Sote kama wadau wa michezo inatakiwa tuwasaidie TFF katika kuhakikisha vijana hawa wanaendelea kuwa pamoja katika kipindi cha miaka mitatu ijayo kwa manufaa ya Taifa Stars ijayo,” anasema Mkwasa.

Anasema japo katika miaka ya hivi karibuni Serikali imejitahidi kuleta makocha wa kigeni kwa nyakati tofauti, kinachoonekana sasa hivi kwa wachezaji wengi wanaounda timu ya Taifa ni kama vile uwezo wao kisoka umeishia hapo walipofikia kwa hiyo si wakati wa kuwalaumu.

Anasema ni dhahiri kuwa moja ya mambo ambayo kwa sasa ni tatizo kwa wachezaji wa Stars na hata klabu za soka nchini, ni uwezo binafsi wa mchezaji, wa kufanya uamuzi sahihi na wakati mwafaka pale anapokuwa uwanjani.

Anasema mara nyingi mchezaji mwenye uwezo kisoka, hasa yule ambaye amefikia hatua ya kuchezea timu ya Taifa lake, anahitaji kuwa na ujuzi ili kumsaidia kufanya uamuzi wa haraka na wenye tija pale anapokuwa uwanjani kwa manufaa ya timu yake.

Anasema tatizo hili pia limekuwa sugu kwa sababu wachezaji wengi wanajiunga na klabu mbalimbali vya soka hapa nchini, kwa sababu wana vipaji vya kucheza mpira lakini hawapati ujuzi wowote wa ziada katika umri mdogo wakati wakianza kucheza soka.

Jamal Malinzi, Rais wa Shirikisho la soka Tanzania, akizungumza na JAMHURI anasema wao kama wasimamizi wakubwa wa soka ndani ya nchi tayari wana mipango ya muda mrefu na mfupi wa timu hiyo kuwa timu ya Taifa katika siku zijazo.

Anasema timu ya vijana ya Serengeti Boys inatarajiwa kuweka kambi ya wiki mbili nchini Korea Kusini inakotarajiwa kucheza mechi tano za kirafiki za kimataifa na timu kutoka nchi mbalimbali.

“Tutahakikisha vijana hawa wanakuwa na kambi ya pamoja kila baada ya miezi mitatu; hii yote italenga kuhakikisha kuona tunaendelea kuwa na vijana hawa bila ya kuwapoteza,” anasema Malinzi. 

Anasema timu hiyo iliyoundwa kwa kipindi cha miaka miwili imeonesha uhai mkubwa kwenye mashindano ya vijana, imetokana na zao la vijana kutoka kwenye Copa Coca na Airtel Rising Star.

Anasema pamoja na majukumu mazito yanayolikabili Shirikisho hilo lakini watahakikisha vijana hao wanakuwa salama katika kuhakikisha vipaji vyao vinalindwa kwa manufaa ya Taifa katika siku za usoni.

“Nia yetu ni kuwaona vijana hawa wanakuwa wawakilishi wetu katika timu ya wakubwa Taifa stars katika miaka ijayo na tuna imani kubwa kuwa vijana hawa watatufikisha mbali katika mashindano mbalimbali katika bara hili,” anasema Malinzi.

Serengeti Boys imeshindwa kukata tiketi ya Fainali za Afrika mwakani Madagascar baada ya kufungwa 1-0 na wenyeji Kongo Brazzaville Uwanja wa Kumbukumbu ya Alphonse Massamba-Debat mjini Brazzaville katika mchezo wa marudiano hatua ya mwisho ya mchujo.

Kwa matokeo hayo, Serengeti Boys ilitolewa kwa bao la ugenini baada ya sare ya jumla ya 3-3, kufuatia kushinda 3-2 katika mechi ya kwanza wiki mbili zilizopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wachezaji wa Serengeti Boys iliyo chini Mkurugenzi wa Ufundi, Mdenmark Kim Poulsen, Kocha Mkuu, Bakari Shime na Kocha wa makipa na Muharami Mohammed ‘Shilton’ wamesikitishwa na matokeo hayo mjini Brazzaville.

Hii inakuwa mara ya pili Serengeti Boys kuikosa tiketi ya fainali za Afrika baada ya mwaka 2005 kufuzu fainali za Gambia, kwa kuzitoa Rwanda, Zambia na Zimbabawe, lakini ikaenguliwa kwa kashfa ya kumtumia mchezaji aliyezidi umri, Nurdin Bakari, aliyekuwa anachezea Simba SC wakati huo.

By Jamhuri