Mpita Njia, maarufu kama MN, ameendelea kufurahishwa na pilikapilika za mapokezi ya wageni wa nchi mbalimbali wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). MN ameshuhudia pilikapilika za usafi katika maeneo ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam na kipande cha Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Clock Tower ama Mnara wa Saa uliopo eneo la Mnazi Mmoja unaounganisha barabara za Uhuru, Nkrumah na Samora umekuwa wa kihistoria, historia ambayo msingi wake ni uamuzi wananchi wa Dar es Salaam kuujenga kwa ajili ya kumbukumbu ya mji huo kuwa mji mkuu, Desemba 11, 1961.

Kwa hali yoyote, waliofikia uamuzi wa kujenga mnara huo hawakuwa na kasoro zozote katika maarifa ama elimu yao, hasa ikizingatiwa kuwa wakati nchi ikielekea kupata uhuru wake na hata baada ya kupata uhuru huo miaka michache iliyopita haikuwa na wasomi wengi.

Lakini kwa uchache wao, wasomi hao walifanya ubunifu wa namna bora ya kupendezesha mji wa Dar es Salaam kama ulivyojulikana baada ya uhuru. Miongoni mwa hatua walizochukua ni kujenga mnara huo wa saa ambao bila shaka, pamoja na mambo mengine, kulilenga kuwawezesha wananchi kujua mwenendo wa majira ya siku.

Hata hivyo cha kushangaza, miaka takriban 57 ikiwa imepita nchi ikiwa na wasomi lukuki, nguvu kazi ya kutosha, ikiwa huru na yenye bajeti inayokua, watendaji katika Idara ya Mipango Miji katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wamekuwa watu wasioeleweka.

Hawaujali mnara huo, saa ni mbovu, haifanyi kazi. Mnara ni mchafu, ukiwa umepauka kwa kutopakwa rangi miaka nenda miaka rudi. Jambo la kushangaza, watendaji hawa na viongozi wao wakuu ngazi ya mkoa wamekuwa mahodari wa kufanya shughuli nyingine za uhamasishaji jamii, lakini hii inayowahusu wao wenyewe, angalau kuonyesha namna wanavyomudu kuenzi kazi za wasomi wetu wa zamani imewashinda kabisa.

Bila shaka watendaji wa namna hii ni watu waliokuwa na nia ya kutafuta ajira tu na si kutumia maarifa na elimu yao kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa katika nyanja mbalimbali na watendaji wengine watangulizi serikalini, mithili ya hao wa awamu ya kwanza, chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Kubwa zaidi, inashangaza kumsikia mkuu wa mkoa akitangaza watu wasiooga kutofika mjini wakati wa vikao vya SADC lakini pengine hajui kuwa mji ama mkoa anaouongoza ni mchafu, tena uchafu wenyewe upo jirani na Ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Clock Tower, ambako wengi wa watendaji wa ofisi hiyo hupita hapo wakiwa kwenye magari yao au hata kwa kutembea wakati wa shughuli zao mbalimbali. Tunahitaji wafadhali kufufua Clock Tower ya Mnazi Mmoja? Aibu!

By Jamhuri