Wiki jana nilikumbuka baadhi ya mabomu mabaya zaidi duniani, ambayo Tanzania pia tunajitahidi kuyatengeneza japokuwa mataifa makubwa yanayotengeneza silaha kali, hayataki kuja kutuchunguza ili tuwekewe vizingiti vya kiuchumi.

Wiki yote hii nimekuwa nikipokea ujumbe mfupi katika simu, nikiambiwa mabomu yale ni baadhi tu ya mengine ambayo sikuyachambua kiundani athari zake. Nakubaliana nao lakini pia mmoja wao alisema kama kuna bomu baya la nyuklia ambalo ni kubwa kuliko lile la kule Korea Kaskazini tena la masafa marefu, basi ni hili la mchanganyiko maalum wa vijana na elimu yao na ajira zisizopatikana.

 

Mtoa maoni alisema vijana wengi wasio na ajira wameamua kutumia dawa za kulevya, bangi na kuwa na hisia za mafanikio ya muda mfupi, mafanikio ya kufikirika yasiyo ya kufanya kazi, matumaini ya kutendewa badala ya kutenda, matumaini ya maisha bora kuliko bora maisha waliyonayo sasa, ndoto na matumaini hayo yakibadilika matokeo yake ni kwenda kinyume na maadili ya kibinadamu.

 

Wenye mioyo laini watafikiria suala la waganga wa kienyeji, ambao ni bomu jingine jipya, watakwenda huko na kutakiwa kuwatafuta wenye ulemavu wa ngozi, ama watoto wadogo wasio na hatia katika nchi hii na kuyakatisha maisha yao kikatili wakiaminishwa kufanikiwa kimaisha.

 

Wenye mioyo migumu wataingia mstari wa mbele kwa namna yoyote ile, iwe kwa maandamano ya kisiasa, asasi za kiraia ambazo pia zimetokana na ugumu wa maisha, au kuanzisha kajeshi maalum ka kanda kwa muda maalum, iwe usiku, au mchana, iwe barabarani ama msituni, iwe nyumbani kwa mtu, au ofisini, ikiwezekana hata mochwari ilimradi wapate mkate wao wa siku.

 

Hili ni bomu linalotokana na mchanyato wa elimu duni, ajira na njaa ukijumlisha na mchanganyiko wa dawa za kulevya na bangi na siasa za matumaini, kijacho mbele ni taifa lisilo na mategemeo na matumaini.

 

Tunazalisha waganga wengi wa kienyeji ambao wengi wao ni matapeli, waganga vijana waliostahili kushika jembe na kulima, waliostahili kuwa viwandani wakishinda wakipiga ramli za kisanii, na kibaya zaidi ni kazi yao kukubaliwa kisheria na jamii.

 

Barua yangu ya leo, ni mwendelezo tu wa barua ya wiki jana ambayo maoni ya watu yamenisukuma kuandika tena baada ya kuona nimeguswa na hali hii ya vijana kuachwa kando, huku wakiwa hawana matumaini ya maisha ya kesho, vijana ambao tulidhani ni taifa la kesho, vijana ambao tulidhani tukiwekeza vizuri kama taifa, watakuwa na manufaa kwa uzee wetu lakini matokeo yake ni tofauti na fikra zangu za kipumbavu ambapo nawaona vijana kama maadui wangu wa uzeeni.

 

Ningelipenda baadhi ya mawazo ya watu wanaoliona hili kama ni tatizo, wasibezwe ama kuchukuliwa kama wanasiasa ama viongozi wanafiki. Wanafiki ni wale wanaopingana na hoja hii, wavae miwani itakayowasaidia kuona mbali na jinsi ambavyo tunaweza kupingana na hili kama taifa, tuwaangalie vijana wenye uchu na maisha bora, tuwaangalie vijana kama nguvu kazi ya kesho, wazee wa kesho na walimu wa wenzao wa kesho, yaani wajukuu zetu.

 

Lakini kibaya zaidi niliambiwa kuwa na mimi nashuhudia hili kwamba vijana hawa wako kidotcom zaidi, kwamba hata hiyo nidhamu ya kuangalia hawana ukiachilia mbali nidhamu ya kufundishwa.

 

Wengi wao sasa hivi wanajiona wako sawa na wazazi wao, wanaweza kuwajibu watakavyo na wanaweza kuchukua uamuzi wautakao bila kujali athari za baadaye.

 

Hii ndiyo Tanzania ninayoijua mimi, Tanzania ya sasa, Tanzania ambayo haina mwenyewe, awe kiongozi ama raia wa kawaida, awe mtumishi wa umma ama aliyejiajiri mwenyewe. Kutojali nidhamu na kukubali kubadilika kwenda na wakati ambao tunahitaji kujituma zaidi kwa ajili ya maendeleo, tumeugeuza wakati huo ambao ni ukuta katika malumbano ya kisiasa, kutumia headphones kusikiliza miziki, kuchati, bbm, whatsup, facebook na skype.

 

Naipenda Tanzania, niko tayari kutoa ushauri wa bure, naijua Tanzania yetu ambayo tulikuwa tukipata ajira viwandani na mashambani hata tukimaliza darasa la nne, naijua Tanzania ya kisomo cha watu wazima ili kuondoa adui ujinga, naiona Tanzania yenu ya mwanafunzi wa darasa la saba asiyejua kusoma wala kuandika lakini anafaulu mitihani, Tanzania isiyo na mashamba wala viwanda, Tanzania iliyosahau nguvukazi ya kesho, Tanzania inayotaka amani ya nadharia bila kuzuia vitendo tarajiwa.


Zamani mwisho wa hotuba za mwenyekiti wa chama chetu alikuwa anasema, Tanzania hoyee, TANU hoyee, vijana hoyee, Azimio la Arusha hoyee, zidumu fikra za chama, zidumu!!

 

Leo sijui nisemeje mwisho wa barua yangu, labda niseme E Mola tuepushe na KIKOMBE HIKI.


Wasalaam,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.


 

By Jamhuri