Baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu, mwanamuziki nguli wa miondoko ya reggae hapa nchini, Ras Inno Nganyagwa, anarudi tena jukwaani kwa kuitambulisha rasmi bendi yake.

Ras Inno, ambaye ndiye aliyeshika mikoba ya Justin Kalikawe baada ya nguli huyo kufariki duniani, wakati huo alionekana kuwa kizazi kipya cha muziki wa reggae.


Baada ya kutamba kwa muda mrefu, ghafla Ras Inno akawa kimya na muziki wa reggae ukawa kama upotea masikino mwa watu. Lakini sasa, Ras Inno ameibuka na kutaka kuurejesha muziki huo katika hadhi yake.


Katika mahojiano na JAMHURI hivi karibuni, Ras Inno amesema ataitambulisha rasmi bendi yake katika onesho mahsusi litakalofanyika katikati ya mwezi ujao, jijini Dar es Salaam.


Amesema nia ya kuanzisha bendi hiyo ni kuongeza ufanisi katika kazi zake za muziki.

“Huu ni mwanzo wa kutimiza mikakati yangu ya kurudi kwenye fani, baada ya kujiweka pembeni kwa muda mrefu,” amesema.


Rasi Inno ambaye pia ni mtafiti wa masuala ya kijamii na mwandishi wa safu mbalimbali katika magazeti tofauti ya hapa nchini, anabainisha kwamba baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu ameweza kubaini upungufu kadhaa.


“Ukimya wangu wa muda mrefu una sababu kadhaa zikiwamo za kibinafsi kimaisha, lakini muda niliokuwa nje ya ulingo, nimeyasoma vyema mazingira yanayoukabili mtindo wa reggae hivyo naamini ninayo dozi ya kuutibu.


“Hivyo nimeamua kubuni mikakati mbadala na namna bora ya kurudi jukwaani kwa dhamira ya kuipaisha reggae, pia kukonga nyoyo za mashabiki wangu ambao hawajaniona jukwaani kwa muda mrefu,” amesema.


Pia anasema onesho hilo litaitambulisha taasisi yake aliyoiunda, itakayosimamia kazi zake pamoja na miradi aliyoibuni, yenye lengo la kuupromoti muziki wa reggae ili vijana wengi wavutike na kujitosa kwenye miondoko hiyo, na hivyo kuibua vipaji vipya na kupanua wigo wa idadi ya wanamuziki wa reggae.


Katika onesho hilo atacheza nyimbo zake za zamani zilizompatia umaarufu miaka ya nyuma ukiwamo wimbo wa ‘Gila’ kutoka albamu yake ya Money-Pesa (1994), pamoja na nyimbo mpya zilizomo kwenye albamu yake mpya ya ‘Kwa Nini’.

 

Atasindikizwa na kundi la kizazi kipya cha reggae, Bendi ya Fimbo, inayopiga miondoko ya asili, mwimbaji wa muziki wa Kiinjili, Annette Mwasambogo, na DJ maarufu wa disco la reggae hapa nchini, Aluta Warioba, kutoka Times FM.


By Jamhuri