Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Serikali imesema Miliki Ubunifu ni nyenzo muhimu katika kuendeleza na kukuza uchumi na biashara nchini.

Hayo yameelezwa leo Mei 9, 2024 na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamisi Mwinjuma wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Miliki Ubunifu Duniani yaliyoandaliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).

Amesema serikali inauhakika Miliki Ubunifu itaondoa changamoto na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja nchini.

“Serikali imeshaweka mazingira bora na wezeshi katika suala zima la biashara kwa kutumia Miliki Ubunifu kwani tunaamini maendeleo ya nchi yanategemea Miliki Ubunifu kwa ukuaji wa uchumi,” amesema Mwinjuma.

Ameongeza kuwa serikali kwakushirikiana na Taasisi nyingine itawezesha ukamilikaji wa sera ya Miliki Ubunifu ambayo italeta mwanga katika kusimamia mwongozo wa Haki Miliki Tanzania.

Hata hivyo, Mwinjuma amesema anatambua kazi nzuri inayofanywa na BRELA katika kuwaimarisha wafanyabiashara na wenye makampuni kutekeleza shughuli zao za kimaendeleo.

“Tutahakikisha ifikapo mwaka 2030 kunakuwa na uwiano wa maendeleo duniani kwa kutumia Miliki Ubunifu,” amesema Mwinjuma.

Ameiagiza BRELA na Cosota kushirikiana kutoa elimu ya Miliki Ubunifu kwa jamii ili kujenga uelewa wa namna ya kulinda kazi hizo ili wabunifu waweze kunufaika zaidi

Awali Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa BRELA Godfrey Nyaisa amesema masuala ya ubunifu yatasaidia kusukuma gurudumu la maendeleo.

Amesema hivi sasa wana mpango wa kuanzisha programu ya Miliki Ubunifu katika vyuo vyote nchini lengo ni kuendeleza ubunifu.

Nyaisa amesema nchi nyingi zinaendelea duniani kwa sababu ya kueneza miliki bunifu sehemu mbalimbali ndani ya nchi zao.

Mwenyekiti wa bodi ya ushauri BRELA, Profesa Neema Mboya amesema Maadhimisho hayo ni muhimu kuendelea kushereherekewa nchini kwani yanatoa fursa ya kukutanisha wadau mbalimbali na kuweza kujadiliana, kujifunza na kupata fursa ambazo zitasaidia kukuza bunifu za wabunifu nchini.

Amesema kufuatia maboresho yanayofanywa ndani ya BRELA yamepelekea kupokea wageni wengi kuja kujifunza wakiwemo Burundi pamoja na Sudan kusini.

By Jamhuri