Nianze kwa kuomba radhi kwa kutoonekana wiki jana kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wangu, nia ni moja na tuko pamoja katika kufanikisha mambo muhimu kwa jamii yetu iliyoparaganyika kimaadili, kisiasa na kiuchumi.

Wiki juzi nimepata maoni mengi kwa kutaka kuwa mheshimiwa mbunge, nawashukuru sana, vilevile wapo walionitaka nisiwe mwanasiasa kwa kutumia maneno mengi ya kisanii na undugu, wote naupokea ushauri wenu hata yule aliyesema niache mbwembwe niwahukumu moja kwa moja ninaowalenga.


Jamani, naomba mkumbuke kuwa umri wangu ndiyo unaonisuta kuanza na mambo ya dotcom, nimeona mengi nimekula chumvi nyingi, nimekutana na mambo mengi kwa hiyo sina budi kuwa na kumbukumbu ya mambo ya kiutu-uzima na hekima ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.


Wanangu, tumesikia Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani amefanya uamuzi mgumu wa kujiuzulu nafasi yake ya upapa. Kwa umri wangu sijasikia jambo hili kwa muda mrefu, na pengine niseme sijawahi kusikia kabisa.


Huyu kajiuzulu kwa sababu ambazo kazitaja kama ni shinikizo kwake kuachia ngazi. Mojawapo ya sababu zake ni kushindwa kukabiliana na mabadiliko kutokana na nguvu alizonazo kama Papa. Pili ni umri wake kwenda harijojo na kuona maovu yakifanyika na kushindwa kuyakabili kwa wakati kama kiongozi mkuu wa kanisa.


Leo ninaandika barua hii nikiwa na nguvu ya kutamka kuwa tunahitaji kiongozi awe rais, au wa namna yoyote aweze kuchukua uamuzi wa Papa anapoona mambo yanakwenda mrama ndani ya utawala wake.


Huu si utamaduni wetu japokuwa wapo walioweza kuthubutu kufanya hivyo. Namkumbuka Mwalimu Nyerere aliwahi kujiuzulu uwaziri mkuu kwa nia njema kwenda kuimarisha chama na nafasi yake akamwachia Rashidi Kawawa. Namkumbuka Ali Hassan Mwinyi alijiuzulu uwaziri wa Mambo ya Ndani kutokana na kashfa ya mauaji kule Shinyanga.


Nawafahamu viongozi wengine ambao wameweza kujiuzulu, iwe kwa nia ya kuchunguzwa, tuhuma, kushindwa kazi, kushindwa kwenda sanjari na viongozi wengine, kukwepa unafiki na kadhalika. Hawa wote wana nia njema katika nafasi zao walizojiuzulu, hili halina ubishi na wala halistahili kujadili kwa kuwa mfano mzuri ni wa Papa.


Nchi za Afrika zimegubikwa na viongozi wanafiki na wasioweza kuhimili majukumu wanayokabiliwa nayo, na hii inatokana na umaskini uliokithiri wa kujitakia kutokana na wao kushindwa kuwa na moyo wa uthubutu katika kuacha wengine wajaribu hata kama wanaowaachia watafanya kazi ileile ambayo imefanywa na huyo aliyejiuzulu.


Nimeamua kuandika barua hii, nikijaribu kuvuta kumbukumbu yangu kwa viongozi mbalimbali waliowahi kujiuzulu Afrika na Tanzania kwa ujumla wake. Najiuliza, tuna viongozi wangapi walioweza kuwa na moyo wa uthubutu kama huo na wakaamua kukaa pembeni kuwapisha wengine waweze kufanya kazi?


Uzoefu unaonesha yeyote mwenye moyo wa uthubutu ndiye kiongozi bora, kama yeye anaweza kuthubutu basi anayemwongoza hawezi kuacha kujiuzulu anapofanya kosa chini ya mtawala mwenye uthubutu. Uthubutu ni moyo wa kizalendo zaidi kuliko demokrasia.


Leo nathubutu kuongeza pale alipoachia kusema Mwalimu Nyerere katika Hoteli ya Kilimanjaro, kwamba tusimzungumzie mtu bali tuangalie tuna matatizo gani na katika uongozi wetu, tuwe na mtu atakayeogopwa kwa matendo yake, aogopwe kwa kusimamia sheria na aweze kusema hapana kwa jambo ambalo anaona si sahihi na ni baya kwa taifa.


Tunataka kiongozi wa mfano wa Papa atakayesema yeye ameshindwa na si kung’ang’ania madaraka hata kama yamemshinda, akaamua kuachia ngazi ili kupisha wengine wafanye.


Nimependa uamuzi wa Papa na ningependa tutumie hicho kuwa kigezo cha kiongozi katika nchi yetu, kwa kuwa tunaapa kwa kutumia Msahafu na Biblia tumwogope Mwenyezi Mungu katika utekelezaji wa kazi zetu kila siku.


Ningependa kumpendekeza rais lakini ni mapema mno. Naendelea kufanya tafakuri katika viongozi wetu ambao wana moyo wa uthubutu kama wa Papa na wanaweza kusema sasa inatosha anaona ni vema akawapisha wengine waendelee, kwa kuwa yeye ameshindwa, lakini wakifikia uamuzi huo tayari viongozi wengi watakuwa wametoka madarakani bila ridhaa kwa kuwa si utaratibu wetu.

Mzee Zuzu

Kipatimo.


By Jamhuri