Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Chalinze

MWENGE wa Uhuru Kitaifa umeingia Mkoa wa Pwani ukitokea Mkoa wa Morogoro ambapo utakagua, kuweka jiwe la msingi na kutembelea miradi 126 yenye thamani ya trilioni 8.536 .

Kati ya miradi hiyo 18 itawekwa mawe ya msingi, 22 itazinduliwa , 86 itakaguliwa katika umbali wa km1225.3.

Akipokea Mwenge wa Uhuru April 29, 2024 eneo la Bwawani kutoka kwa Mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Malima, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alieleza, mwenge utakimbizwa katika halmashauri Tisa na wilaya Saba .

Alieleza ,kati trilioni 8.536, bilioni 13.6 Serikali Kuu, Halmashauri za wilaya bilioni 2.3 ,nguvu za wananchi na wawekezaji trilioni 8.5 na wadau wa maendeleo bilioni 14.6.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali ya awamu ya sita kwa jitihada za makusudi za kutafuta fedha na kushirikisha wadau katika kuleta maendeleo na kwa kuweka mazingira bora kwa ustawi na ufanisi na sekta binafsi nchini” alisema Kunenge.

Alisema kwa kuzingatia ujumbe Mkuu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 ,Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa Taifa Endelevu ,mkoa unahimiza wanachi kushiriki uchaguzi kwa Amani na utulivu.

“Katika kutekeleza adhma ya utunzaji mazingira kwa kipindi cha 2023/2024 mkoa una malengo ya kupanda miti 13.500.000 hadi kufikia mwezi Juni 2024.

Kunenge alifafanua, hadi sasa jumla ya miti 8.884.938 imepandwa kwenye maeneo mbalimbali.

Wakati huo huo, Kunenge alikabidhi Mwenge huo kwa Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Halima Okash na kusema Bagamoyo utakimbizwa katika halmashauri ya Chalinze na Bagamoyo.

“Mwenge huu utaanzia halmashauri ya Chalinze, April 30 utakuwa halmashauri ya Bagamoyo miradi itakayopitiwa ni 29 yenye thamani ya bilioni 15.2.”alisema Okash.

Katika halmashauri ya Chalinze Mwenge umezindua barabara na ujenzi wa daraja Kwamela -Lukwambe uliogharimu milioni 365.975 ,upande wa daraja milioni 190.205 katika mwaka wa fedha 2022/2023 TARURA Bagamoyo kupitia fedha za mfuko wa jimbo.

Miradi mingine ujenzi wa shule ya awali na msingi ya Ridhiwani Kikwete, mradi uliotekelezwa kwa kutumia force account, ujenzi ambao ulitokana na shule ya awali na msingi Bwilingu A kuwa na msongamano wa wanafunzi wapatao 1984.

Pamoja na hayo umeweka jiwe la uzinduzi mradi tanki la maji Bwilingu, kuona uendelevu wa mradi wa redio katika kituo cha redio Chalinze FM 97.5 ,kukagua mradi wa huduma ya kijamii duka la dawa kwenye kituo cha afya Bwilingu na kuweka jiwe la msingi mradi wa afya kwa waraibu wa dawa za kulevya kituo cha afya Chalinze.

Please follow and like us:
Pin Share