Msanii Naseeb Abdul maarufu Diamond Platinumz jana amewasili katika ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa ajili ya mahojiano kutokana na tuhuma za kusambaza katika mitandao ya kijamii video isiyokuwa na maadili.

Msanii huyo anatuhumiwa kusambaza video inayomuonyesha akiwa katika faragha na mwanamke ambaye ni mzazi mwenzake, Hamisa Mobetto.

Siku ya Jumanne, Diamond alishikiliwa na Polisi Katika Kituo Kikuu cha Polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam, kufuatia kusamba kwa video hizo, ambapo alihojiwa kisha kuachiwa kwa dhamana na hati yake ya kusafiria ikishikiliwa.

Siku ya leo Alhamisi Msanii mwingine, Faustina Mfinanga ‘Nandy’ nae amefika katika ofisi za mamlaka hiyo, kwa ajili ya mahojiano baada ya kutuhumiwa kusambaza video iliyomuonyesha akiwa katika faragha na msanii Bilnass.

Nandy alifika katika ofisi za TCRA zilizoko mkabala na Barabara ya Sam Nujoma saa 5:48 asubuhi, huku Diamond akifika dakika 27 baadaye.

Diamond alisindikizwa na Said Fella pamoja na baadhi ya watu wa kundi la WCB.

1998 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!