Mkoa wa Geita ni miongoni mwa mikoa ambayo kuna migodi ya dhahabu, ambayo pia inahusisha matumizi ya kemikali bila kufuata masharti kama yalivyoainishwa na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Kumekuwapo na matumizi ya kemikali hatarishi katika mazingira bila kujali madhara yake kwa binadamu na mazingira.

Mwaka 2013 Mkoa wa Geita ulikuwa na viwanda vidogo vya kuchomea dhahabu vipatavyo 21. Viwanda vya uchenjuaji dhahabu (elution plants) vilianzishwa na watu mbalimbali bila kuangalia kama maeneo hayo yanaruhusiwa kujenga viwanda.

Mwaka 2013, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo wa Geita, Said Magalula, alitoa mwongozo wa kuhamisha viwanda vya kuchenjua dhahabu katika makazi ya watu na kupeleka katika maeneo ambayo yalitengwa kwa ajili ya viwanda.

Kuhamishwa kwa viwanda hivyo kutoka katika makazi ya watu kwenda kwenye maeneo maalumu, kulitokana na malalamiko ya wananchi juu ya athari za matumizi ya kemikali katika maeneo yao.

Maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli hizo ni Mpomvu na Nyanza Katundu.

Sheria ya Kemikali Na 3 ya mwaka 2003 kifungu cha 27, inasema kila mtu au kampuni inayojihusisha na kemikali ni lazima iwe imesajiliwa na kupewa cheti cha kufanya biashara hiyo. Kabla ya kupewa cheti hicho ni lazima akaguliwe na kuona iwapo anakidhi matakwa ya sheria kifungu 19 kama niliyoyataja awali.

Kutokana na matakwa hayo ya kisheria, Mkemia Mkuu wa Serikali alisajili kampuni ambazo zimekidhi vigezo vya kisheria baada ya kukaguliwa. Migodi ambayo imekaguliwa na kusajiliwa ni Tryphon John, Mpondi Co. Ltd, Seleman Malale, Gold Empire na Sifuni Mchome.

 

Utekelezaji wa agizo la aliyekuwa Mkuu wa Mkoa

 Viwanda vitatu vilihamishwa kutoka Geita Mjini na kupelekwa eneo lililotengwa la Mpomvu, eneo hilo liko nje kidogo ya mji wa Geita. Pia viwanda vilivyokuwa maeneo mtaa wa Nyanza Kitunda pia vilihesabiwa kuwa maeneo ya viwanda baada ya eneo hilo kuthibitishwa kuwa eneo la viwanda.

Mbali na kuwapo kwa sheria inayoelekeza matumizi ya kemikali, mkoani Geita hali ni tofauti kutokana na kuwapo kwa baadhi ya wamiliki wa migodi ya uchenjuaji dhahabu kutunza kemikali hizo kinyume cha sheria na kuwabebesha watu ambao hawana mafunzo ya namna ya kujikinga na madhara yatokanayo na kemikali.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kijijini hapo, waathiriwa wa kemikali – Malimi Kang’ongo (39) pamoja na Jackson Msengi (50) – wanasema wamepata matatizo wanayodhani yametokana na kutokuwa na vifaa maalumu vya kubeba kemikali.

Wameiambia JAMHURI, maradhi hayo waliyopata yametokana na kubeba mifuko yenye kemikali mali ya Richard Kasubi, huku wakisema hawapati msaada wowote kutoka kwa mmliki huyo licha ya kuwapa shilingi laki mbili na elfu kumi kila mmoja kwa ajili ya matibabu.

Akizungumza na JAMHURI, Kasubi amesema anatambua tatizo la vijana hao kubabuka ngozi wakati wakipakua kemikali, huku akikana kuwa sehemu ya waajiriwa wake.

“Ni kweli hawa vijana nimewaona walivyobabuka lakini sikuwaajiri mimi…maana ninapoagiza mzigo huwa nalipia gharama zote za kupakia na kupakua mzigo unapofika ghalani kwangu.

“Wanaopakua mizigo walishapewa elimu ya upakuaji kemikali…sasa nilishangaa na wao kuwapa kazi watu wasio na elimu ya kupakua mizigo kama huo…ndiyo maana nasema nimefanya fadhila tu hata kuwapa hela ya matibabu…hivi mtu unapompa jembe akalime akijikata nani wa kulaumiwa?’’ alihoji Kasubi.

Taarifa zaidi zinasema, Desemba 8, 2016, walipewa kazi ya kupakua kemikali za kuchenjulia marudio ya dhahabu aina ya ‘Lime’ mifuko 600, kwa ujira wa Sh 50, 000/-.

Wapagazi hao wamesema walipofika majumbani mwao na kupata maji ya kuoga walianza kuhisi miwasho na maumivu makali sehemu zote ambazo walikuwa wanagusisha mifuko ya kemikali hizo.

“Desemba 10, tulikwenda kwenye zahanati ya Nyarugusu ambako tuliambiwa tutumie kwanza dawa tulizokuwa tumenunua dukani zikiisha ndiyo turudi kwa uchunguzi zaidi, ambapo tulifanya hivyo na kupitia kituo kidogo cha polisi Nyarugusu ambako tulipewa PF3 huku polisi wakishauri twende katika hospitali teule ya Mkoa wa Geita kwa uchunguzi zaidi,’’ amesema Msengi.

Akizungumza na JAMHURI, Malimi Kang’ong’o amesema awali mmiliki wa ghala hilo alikuwa na majibu yasiyoridhisha na alifikia hatua ya kuwakashifu walipomueleza matatizo yaliyotokana na kazi ya kubeba kemikali.

“Siku alipopigiwa simu na uongozi wa kitongoji na kijiji alikuwa na majibu yasiyoridhisha kwani alituambia kwamba mtu akikupa jembe ukalime ukijikata ni nani alaumiwe? Lakini baada ya waandishi kumtafuta ametutumia lakini mbili kwa ajili ya matibabu,’’ amesema King’ong’o.

Kwa sasa watu hao wanatumia dawa walizopewa katika hospitali teule ya Mkoa wa Geita, huku wakiendelea kuomba msaada ili kwenda kwenye hospitali kubwa kuchunguza kiwango cha madhara ya kemikali hizo katika miili yao.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kiomboi, Juma Mpinga, amesema alipoletewa malalamiko na wananchi hao alikutana na mwenyekiti wa kijiji na kumpigia mmiliki wa kemikali hizo.

‘’Kwa kweli baada ya kuwaona hawa wananchi nilishtuka sana na kuamua kumtaarifu mwenyekiti wa kijiji, Daniel Mwigulu, ambaye alimpigia simu Kasubi na katika maongezi yake alionesha kutoguswa na tukio hilo maana mwenyekiti alikuwa ameweka kipaza sauti,’’ amesema Mpinga.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji, Daniel Mwigulu, mbali na kuthibitisha kuwapo kwa tukio hilo, amesema baada ya mtuhumiwa kufika ofisini kwake aligeuka mbogo huku akidai kutowatambua vijana hao akisisitiza kuwa waliajiriwa na vijana wake aliokuwa amewapa kazi ya kupakua kemikali hizo kutoka kwenye gari na kuziingiza kwenye ghala.

Mwenyekiti huyo ameziomba mamlaka zinazohusika kufanya ukaguzi mara kwa mara kwa wamiliki wa migodi na maghala ya kutunzia madawa ya kuchenjulia marudio ya dhahabu, ili kujua kama kemikali hizo zinahifadhiwa kwa mujibu wa taratibu.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Nyarugusu, Thobias Ikangala, mbali na kukiri uwepo wa wananchi hao walioathiriwa na kemikali, amesema baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa mwenyekiti wa kijiji alimuagiza kuwapa mwongozo wa kimatibabu wananchi hao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanapatiwa fomu namba 3 kutoka Polisi (PF3).

“Ni kweli hili tukio lipo na nilichokifanya mimi baada ya kupata taarifa hizo nilimweleza mwenyekiti awasaidie hao watu wafike polisi na kupatiwa PF3 ili waende Geita kufanyiwa uchunguzi…niombe sasa ofisi ya mkemia mkuu ifungue tawi lake hapa Geita,” amesema Ikangala.

 Akizungumza na JAMHURI, Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof Samweli Manyele, amesema huduma zitolewazo na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali hufanyka katika vituo vya Makao Makuu Dar es Salaam, Kanda ya Ziwa ambapo maabara ya Kanda iko Mwanza, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini – Maabara ya Kanda ipo katika Jiji la Mbeya.

Maabara nyingine ni ile ya Kanda ya Kaskazini iliyoko Arusha, Kanda ya Kusini, iliyoko Mtwara.

Prof Manyele amesema kemikali zote ziingiazo na kutoka nchini, usafirishaji wa kutoka eneo moja kwenda jingine kunahitajika kibali kutoka wakala wa maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika vituo vilivyotajwa.

“Kutokuwa na vibali vinavyoruhusu usafirishaji, utumiaji, utunzaji, uagizaji na usambazaji  ni kosa kisheria na adhabu yake ni kifungo au faini kama ilivyoainishwa kwenye sheria ya Usimamizi na udhibiti wa Kemikali za Majumbani na viwandani sura 182 ya mwaka 2003,” amesema Prof Manyele.

Mkemia Mkuu amesema jukumu la wananchi ni kufuata sheria na kanuni zake ili kuzuia madhara ya kemikali katika meneo yao na wanapoona ukiukwaji wa sheria wanapaswa kutoa taarifa Polisi au Ofisi ya kanda iliyo karibu.

Prof Manyele amesema kwa sasa ofisi yake haina mpango wa kufungua ofisi nyingine mkoani Geita na badala yake ofisi ya Kanda iliyoko Mwanza ndiyo iendelee kutumika.

“Umbali wa kutoka Geita hadi Mwanza ni kilometa 70, hata hivyo gharama za kuendesha ofisi yenye uwezo wa kufanya uchunguzi na kusimamia biashara za kemikali, sheria ya vinasaba na maabara za kemia ni gharama kubwa na zinahitaji rasilimali watu na fedha.

“Kwa sasa Serikali haina uwezo wa kufungua ofisi katika Mkoa wa Geita. Hata hivyo bado kuna nafasi katika siku za usoni iwapo Serikali itaruhusu na uchumi utaruhusu kufungua ofisi kama hiyo ili kusogeza huduma kama hii karibu na wananchi,’’ amesema Prof Manyele.

Naye Katibu Mkuu wa chama cha wachimba madini Mkoa wa Geita, Golden Hainga, mbali na kukiri uwepo wa matumizi holela ya kemikali kwenye maeneo ya migodi, anasema wameanza kujipanga ili kutoa elimu kwa wananchi juu ya athari zitokanazo na kemikali.

Afisa Mazingira wa Wilaya ya Geita, Hellen Eustace, ameahidi kufuatilia suala hilo pamoja na kuchukua hatua iwapo atakuta kuna uvunjwaji wa sheria ya mazingira namba 24 ya mwaka 2004.

Akizungumza kwa niaba ya Ofisa Madini Mkazi kanda ya Geita, Mhandisi Ally Maganga, anasema idara ya madini imekuwa katika mikakati mbalimbali ya kutoa elimu kwa wahusika ili kutambua madhara ya uendeshaji wa shughuli zao.

“Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na kanuni zake inabainisha wazi taratibu za kuzingatia wakati wa uendeshaji wa shughuli za madini, kwa mfano kanuni ya namba 8 ya madini inazuia mchimbaji mdogo kutumia kemikali ya ‘Cyanide’ kuchenjua madini pasipo kuruhusiwa na Mkaguzi Mkuu wa Migodi,” amesema Maganga.

‘Sulphuric acid’ na ‘Nitric acid’ – kemikali hizi huweza kuunguza ngozi na hata kusababisha kifo. Pia kemikali hii husababisha muwasho kwenye macho, ngozi, pua, koo, kusababisha kukohoa na kichwa kuuma.

‘Folluculant’ na ‘Borax’ – kemikali hii husababisha muwasho kwenye macho, ngozi, pua, koo, kusababisha kukohoa na kichwa kuuma.

Madhara ya kemikali hizi yanaweza kuzuiwa kwa kila anayejihusisha na kemikali hizo kuvaa vifaa vya kujikinga (Proper chemical PPE) vilivyo madhubuti.

Geita ni mkoa wenye migodi mingi midogo na ya kati katika Kanda ya Ziwa. Mkoa unayo migodi 226 midogo yenye kutumia zebaki, migodi 100 ya kati inayotumia sayanidi na mgodi mmoja mkubwa.

Hii inaufanya mkoa huu kuwa muhimu zaidi kwa uchumia wa wananchi, Taifa na jamii kwa ujumla. Faida hii inaleta changamoto katika matumizi ya kemikali.

1358 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!