Siku kama ya leo, miaka 38 iliyopita, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), likishirikiana na wapiganaji wa Uganda waliokuwa wanapambana dhidi ya majeshi ya Uganda waliteka Jiji la Kampala na kusambaratisha majeshi ya Idi Amin.
Serikali ya Amin ilianguka na yeye mwenyewe kukimbilia uhamishoni nchini Libya, na baadaye akahamia Saudi Arabia ambako aliishi hadi alipofariku dunia mwaka 2003.
Miaka 38 ni mingi kwa namna nyingi tu. Muda mrefu kama huo unapopita tangu kutokea tukio muhimu la kihistoria kama Vita ya Kagera, zipo athari zinaanza kujitokeza. Athari mojawapo ni ya kusahau maana ya vita.
Ni nadra vita itokee popote ulimwenguni ikahusishwa na jambo jema. Ni tukio ambalo siku zote huleta madhara makubwa, na madhara hayo huendelea hata baada ya tukio lenyewe kwisha.
Majeshi ya Idi Amin yalipovamia Mkoa wa Kagera mashambulizi ya kwanza kutoka JWTZ yalifurumusha wavamizi na kuwarudisha nchini Uganda. Ni kwenye hatua ya pili ya mashambulizi ndipo JWTZ ilivuka mpaka wa Uganda na kuendeleza vita kwenye ardhi ya Uganda. Lakini hata kwenye ile hatua ya awali, tayari hasara za vita zilikuwa zinakadiriwa kuigharimu Serikali ya Tanzania kiasi cha dola milioni moja za Marekani kwa siku.
Ingawa si rahisi kukadiria gharama halisi ya vita, ni wazi kuwa gharama ilikuwa kubwa. Matokeo yake ni kuwa kasi ya kukua kwa uchumi wa Tanzania iliporomoka kuanzia mwaka 1980 hadi mwaka 1983 ilipoanza kukua tena.
Athari za vita si za kiuchumi tu. Raia wengi wa Kagera waliuawa na wanajeshi wa Uganda walipovamia eneo hilo. Kwa mujibu wa tovuti inayoitwa FindTheData vifo vya raia Watanzania vinakadiriwa kukaribia 1,500 wakati vifo vya raia wa Uganda vinakadiriwa kukaribia 500.
Hatufahamu idadi ya wanajeshi waliopoteza maisha pande zote mbili, lakini haihitaji kupata taarifa sahihi kufahamu kuwa wanajeshi wengi walipoteza maisha kwenye vita hiyo.
Vita hiyo pia ilisababisha majeruhi kwa pande zote mbili, baadhi yao wanaoishi hadi leo na athari za majeraha yao.
Nchi ambazo zimekuwa zinashiriki vita mbalimbali kwa vipindi virefu, mathalani Marekani, ni nchi ambazo zina kundi kubwa la wanajeshi wastaafu wanaougua magonjwa ya akili yanayohusiana na athari za kushiriki vitendo vya kuua binadamu wengine, au kushuhudia kwa muda mrefu binadamu wakifa.
Imani ya baadhi ya dini kuwa binadamu tunaumbwa wema ni suala ambalo linajidhihirisha kwa kuangalia jinsi gani kushuhudia ukatili kwa muda mrefu kunavyomwathiri mwanadamu. Ipo theluthi ndogo sana ya binadamu ambayo haiathiriki kwa kushuhudia au kushiriki kwenye ukatili, lakini wengi wetu hatuwezi kuvumilia hali hii kwa muda mrefu.
Lakini pamoja na athari hizi za wazi za vita, inaelekea kuwa miaka 38 ya vita inaanza kufifisha kumbukumbu zetu juu ya mabaya ya vita. Na hii inawezekana inatokea kwa sababu ingawa wapiganaji wa Tanzania wameshiriki mapigano kwenye Vita vya Ukombozi Msumbiji, uvamizi wa Kisiwa cha Anjouan, na mapigano dhidi ya waasi wa DR-Congo hivi karibuni, ni kwenye vita ya Kagera pekee ndipo raia waliweza kushuhudia athari mbaya za vita.
Kwa sababu hii inawezekana kuwa ni raia wenzetu wa Kagera tu ambao watakuwa wa mwisho kuunga mkono nchi yetu kutumbukia kwenye vita.
Inavyoonekana hapa ni kuwa tusiyoyaona machoni tunayasahau haraka na miaka 38 inatosha kabisa tusahau kuwa vita siyo rumba.
Katika mifumo iliyopo ya kuendesha nchi kwa kawaida ni wanasiasa wanaoamuru nchi kuingia vitani. Bila shaka kuna mazingira ambayo nchi inalazimika, itake isitake, kuingia vitani. Lakini yapo mazingira ambayo wanasiasa wanakuwa na haraka sana ya kupigana vita bila kuangalia njia nyingine ambazo zinaweza kuleta suluhisho na kuepuka vita.
Miaka ya hivi karibuni Tanzania na Malawi zimeingia kwenye mgogoro wa mpaka wao; mgogoro ambao umeendelea kwa muda mrefu. Malawi inadai sehemu yote ya Kaskazini ya Ziwa Nyasa (wao wanaliita Ziwa Malawi) ni eneo la Malawi, wakati Tanzania inadai kuwa sehemu ya ziwa hilo ni eneo la Tanzania.
Wakati majadiliano kati ya serikali hizi mbili yaliyoshirikisha msuluhishi yakiendelea, raia wa pande zote mbili wamekuwa wakipandisha jazba kuashiria kuwa yasiyowezekana kwa mazungumzo yamalizwe kwa vita.
Lakini haikuwa raia tu walioanza kutangaza utayari wa Tanzania kuingia vitani. Baadhi ya viongozi nao walisema Tanzania ipo tayari kupigana vita. Jazba ya vita ilizimwa tu Rais Jakaya Kikwete alipotamka kuwa Tanzania haitapigana vita na itatafuta suluhisho ya kidiplomasia.
Miaka kadhaa iliyopita Tanzania na Rwanda nazo ziliingia kwenye malumbano ya kisiasa na kusababisha viongozi wa nchi hizi mbili kufikia hatua ya kutoelewana.
Malumbano yale yale ya vita yalianza kusikika baina ya raia wa nchi hizi mbili. Lakini, kwa bahati nzuri, yakaishia kuwa maneno tu ingawa ingewezekana kabisa kupigana vita dhidi ya Rwanda.
Kama lipo somo muhimu la kujifunza kutoka kwa uvamizi wa Idi Amin ni kuwa vita inatakiwa kuepukwa kwa kila njia. Ingekuwa vyema athari za vita likawa ni darasa mahsusi la somo la historia inayofundishwa kwa wanafunzi katika ngazi za awali kabisa. Watoto wote kwa kawaida yao wanamaliza tofauti zao kwa kutwangana makonde. Wakiachwa wakawa watu wazima na tabia hiyo tunajenga raia na viongozi ambao hawaoni njia nyingine ya kumaliza matatizo; ila kupigana.
Baada ya kudondoshwa kwa bomu la maangamizi kwenye miji ya Hiroshima na Nagasaki na kushuhudiwa maafa makubwa yaliyotokea, Robert Oppenheimer, mwanasayansi Mmarekani aliyeongoza jopo la wanasayansi wenzake kuunda bomu la kwanza la maangamizi alisema: “Wanafizikia wameibaini dhambi, na hilo ni somo ambalo hawatakiwi kulipoteza.”
Si sahihi kabisa kusema kuwa vita haileti jambo jema. Leo hii, kutokana na Vita ya Kagera, uhusiano wa serikali na watu wa Uganda na Tanzania upo imara kabisa. Kama wapo wanaofikiri kuwa nchi hizi mbili zinaweza kupigana tena vita itakuwa ni wale wanaochunguza matokeo ya kubadilika kwa enzi.
Kubadilika kwa enzi humfanya binadamu kusahau, na kusahau kunamrudisha binadamu kutenda makosa ambayo yatamletea athari.

By Jamhuri