Sasa tusaidie wastaafu tunaoambulia Sh laki moja kwa mwezi

 

Agosti 3, 2019, mimi mkongwe mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) nilibahatika kutokea kwenye vyombo vya habari bila ya kutarajia hata kidogo. Nadhani wengi waliona kupitia runinga nikiwa Mtaa wa Kilongawima, Jangwani Beach.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alinishangaza aliponiambia umetimiza miaka 89 ya kuzaliwa, Serikali ya Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli inakuzawadia HATI hii ya kiwanja hiki kama zawadi yako ya kuzaliwa – “HAPPY BIRTHDAY.” Nikasema: “Waao!”

Kwanza, sikuyaamini masikio yangu kwa kile nilichokisikia. Watu wanasema matukio ya ghafla yanawafanya watu kushikwa butwaa, bumbuwazi na pengine hata kuchanganyikiwa! Wazungu wanasema “for a moment I got a blackout”.

Baada ya kuzinduka, nikajisikia tu natamka: “Asante sana Mheshimiwa.” Mazungumzo yaliyofuata mmeyasikia na kuyaona kwenye runinga, sina haja ya kuyarejea hapa.

Aidha, nakumbuka tamko la pili la Mheshimiwa Waziri Lukuvi ni lile kuwa: “Wewe Brigedia Jenerali ni maskini na umetaabika kwa muda mrefu ukitumia ka-pensheni kako hako kulipa mwanasheria akutetee haki yako.

“Leo rais amekusikia. Toka leo kiwanja hiki ni chako – Brigedia Jenerali Francis Xavier Mbenna.” Hapo nikakakabidhiwa ile HATIMILIKI yangu.

Basi, nimeona kwa namna serikali hii ya Awamu ya Tano ilivyonikabidhi hati ile hadharani ninawiwa moyoni kutoa shukrani zangu za dhati kwa Rais Dk. John Magufuli kupitia mkono wa Waziri wake wa Ardhi, Nyumba na Makazi, William Lukuvi hadharani pia.

Mtume Paulo aliwaandikia Wathesalonike waraka wake wa 1. Basi katika ile ibara ya 5, alitumia maneno haya: “Angalieni, mtu awaye yote asimlipe mwenziwe mabaya kwa mabaya, bali siku zote lifuateni lililo jema, nyinyi kwa nyinyi na kwa watu wote. Furahini siku zote, ombeni bila kukoma, shukuruni kwa kila jambo, maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu, katika Kristo (1 The. 5:15-18).

Kwa mujibu wa imani yetu Wakristo, mimi pale pale kwenye saiti nilimsamehe Bwana Mongi. Dai langu la usumbufu na gharama zote za ‘makesi’ kuanzia Baraza la Nyumba Kinondoni hadi Mahakama Kuu. Nikamsamehe kabisa na kumwacha huru.

Pili, nilishikwa furaha isiyo kifani maana nimekuwa nikiomba bila kuchoka kwa muda wa miaka 20 sasa. Kwa uamuzi ule wa Waziri Lukuvi, baada ya saa 1 tu ya kusimama pale saiti ndipo nikaamua kutoa SHUKRANI ZANGU HIZI hadharani zimwendee Amiri Jeshi Mkuu wangu, Mheshimiwa John Magufuli na kwa Mheshimiwa William Lukuvi, Waziri mwenye dhamana ya Ardhi, Nyumba na Makazi.

Kwanza kabisa, baada tu ya kukabidhiwa ile hatimiliki yangu pale saiti Kilongawima, nilirudi nyumbani kupumzika. Nikajiona nawajibika kwenda kanisani kwangu Chang’ombe kuongea na Mungu ili nimshukuru kwa hili alilonitendea.

Kwa muda wa miaka karibu mitatu sasa, mimi kutokana na afya yangu kutetereka, huwa ninapelekwa kanisani dominika kwa gari. Lakini amini usiamini, Jumamosi ile ya Agosti 3 nilijikakamua nikatembea kwa miguu kutoka nyumbani kwangu Mtaa wa Litapwasi, Uwanja wa Taifa mpaka kanisani Chang’ombe, kwenda kumtukuza Mungu kwa miujiza (ninavyoita mimi) aliyonitendea kwa kunirudishia kiwanja changu hiki, kitalu namba 388, Jangwani Beach.

Wale walioniona pale kanisani hawakuamini macho yao. Waliniuliza: “Wewe si afande Mbenna mgonjwa tunayekuombea, leo mbona hukuja na gari, kwani imekuwaje? Jibu rahisi: “Ni maajabu ya Mungu niliporwa kiwanja sasa nimerudishiwa na kwa furaha niliyonayo nimeamua nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa msaada na uwezo wake huu, NITEMBEE mpaka hapa kanisani na nitarudi kwa mguu tena mpaka nyumbani.” Na ndivyo nilivyofanya.

Basi, kwake Muumba wangu, mpaji wa yote ninasema tu “DEO GRATIAS.” Pili, katika kumshukuru Mungu asiyeonekana huwa tunashukuru ukarimu wake kupitia viumbe aliotuwekea watuongoze ambao ni binadamu kama sisi. Hapo ndipo ninamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. John Magufuli anayeongoza serikali inayojali na kuwathamini wanyonge. Nasema “WABEJA GETE GETE BABA.”

Aidha, kwa Waziri wa Ardhi, Lukuvi aliyetamka: “…Nakukabidhi hati yako hii ya kiwanja hiki ni chako toka sasa. Ni zawadi ya mwaka wa 89 wa kuzaliwa kwako kutoka kwa Serikali ya Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli.” Ninasema…“NDILUMBA SANA MKURU VANGU, INGURUVI YIKULINDAGE.”

Mwisho, kwa ndugu zangu wote mlionipigia simu za pole na pongezi, mlionitumia SMS na Whatsapp nasema kwenu nyote kwa ujumla wenu: “MSENGWILE SANA MWA WALONGO. ASANTENI SANA.”

Baada ya kushukuru kwa moyo wangu tukio lile la heshima kurejeshewa kiwanja changu No. 388 Jangwani Beach, ningependa pia kuomba kama ilivyo ada ya wakongwe duniani. Kiimani yangu kushukuru kuna maana ya kuomba zaidi.

Namnukuu tena Mtume Paulo waraka wake kwa Wathesalonike kama nilivyonukuu hapo juu – amesema: “OMBENI BILA KUCHOKA” (1 The. 5:17). Hapo ombi langu la wakongwe wastaafu ni moja tu la kurekebishwa MALIPO YA PENSHENI ZAO NDOGO.

Kwanini nchi yetu inatumia sheria mbili tofauti kuwalipa wastaafu mafao ya uzeeni?

Nitalieleza kidogo hili la sheria mbili tofauti kwa wastaafu wa nchi moja, serikali moja, utumishi mmoja. Ni hivi Mheshimiwa Rais:

Kwanza, ninaomba nikunukuu matamko yako mbalimbali.

1. Siku ya Jumanne, tarehe 03 Julai, 2018 kama nakumbuka vema miaka, uliwakaribisha wastaafu wa ngazi za juu (Staff Grade Salaries) pale Ikulu ukaongea nao na kuwashukuru kwa michango yao kwa taifa. Ulisema kwa kifupi “…Mlitumikia taifa kwa uadilifu mkubwa, mlitimiza wajibu wenu na mimi napenda siku moja nikistaafu niwe miongoni mwenu…”

2. Tarehe 18 Julai, 2019, ukiwa Kongwa, Dodoma baada ya ile ziara yako kule Gereza la Butimba mkoani Mwanza, ulisikika kutamka haya “…Mlinichagua kwa ajili ya watu wote, hasa wanyonge wanaopata shida. Siwezi nikatawala nchi ya machozi. Machozi haya yananiumiza. Siwezi kutawala wanaosikitika, wako kwenye unyonge na unyonge wenyewe ni wa kuonewa…Nitaendelea kuwa mtumishi wenu. Naomba Mungu aendelee kunilinda. Kazi hii nisiifanye nikiwa na kiburi, nikawe mtumishi wa kweli bila ya kupendelea mtu na huruma ya kweli ya upendo wa Mungu ikanijae katika moyo wangu…”

3. Wakati unazindua rasmi ‘Terminal III’ katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Agosti mosi, 2019 Dar es Salaam ulitamka mengi mazito yenye kuonyesha moyo wako wa kutoa uamuzi wenye uthubutu wa dhati ya maendeleo kwa nchi yetu. Siku hii tena ulisikika ukisema: “…Serikali imeamua kutekeleza miradi mingi kwa FEDHA ZA NDANI…Ndugu zangu Watanzania, kinachotakiwa ni kujiamini na kuamua kufanya…Nataka kuwaambia, kujiita maskini tukutupe, nchi yetu hii ni tajiri…”

Basi, yapo mengi ambayo mtu angeweza kumnukuu rais wetu, lakini kwa mahitaji ya ombi la wakongwe ninalokusudia kulitoa mimi, hayo niliyonukuu naona yanatosha.

Hali halisi katika nchi yetu iko hivi: Tupo wastaafu wa aina mbili tofauti; na zipo sheria mbili tofauti zinazotumika katika kutulipa mafao ya UZEENI – PENSHENI.

Kundi moja na dogo sana la wastaafu wa zamani kabla ya Juni 30, 1999, wakongwe hawa nadhani hawazidi 3,000 kwa sasa, kwa Kiingereza wanaitwa “THE ELDERLY”. Ni wakongwe wote walioajiriwa kuanzia enzi za ukoloni miaka ile ya 1950 huko mpaka walioajiriwa miaka ya 1963 – 1964. Wakongwe hawa wote sasa wamestaafu mpaka kufikia tarehe hiyo ya Juni 30, 1999.

Basi, wote hawa walitungiwa sheria na mkoloni Mwingereza iliyoitwa “THE MASTER NATIVE ORDINANCE Cap 78” 1924 na ikaja kuboreshwa mwaka 1954 na sasa ikaitwa “THE PENSIONS ORDINANCE of 1954(mwaka nilioajiriwa mimi na wengine wengi).

Kwa mujibu wa sheria hii, wakongwe wanalipwa kidogo sana. Kule Hazina kuna orodha yetu kamili. Wakongwe wote hawa wanarundikwa katika kapu au fungu moja la malipo ya uzeeni na wote wanalipwa Sh 100,000 (laki moja) tu kila mwezi – tunasema “flat rate”, haijalishi ulikuwa na cheo gani, madaraka yapi au mshahara upi – wewe alimradi ulistaafu kabla ya Juni 30, 1999 basi malipo yako Hazina wanakupa hizo Sh 100,000 kila mwezi, zikutoshe zisikutoshe shauri lako.

Aina ya pili au kundi la pili la wastaafu ndio hawa wazee kwa Kiingereza wanalipwa  “The RETIREES”. Kundi hili linawabeba wale wote waliostaafu kuanzia Julai mosi, 1999 mpaka sasa. Hawa wazee wastaafu wa umma kama wale wazee waliostaafu kabla ya Juni 30, 1999 lakini wao wanalipwa kwa mujibu wa sheria mpya inayoitwa The PUBLIC SERVICE RETIREMENT BENEFITS ACT No. 2 of 1999 Cap ile ile 371. Lakini hii ni maboresho ya sheria msingi ya Cap 371 ya 1954.

Sehemu ya sheria hii inasomeka hivi, nanukuu: “The Public Service Retirement Benefit Act No. 2 of 199 REPEALS The Pensions ordinance of 1954.” Pamoja na kusema Repeals the Pensions ordinance of 1954 kimekwa kifungu chenye maneno haya: “….. However, the Act goes further to provide commencement date of the Act; those who were receiving pensions, allowances and other benefits under the provisions of the ordinance similar to those set out under section 20(4) of the Act, will continue to receive the benefits as if the Pensions Ordinance had not been repealed.”

By Jamhuri