Home Makala Tuwe waungwana baada ya kutimiza wajibu

Tuwe waungwana baada ya kutimiza wajibu

by Jamhuri

Binadamu anakula matunda mbalimbali katika mzunguko wa majira ya mwaka, yakiwa ni chakula, kinywaji na tiba katika mwili wake. Baadhi ya matunda hayo ni boga, tikiti na mung’unye.

Watanzania wanakula sana matunda haya kujenga siha ya miili yao. Zaidi ya kuwa ni chakula, kinywaji na tiba, wanatumia asili (maumbile) ya hali ya matunda haya kama vielelezo vya mafunzo ya tabia na mwenendo wa mtu katika jamaa yake au jamii yake anamoishi.

Katika mafunzo hayo, boga, tikiti na mung’unye yanatumika katika methali za Kiswahili kutoa nasaha, mafunzo na maonyo kwa mtu. Inaelezwa kuwa: “Ukipenda boga ulipende na ua lake.” “Tikiti baya li shambani mwako” na “ Umekuwa mung’unye waharibikia ukubwani.”

Methali hizi zinatoa asili ya hali ya matunda haya na kulinganishwa na tabia au mwenendo wa mtu katika shughuli zake za kila siku. Baadhi ya Watanzania wanapatikana katika uga wa methali hizi, iwe kwa kukusudia au kwa kutokusudia.

Wapo watu wanaopenda boga, hawapendi ua lake. Labda kwa sababu ya umbo, rangi au riha yake. Kibaolojia ua huanza kumea na baadaye humea boga. Kutokana na asili hii mtu atatakiwa kulipenda ua ili apate boga alipendalo. Ndipo msemo, “Ukipenda boga ulipende na ua lake.”

Tikiti ni zuri na tamu. Lipo changa na pevu, dogo na kubwa. Linapendeza ulionapo shambani au sokoni. Mkulima anapojaliwa kupata tikiti baya shambani mwake husononeka moyoni na sokoni haliuziki. Bado litabaki shambani mwake. Ndipo msemo, “Tikiti baya li shambani mwako.”

Mung’unye ni tunda mithili ya mboga. Likiwa bichi huliwa kwa kupikwa. Linapokauka gamba lake hutengenezwa kibuyu na nyama yake haifai kuliwa imeharibika. Ndipo msemo, “Umekuwa mung’unye, waharibikia ukubwani.”

Mara kadhaa tumepata kuona au kusikia mkuu fulani mahali fulani akitimiza wajibu wake katika kufanya kazi, na kupewa sifa ni mfanyakazi bora na mwadilifu. Utendaji wake huhesabika umetukuka na anapomaliza muda wake kazini hustaafu na kuzawadiwa zawadi mbalimbali na pongezi nyingi.

Chenye mwanzo kina mwisho wake. Ni methali inayomgusa kila mtu baada ya kutimiza wajibu wake kwa jamii. Hana tena mamlaka wala madaraka katika sehemu hiyo ya kazi. Anapoteza sifa ya kuitwa mfanyakazi na anapewa sifa ya mstaafu, ambayo inampa heshima kubwa sana maishani mwake.

Mstaafu huyu anajikuta katika wajibu mpya wa kutoa ushauri kwa wakuu wapya au wa badala yake walioshika dhamana na mamlaka. Si kutoa kashfa au kusema maneno ya dharau na kebehi. Anapowadharau au kuwaonea wivu walio madarakani, ukweli anajivunjia heshima yake kwa jamii.

Si vema kwa mtumishi wa umma uliyepewa sifa ya kutukuka kutaka kutonesha kidonda. Toa busara kidonda kitiwe dawa kipone haraka, ingawa kitaacha kovu, ni maumbile yake. Narudia kusema, wajibu wa mstaafu ni kufundisha, kuelekeza na kushauri mambo mazuri na yenye tija.

Kutia hofu na kuleta taharuki katika jamii si sifa ya mstaafu yeyote. Na wala haipendezi kuipa nafasi taharuki kububujika mithili ya maji ya chemchemi. Ni vema kudhibitiwa. Aidha, muungwana hasababishi wala haendekezi matendo maovu kutokea katika jamii.

Nawaomba wakuu wa mamlaka mbalimbali na wastaafu wa fani yoyote nchini kuwa makini katika kauli na matendo kabla ya kufanya. Utulivu wa nchi hauoti kama uyoga wala haujengwi na taharuki, unajengwa na usikivu, umoja na mshikamano.

You may also like