Sigara feki zatinga Dar

Biashara ya magendo imechukua sura mpya, baada ya kubainika kuwa sigara zisizolipiwa ushuru tayari zipo katika soko la Dar es Salaam, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

“Kwa sasa zinatumika mbinu mbili. Sigara za Export watu wanatengeneza makasha ya Portsman na SM. Sigara zinafaulishwa usiku kucha. Export zinaonekana ni za hapa nyumbani. Rais [John] Magufuli kazi anayo. Inampasa kudhibiti magendo. Kama ulivyoandika, si sigara tu, wenye pesa wengi wanaingiza karibu kila kitu kwa njia ya panya,” anasema mtoa habari.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa sigara za export zinauzwa maeneo ya Buguruni Sheli na Mbagala Rangi Tatu. “Kuna wasiwasi kuwa hizi sigara zinazouzwa kwenda Msumbiji zinaishia Mbagala au zinafika kule na kurejeshwa. Wengi wanaouza sigara hapa wanapata faida kubwa kwa kutolipa kodi,” anasema mtoa habari mwingine.

Wiki iliyopita, gazeti hili limechapisha taarifa inayoonesha kuwa Serikali inapoteza wastani wa Sh bilioni 100 kutokana na kodi za bidhaa mbalimbali na ushuru kutolipwa katika mpaka wa Tunduma. Sigara peke yake zimebainika kuwa zinalipotezea Taifa wastani wa Sh bilioni 30 kwa mwaka. Wananchi waliozungumza na JAMHURI wameitaka Serikali kufanya msako wa haraka kunusuru hali. 

 

 RC Galawa aeleza mkakati Mkuu wa Mkoa wa Songwe, baada ya kutaja kuwa wanapanga kubomoa nyumba zaidi ya 3,000 zilizoko katika mpaka wa Tunduma, kwa nia ya kuweka ukanda huru wa mpaka (no man’s land), anaongeza:

“Sasa roundabout (mzunguko wa Tunduma) ile inakuja kuingia kwenye nanii, one stop border post (kituo kimoja cha mpakani). Ile ni ya pamoja ni ya Zambia na sisi… barabara ya kwenda Sumbawanga kwa hapa mjini itakuwa ya mwisho, lakini ukienda mbele zaidi kule panaingia. Lakini kwa hapa unakokwenda hapa kutakuwapo Wazambia wanaofanya kazi kwa kule na Watanzania wanaofanya kazi kwa huku, lakini mtu anayetaka kuja hapa, hana shida tena ya kuingia upande wa pili, akishughulikiwa anamaliza kila kitu sehemu moja.

“Shida ya mpaka… mpaka ni shida. Mimi nimeanza kata nyingine ipo kule, kwenye Halmashauri ya Momba, ya Kapele, na yenyewe nimekuta hivyo hivyo. Kilomita kama 150 mpaka uko hivyo. Watanzania wamejenga shule, na hii unakuta imeingia Zambia. Kanisa liko huko, yaani… Wazambia wako mbali, wanasema kwa nini mnaingia kwetu? Kwa hiyo yaani, nimeanza na hii kata, lakini kikubwa tumeanza kupima.

“Tuwe na mpango wa matumizi ya ardhi lakini tunataka pia viwekwe vipimo vyetu vya mita 50, haya makubwa (mawe ya mpaka wa nchi) yanakuwaga kilomita 3 mpaka ufikie lingine, kwa hiyo it is too far (ni mbali). Ndiyo maana watu wanashindwa kujua, na siyo kwamba wengine wameingia kwa sababu wanataka, wanaona wenyewe ni eneo lilelile.

“[kwamba Nyerere na Kaunda waliwaachia mpaka huu] haiwezekani hiyo, kwa sababu sasa hivi mtu anafanya uhalifu huku anakimbilia kule. Hata kama wapo ndugu zako kule, wanafanya hivyo, ndiyo maana sisi mauaji, actually sisi mauaji ni order of the day (ni kawaida) ikipita siku hajauawa mtu tunashangaa. Kwa hiyo, hivyo hivyo wanafanya wanaua… wanaiba bodaboda na wanaua. Haiwezekani unaiba bodaboda halafu usiue. They kill, this is bad (wanaua, hili ni jambo baya).

“Kwa hiyo, tuna mipango mizuri tu ya kufanya, lakini kama nilivyokwambia it has taken so long (imechukua muda mrefu) ni kama kansa, sasa huwezi kwenda ukasema nakwenda kuiondoa mara moja. Imekaa muda mrefu,” anasema Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa.

Alipoulizwa katika muda mfupi ujao nini wataanza nalo kurekebisha hii hali ya mpaka wa Tunduma inayozaa magendo ya hali ya juu, akasema: “Kwanza tumeanza na hii master plan. Na sasa tumeishawatangazia watu kuwa msijenge bila kibali cha ujenzi. Kuna tatizo kubwa sana la maji, watu wanajichimbia visima. Na Waziri wa Maji nimemwalika tarehe 23 na 24 anakuja tuone tunamaliza vipi tatizo la maji.

“Lakini ukiacha kuja kwa waziri, hawa wenzangu nimewaomba wanisaidie kumalizia kupiga picha, maana it is very expensive (ni ghali sana), lakini nimewaomba wanipigie tu. Tukiishakamilisha nitatoa Ilani. Nitaomba wanipige X, na kuwataka watu kwamba jamani ehee, huko kwenye ‘no man’s land’, huku halmashauri nayo tunaisukuma kwa ajili ya kupata mkopo kujenga soko la kisasa,” amesema.

Alipohojiwa juu ya fidia kwa watu ambao wamezaliwa mpakani na mipaka ya wakoloni ilikuta vizazi vya baba na babu zao hivyo wastahili fidia, akasema: “Hakuna cha kuzaliwa hapa, umezaliwa hapa vipi. Hata ukizaliwa hapa, huu ni uamuzi halali wa kumaliza tatizo lililodumu kitambo. Hakuna cha fidia, wote wataondoka tu,” amesema.

 

Maduka, baa Zambia

 Wiki iliyopita baada ya kuchapisha habari ya magendo katika mpaka wa Tunduma, nimepata pongezi nyingi. Nimepewa pia ushauri wa kisheria kuwa kwa baa na maduka yaliyoko Zambia, kwa nia ya kuimarisha uhusiano wa kimataifa baina ya Tanzania na Zambia si vyema mno kutaja maduka na baa zao kana kwamba zinafanya uhalifu wakati kwao zinafanya biashara halali.

“Kimsingi umefanya kazi nzuri. Lakini kama unavyoona Serikali wenyewe wanasema Mtanzania akivuka mpaka akaenda Zambia hawana cha kumfanya, kisheria si vyema sana kuanza kuanika majina ya baa na maduka yanayofanya kihalali biashara huko Zambia.

“Kwamba maduka haya yanauza bidhaa nusu ya bei ya Tanzania hilo si kosa lao. Hii inatokana na mfumo wa kodi tulionao. Tanzania inatoza kodi nyingi kwenye vinywaji na sigara na kufanya bidhaa hizo kuwa bei ghali kwa kuwa ndiyo chanzo pekee cha mapato kwa Taifa hili. Hatuna kiwanda cha kuzalisha hata majembe au baiskeli kinachoweza kuingiza kodi tukaachana na vinywaji na sigara.

“Angalia kila mwaka kodi zimekuwa zikipandishwa kwa sigara na vinywaji. Ndiyo maana unakuta mwaka huu tunasema afadhali. Tumempaka Rais Magufuli anayesimamia dhana na sera ya ujenzi wa viwanda. Huo ndiyo mwelekeo sahihi. Bila kuwa na viwanda vyetu tukashindana kuuza bidhaa zetu nje ya nchi kwa kuwa na wingi wa bidhaa ndani kwetu, lazima magendo yashamiri.

“Viwanda vya bia kama Heineken ulizozitaja au vinywaji vya kuongeza nguvu kama Redbull ulivyovitaja pia, tulipaswa kuwa na kiwanda kinachofanya kazi under licence hapa nchini. Soko lipo. Kusafirisha vinywaji hivyo kutoka nchi zao kuja hapa, tunapoteza ajira, tunaongeza gharama za usafirishaji, ilibidi tuwe navyo hapa nchini,” anasema mmoja wa wataalamu wa sheria za kimataifa aliyeomba jina lake lisitajwe gazetini.

Mwanasheria mwingine, ameiambia JAMHURI kuwa kama ni wajibu gazeti hili tayari limeutimiza vyema. “Huna sababu ya kujenga uhasama na wenye maduka huko Zambia. Hawa watu ukiona polisi wa Zambia hawawakamati, ina maana wana leseni na wanafanya biashara kwa njia halali. Kwamba bei za bidhaa zao ziko chini na ni kishawishi kwa Watanzania kwenda kununua bidhaa hizo na kuzivusha kwa njia hizo za panya 320 ulizozitaja, hali iko wazi. Ni kazi ya Serikali sasa kuhakikisha inadhibiti magendo hayo,” anasema mtaalamu mwingine.

Baada ya kushauriana ndani ya chumba cha habari hapa, imeonekana ni vyema kutoorodhesha maduka ya upande wa Zambia yanayouza bidhaa zinazovushwa kuja Tanzania na kwa sababu za kisheria, hata baa zilizoko upande wa Tanzania zinazouza bidhaa hizo inaweka ugumu kutaja majina yake kwani bidhaa hizi zinahamishika, ila sasa liwe jukumu la polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kusaka wafanya magendo.

 

Nilivyoingia Zambia siku ya pili

Wiki iliyopita niligusia mbinu nilizozitumia kuingia Zambia na nikaahidi kueleza zaidi wiki hii. Hili nalo washauri wa masuala ya kihabari wameniambia halina afya kwa upatikanaji wa habari za uchunguzi. Kwa kufanya hivyo au, kuzitaja mbinu nilizotumia itawapa shida wanahabari wengine kuzitumia siku za usoni kwani zitabainika kwa urahisi.

Hata hivyo, itoshe kusema tu kuwa bidhaa za magendo zinazovuka kutoka Zambia kuja Tanzania ni nyingi. Vinywaji kama Redbull, kopo moja linauzwa Sh 1,900 upande wa Zambia, huku likiuzwa Sh 3,000 upande wa Tanzania. Bia kama Heineken inauzwa Sh 1,900  Zambia, Tanzania inauzwa Sh 3,000. Chupa ya kinywaji kikali kama Gordons ya mililita 750  inauzwa Sh 13,000 Zambia na Tanzania inauzwa Sh 36,000.

Bidhaa hizo pamoja na vipodozi, inakisiwa kuwa kwa ujumla wake vinaipotezea Serikali zaidi ya Sh bilioni 100 kwa mwaka, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

1796 Total Views 3 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons