Wakati idadi ya wananchi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inasadikiwa kufikia watu milioni 160, baadhi ya mikoa iliyounganishwa katika miundombinu ya barabara inashindwa kulifikia soko hilo.
Baadhi ya mikoa hiyo ni pamoja na Singida, mkoa unaozalisha alizeti pamoja na vitunguu kwa wingi hapa nchini. Ikumbukwe kwamba soko kubwa la vitunguu la Jumuiya ya Afrika Mashariki liko mkoani Singida.
Jiografia ya Mkoa wa Singida inatoa fursa kwa mkoa huo kufanya biashara na nchi jirani kama Rwanda, Burundi, Uganda, Kenya pamoja na Sudani ya Kusini, nchi ambayo imejiunga hivi karibuni katika jumuiya hiyo.
Mkoa huo umeunganishwa kwa barabara za lami na maeneo ya mipaka ya zilizotajwa, mfano mfanyabiashara anaweza kuamua kwenda kuuza vitunguu vyake Kenya, kwa kupitia Babati mpaka Namanga, hivyo kulifikia soko kwa haraka zaidi.
Hali haiko hivyo, wakulima wanaendelea kulima kwa bidii na kuleta mazao kama vitunguu kwenye soko hilo la kimataifa lakini hawapati wateja. Kikubwa ni kwamba wananchi pamoja na wafanyabiashara hawajaweza kuchangamkia fursa hizo.
Akizungumza na JAMHURI, Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), Culvert Nkurlu, amesema hakuna jambo ambalo limekuwa linafanyika katika mkoa wa Singida linalowaunganisha wananchi na fursa za kiuchumi zilizopo katika Jumuiya.
Amesema Mkoa wa Singida ni maarufu kwa kilimo cha alizeti pamoja na vitunguu, lakini ukiondoa mafuta ambayo kuna wawekezaji wenye viwanda vya kati, ambao wamekuwa wakikamua mafuta, wakulima wa vitunguu wanaendelea kusota.
Nkurlu amerusha lawama zake kwa baadhi ya viongozi wa Serikali pamoja na sekta binafsi, kwa kushindwa kuonesha na kuzitumia fursa zilizopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ameliambia JAMHURI, kwa kipindi kirefu Mkoa wa Singida umekuwa ni soko la vitunguu, ambavyo wakulima wake hawana uhakika wa soko.
Hivi karibuni wadau wa Soko la Pamoja la Afrika Mashariki, wamefanya mkutano Jijini Dar es Salaam wakishirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF) ili kujadili utekelezaji wa Soko hilo.
Akizungumza katika Mkutano huo, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wanachama wa TPSF, Louis Accaro, amesema Afrika Mashariki ina nchi sita zilizokubaliana kuwapo na soko la pamoja, lengo likiwa ni kuondoa vikwazo vya kibiashara.
“Katika utekelezaji wa soko hili, hasa kuangalia vikwazo ambavyo vinazuia biashara isifanyike mfano kutoa mzigo kutoka nchi moja hadi nyingine na vikwazo vingine vya kibiashara,” amesema Accaro.
Mtaalamu wa huduma za biashara wa soko la pamoja, Octavian Kinyiro, amesema kuwa tukiondoa vikwazo mbalimbali vya kibiashara kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, watu wengi watakuja kufanya biashara katika soko hilo.
“Zamani Watanzania walikuwa hawaruhusiwi kuwekeza nchi nyingine, sheria zetu zilikuwa haziruhusu lakini kwa sasa zimeondolewa ili wapate fursa za kuwekeza nje ya nchi,” amesema Kinyiro.
Mwaka 2014, Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliandaa mkakati wa utekelezaji itifaki ya soko la pamoja, ili kurahisisha na kuondoa changamoto zinazolikabili soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mkakati huo unatoa mwelekeo wa utekelezaji wa soko la pamoja katika ngazi ya kitaifa kwa kuendeleza muundo, mipango ya kisekta na programu zitakazosaidia ukuaji wa uchumi.
“Hapa wasipokuja Wakenya na Waganda, soko la vitunguu linakuwa kwenye mtihani mkubwa, lakini huwezi kuona wakulima wetu hapa wakijipanga kwenda nchi wanachama kuuza bidhaa hiyo ya kitunguu ambayo inapendwa sana,” amesema Nkurlu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa soko la kimataifa la vitunguu, mkoani Singida, Saidi Hamoud, Januari mwaka huu soko lake lilikuwa na mafuriko ya vitunguu huku wakiwa hawana wateja wa uhakika.
“Tulikuwa na tani zaidi ya 1,500, za vitunguu hapa, kiwango hicho ni kikubwa sana kwa matumizi ya soko la hapa kwetu, hatukupata wateja kutoka nje ya nchi, hivyo hata bei yenyewe ikashuka sana,” amesema Hamoud.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, wanunuzi wa vitunguu walikuwa ni wafanyabiashara kutoka Kenya na Uganda, lakini kwa sasa inaonekana nao wameanzisha kilimo cha vitunguu huko nchini kwao, na sasa wanaonekana kutokuwa na sababu ya kuhitaji vitunguu kutoka Singida.
Mbali na baadhi ya mikoa na nchi jirani ikiwamo Uganda na Kenya kulima zao hilo kwa sasa, wanunuzi waliokuwa wakifika katika soko la Misuna wameanza kuishia kwenye mikoa jirani inayozalisha vitunguu kwa sasa.
Mkoa wa Singida umekuwa ukizalisha vitunguu wakati wa msimu wa mvua na pale mvua zinapokata hulima kwa njia ya kilimo cha umwagiliaji, ili kuhakikisha zao hilo linakuwa endelevu katika kipindi cha mwaka mzima.
Kwa mujibu mwenyekiti huyo, kwa siku soko hilo limekuwa likipokea tani zaidi ya sita za vitunguu na kuuza tani nne ambazo husafirishwa kwenda nchi za Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan, Oman na Kisiwa vya Madagascar.
Vitunguu vinavyosafirishwa nje ya nchi ni vile vya viwango vya daraja A, wakati vya daraja B na C huuzwa katika mikoa mingine na D na E hupelekwa kwenye minada na magulio.
Pamoja na mikoa jirani kuzalishaji vitunguu, kuondolewa kwa ujazo wa lumbesa pia kumechangia kupunguza bei ya vitunguu na kusababisha baadhi ya wateja kuhama kwa kutoridhishwa na upimaji kwa kutumia mizani.
“Wateja wetu walizoea mshono wa lumbesa ambao ulizuiwa na mkuu wa mkoa na kuwataka wauze kwa mizani. Kwa sasa wateja wanalalamika kwamba hali hiyo inawatia hasara kwa kukata mitaji yao,” amesema.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, bei ya vitunguu ilianza kushuka kuanzia Julai mwaka 2016, baada ya mikoa mingine ikiwamo Dodoma, Manyara na mikoa ya kusini kuzalisha zao hilo na kusababisha wanunuzi kununua vitunguu kwenye maeneo ya karibu badala ya kufika Singida kama ilivyokuwa awali.
Wakulima wa vitunguu mkoani Singida msimu uliopita walizalisha tani 17,334 za vitunguu zenye thamani ya sh. bilioni 3.5 katika maeneo yanayolima zao hilo kwa wingi na kuuzwa kwa wafanyabiashara kutoka nje ya nchi na ndani ya nchi.
Taarifa zilizotolewa kwa vyombo vya habari na Ofisa Kilimo Mkoa wa Singida, Deusdedit Rugangila, zinaeleza kuwa wafanyabiashara kutoka Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, India na Comoro na wengine kutoka mikoa ya Manyara, Arusha, Morogoro, Dar es Salaam, Mbeya na Mwanza ndiyo wanaoongoza kununua vitunguu vya Singida kwa wingi katika soko lililotengwa.
Wakulima wa vitunguu huanza kutayarisha mashamba yao mwezi Novemba hadi mwezi Aprili, tayari vitunguu huanza kuvunwa na kuuzwa.
Rugangila amewahimiza wakulima kutumia mbegu bora ili waweze kupata mazao mengi na bei nzuri ili kukidhi mahitaji ya soko.
Hata hivyo, amewahimiza wakulima kutumia elimu ya kilimo iliyopo kwenye maeneo yao ili waweze kufikia malengo yanayotakiwa.
Mkoa wa Singida katika miaka ya nyuma ulikuwa maarufu sana kwa uzalishaji wa vitunguu, lakini sasa uzalishaji wake umeanza kupungua kutokana na upungufu wa mvua, kukosa dawa za kuua wadudu, na utaalamu mdogo juu ya upandaji, uvunaji na utunzaji wake.

1403 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!