Utapeli wa ardhi Dodoma

Mjane miaka 84 alizwa, mabaraza ya ardhi yakithiri rushwa

Lukuvi aombwa kutatua mgogoro

William Lukuvi

Mkazi wa Kijiji cha Handali, Wilaya ya Dodoma Vijijini, Hilda Mzunde (84), amemwomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kuupatia ufumbuzi mgogoro wa ardhi kati yake na kijana Charles Kwanga anayefanya mikakati ya kumdhulumu kiwanja chake.
Akiongea na JAMHURI, Mzunde ambaye ni mjane, amesema ameishi katika eneo hilo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari nne tangu mwaka 1960 na mumewe Anthony Mzunde ambaye alifariki dunia mwaka 1985.
Mzunde amesema katika eneo hilo ndipo penye makazi yao ambayo ni nyumba mbili na sehemu nyingine ni shamba analolima mazao mbalimbali ikiwamo mizabibu na mahindi.
Amesema nyumba yake ya pili iliyopo ndani ya eneo hilo ambayo ilikuwa haina mtu anayeishi, ndipo alipoomba hifadhi kwa muda kijana huyo (Kwanga) na kwamba akikamilisha ujenzi katika kiwanja chake ataondoka.
“Kwa huruma tu nilimkaribisha aishi katika nyumba hiyo, na yeye siyo wa kwanza, wako watu wengine wawili walioomba hifadhi katika nyumba hiyo kwa nyakati tofauti na waliondoka kwa amani baada ya kupata maeneo yao.
Kijana huyo ameishi katika eneo hilo kwa miaka 15, na kila alipokuwa akiulizwa ni lini ataondoka amekuwa akitoa majibu kuwa avumiliwe kidogo na wakati mwingine anasema hawezi kuondoka katika eneo hilo,” amesema.
Hata hivyo, kutokana na kauli hizo, mjane huyo anasema watoto wake walipofika kijijini hapo na kuhoji kijana huyo anaishi katika nyumba yao kwa utaratibu gani na lini ataondoka! Hawakuridhika na majibu ya mdomo na ndipo walipokwenda pamoja naye kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Handali kwa ajili ya kuandikishana maelezo.
Katika makubaliano hayo kwa njia ya maandishi yakiwahusisha mashahidi wa pande zote yaliyosainiwa na Afisa Mtendaji huyo Februari 12, 2015, Charles Kwanga alikubali kukabidhi eneo la Hilda Mzunde Oktoba 2015.
“Mimi Charles Kwanga kwa kinywa changu nakiri kukabidhi kwa muda uliopangwa,” inaeleza sehemu ya nakala hiyo ambayo JAMHURI linayo, iliyosaniwa Maholi Julius.
Pamoja na kukiri kwa maandishi kwamba ataondoka katika eneo hilo kwa kipindi hicho, hajatekeleza hilo na badala yake ameendelea kumsumbua mjane huyo akidai kwamba yeye ndiye mmiliki wa eneo hilo.
Mzunde amesema tangu mwaka 2015 hadi mwaka huu, ameshindwa kurudisha eneo hilo na katika usuluhishi wa mgogoro huo katika Baraza la Ardhi la Kata ya Handali, mlalamikiwa ametakiwa kutekeleza ahadi yake ya kukabidhi eneo kwa mmiliki wake lakini amekaidi.
JAMHURI limefanya jitihada za kumtafuta Kwanga, kuelezea suala hilo bila mafanikio, kwani hata simu ya kiganjani aliyokuwa akiitumia ilikuwa inapokewa na mkewe ambaye alikiri kumfahamu huku akishindwa kuelezea chochote na baadaye kuizima.
Salome Mzunde (52), mkazi wa Kigamboni, Jijini Dar es Salaam, ambaye ni miongoni mwa watoto wa Hilda, anasema walipokuwa wanafika hapo nyumbani kwao Handali, walimkuta kijana huyo akiwa anaishi kwenye nyumba yao na walipomhoji mama yao aliwajibu kuwa ameomba kujihifadhi kwa muda mfupi na baadaye ataondoka.
Salome amesema kutokana pia walimhoji kijana huyo kuwa ni lini ataondoka katika nyumba yao, lakini alikuwa anaahidi ataondoka wakati wowote bila kutekeleza hilo.
“Pamoja na kuahidi kuondoka katika eneo hilo ambalo wazazi wetu wamekuwa wakilimiki tangu mwaka 1960, ameendelea kung’ang’ania kwa madai kwamba yeye ndiye mmiliki na wasifikirie ataondoka,” amesema Salome.
Kutokana na kitendo cha kugoma kuondoka katika eneo lao, waliamua kwenda kuomba msaaada serikalini kwa Afisa Mtendaji na kuandikishana kwa maandishi ambako aliahidi kuondoka ifikapo Oktoba 2015, lakini hadi sasa amegoma na kufanya jitihada za kupora eneo hilo.
Amesema wamefuatilia suala hilo katika Serikali ya Kijiji na Mabaraza ya Ardhi ya Kata na Wilaya wanaelezwa kwamba wasimsaidie mama yao kudai haki yake, hivyo wasubiri atapofariki mama yao ndipo wafungue kesi ya kudai mirathi.
“Sasa anaharibu hata mazao yanayolimwa na mama yetu kwa kufyeka mahindi na mizabibu akidai eneo hilo ni mali yake na hiyo imetokana na vitendo vya rushwa vya baadhi ya viongozi wa kijiji cha Handali, kwani wako watu wawili ambao ni mashahidi walioomba hifadhi katika nyumba yetu kwa nyakati tofauti na wameondoka kwa amani baada ya kupata makazi yao.
Tangu aombe hifadhi katika nyumba hiyo hadi sasa, ni muda wa miaka 15, na amekuwa akiuza mashamba aliyogawiwa na mzee wake na kuzitumia fedha hizo kutoa rushwa kwa baadhi ya viongozi wa kijiji hicho kwa lengo la kumdhulumu mama yao eneo lake,” amesema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Handali, Samwel Mogosho, amesema yeye si mtaalamu wa sheria, lakini Baraza la Ardhi la Wilaya lilimpa ushindi Charles na haelewi kwa nini.
Aliyekuwa Mtendaji wa Kata ya Handali, Maholi Julius, amesema yeye ndiye aliyeandikisha hati ya makubaliano kwa pande zote mbili wakiwamo mlalamikaji na mlalamikiwa na mashahidi wa pande zote, amesema kijana huyo alikubali kwamba angeondoka katika eneo hilo Oktoba 2015 lakini haelewi ni kwa nini hakutekeleza makubaliano hayo.
“Kabla kuhama nilikuwa nalielewa suala hilo linavyoendelea na kumshauri huyo mama aende katika Baraza la Ardhi la Kata na ninachofikiri kwamba walitoa uamuzi na sisi hatuingilii masuala hayo kisheria, lakini ninachoelewa ni makubaliano niliyowaandikisha mbele ya mashahidi,” amesema.
Naye Afisa Mtendaji Mpya wa Kata hiyo, Paul Mzuri, amelieleza JAMHURI kuwa hafahamu kama kulikuwa na mkataba waliokubaliana awali mbele ya mtangulizi wake, lakini suala hilo analielewa na hivyo amekuwa akimwelekeza mama huyo aende katika Mabaraza ya Ardhi ya Kata na Wilaya.
Amesema matatizo makubwa kwa vijiji sasa ni migogoro ya ardhi inayoibuka mara kwa mara kutokana na wananchi wengi kupata uelewa kuwa ardhi ni mali.
Agnes Petro, mkazi wa Dodoma Mjini, amesema kwa sasa imeibuka migogoro mingi ya ardhi kutokana na matapeli wengi wa ardhi kuvamia Dodoma baada ya Serikali kuanza kuhamia mkoani humo.
“Hii migogoro ya ardhi imekuwa kero kila mahali, wananchi tunadhulumiwa ardhi na wajanja wachache ambao kazi yao ni kutoa rushwa kwa viongozi wa vijiji, ili wasaidiwe kupora maeneo yetu kwa kutumia hata Mabaraza ya Ardhi ambayo hayaaminiki sasa.
Tunamwomba Waziri Lukuvi atusaidie kwani tunaonewa mno hasa wanawake ambao tunanyanyaswa hata na vyombo vya Serikali ambavyo vimekuwa havitendi haki kwetu,” amesema Petro.

941 Total Views 1 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons