Baada ya ajali ya hivi karibuni mkoani Tabora iliyohusisha gari la mizigo na basi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, ametoa agizo kwa Jeshi la Polisi ambalo litawaumiza waendesha magari wengi.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari juu ya tamko lake, ametaka Jeshi la Polisi kuwapeleka mahakamani mara moja wanaoshikwa kwa kosa la kuendesha gari kwa mwendo kasi.

Kwa maoni yangu ameongeza nyundo kwa Jeshi la Polisi ambalo siamini linahitaji kuongezewa silaha ya ziada kukabiliana na tatizo la mwendo kasi.

Sasa hivi ipo tofauti kubwa sana ya utii wa Sheria ya Usalama Barabarani kwenye awamu hii ya tano ya Serikali. Madereva wengi ambao hawakuzingatia sheria sasa wamebadilika.

Wale wachache ambao bado wanaona kuwa ni muhimu kukiuka sheria, hasa ya kutozingatia mwendo wa uendeshaji unaoruhusiwa, wamehamishia uendeshaji wao usiku ambako maafisa wa polisi waliopo barabarani wanatafuta wahalifu wa aina nyingine, siyo wa mwendo kasi.

Madereva wa mchana wanakumbana na matatizo kadhaa ambayo yameendelea kuwaandama hata kabla ya tamko la waziri. Tamko la waziri ni sawa na kumwongezea Lionel Messi upana wa goli, kutoka kibendera kimoja hadi kingine. Itakuwa ni kuwapa polisi msaada ambao hawahitaji hata kidogo.

Ni mara chache sana tunasikia polisi wamezidiwa nguvu na mtuhumiwa au mhalifu. Na katika mara chache inapojitokeza hali hiyo ya kuzidiwa nguvu, majibu ya polisi huwa yanazima mfurukuto wowote wa ubishi. Kwa kawaida mtu yeyote mwenye kujitakia mema habishani sana na mtu anayeshika silaha.

Kwa bahati mbaya Sheria ya Usalama Barabarani inatoa fursa pana kwa watuhumiwa na polisi kubishana mara kwa mara. Tatizo kubwa linazuka kwenye tafsiri ya sheria yenyewe, pamoja na utekelezaji wake. Sheria hiyo hiyo inabeba tafsiri tofauti kutegemea na mtuhumiwa amesimamishwa wapi na polisi.

Lakini lipo pia tatizo la uhakika kama kweli mtuhumiwa amefanya kosa. Yapo maeneo ya barabara ambako vibao vya alama za mwendo unaoruhisiwa havipo. Pengine vilikuwepo na mjasiriamali mmoja akaamua kuvihamisha na kumuuzia mmiliki wa kiwanda cha kutengeneza nondo.

Dereva anaweza kupita eneo kwa mwendo ambao hauruhusiwi, eneo ambalo awali lilikuwa na vibao hivyo na akasimamishwa na polisi kwa kuendesha kwa mwendo kasi. Polisi ambaye Inawezekana kaamkia kwenye nyumba iliyojengwa kwa nondo inayotokana na kibao cha mwendo kasi ambacho kimeibwa barabarani ni huyo huyo ambaye atachachamaa kituoni kutekeleza sheria.

Polisi anakukamata kwa kumbukumbu yake ya kibao ambacho hakipo, na hataki kusikia maelezo yoyote ya mtuhumiwa kuwa hicho kibao hakipo. Kama nilivyobainisha, polisi hataki mbishi. Kubali uendelee na safari. Kataa ujiongezee changamoto za maisha.

Suala la tafsiri na utekelezaji wa sheria linazua mambo kadhaa. Mfano, si kila mmoja ana uwezo wa kulipa faini ya mwendo kasi hapo hapo, na sheria inaruhusu aliyetenda kosa kulipa ndani ya siku saba. Lakini kama vile changamoto za kawaida tu za maisha hazitoshi, polisi wa maeneo mengi hukataa kipengele hiki cha sheria.

Ukihurumiwa sana utaambiwa uache gari kituoni na ukishalipa ndiyo gari litaachiwa. Ukiwa mwenye safari ya masafa marefu, hiyo inakuwa adhabu ambayo inaongezea tu matatizo ambayo madereva wengi wanakumbana nayo.

Katika kuipa nguvu hoja yao, polisi wanasema kuwa kwa maeneo ambayo faini zimeanza kutolewa kwa mashine inawezekana kumpa dereva muda huo unaoelekezwa ndani ya sheria, lakini katika maeneo mengine hawatoi muda huo. Siyo kweli kwamba ipo sheria ya Dar es Salaam na sheria ya Singida, lakini hali halisi ndiyo hiyo; yapo maeneo ambako polisi wanaongeza vionjo vyao kwenye Sheria ya Usalama Barabarani.

Mara ya mwisho kukabiliana na faini ya mwendo kasi (kilomita 57 kwa saa kwenye eneo ambalo halina kibao) afisa mwandamizi aliniahidi kunipigia simu kunitajia hicho kipengele kinachoelekeza kuacha gari kituoni, lakini mpaka leo sijamsikia.

Haya ndiyo baadhi ya matatizo ambayo yapo. Tamko la waziri linatoa nafasi kuongezeka mengine. Kwanza, polisi wengi wataharakisha kutekeleza agizo la waziri la kuwaweka kapu moja yule aliyeendesha gari kwa kilomita 57 kwa saa na yule aliyeendesha kwa kilomita 150 kwa saa. Polisi wamekabidhiwa kokoro la kusomba papa na dagaa.

Waendesha kasi wengi hukubali kosa, lakini sasa kutokana na tafsiri yangu ya tamko la waziri, wote – waliokubali na waliokataa – watapelekwa mahakamani.

Na wale tunaohoji iwapo sheria inatekelezwa vyema juu ya muda wa kulipa faini, na ulazima au la wa kuacha gari kituoni sidhani kama tumeachwa na nafasi yoyote ya kujenga hoja. Tutaambiwa tukabishane na hakimu.

Hoja moja niliyoisikia kutoka afisa wa polisi ya kutotoa nafasi ya wiki moja kulipa faini ni kuwa baadhi ya watuhumiwa hukimbia, na afisa akalazimishwa kulipa faini na wakuu wake. Hoja hii sijaelewa mantiki yake kwa sababu hata yule aliyepewa muda wa wiki moja kulipa kwenye eneo ambalo linatumia faini za mashine naye anaweza kukimbia.

Mfumo wa vitambulisho vya taifa ukitumika vyema unaweza kufanikisha kumpata mtuhumiwa au mhalifu anayesakwa na polisi. Ukitumika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usalama Barabarani utatoa ahueni kwa madereva wanaokutwa na makosa madogo ya matumizi ya barabara.

Lipo suala lingine linachangia malalamiko juu ya utekelezaji wa sheria, na kuchangia ajali. Wapo madereva wengi wa serikali, viongozi, taasisi za serikali, na mashirika ya umma ambao wanaamini kuwa kipengele cha sheria kinachozuia mwendo kasi hakiwahusu wao. Na wapo polisi ambao wanaamini hivyo.

Mwendo kasi wa kilomita 150 kwa saa hauwezi kuwa salama kwa sababu anayeendesha ni dereva wa waziri. Kama anapita kwa kasi hiyo eneo la makazi atahatarisha usalama wake, wa waziri, na wakazi wa eneo lile kama ambavyo atakavyohatarisha dereva mwingine. Sheria, hata yenye hitilafu, inakubalika zaidi iwapo inawagusa wote, pamoja na dereva wa waziri anayeendesha mwendo kasi.

By Jamhuri