Naandika waraka huu nikiwa najua fika kwamba kuna majonzi juu ya majonzi kwa watu wengi, hasa tasnia ya habari hapa nchi. Wengi wamesikia misiba na ambao hawajasikia ni vema wakajua sasa hata kwa kuuliza.

Naandika waraka huu nikiwa na maswali mengi sana kichwani mwangu, najiuliza nimuulize nani lakini simuoni, nafikiri ni vema nikajiuliza mimi mwenyewe, Ruge ni nani? Nani alikuwa anamjua nje ya tasnia? Na kwanini taifa lilimlilia? Ni maswali ambayo kwa kadiri ya uelewa wangu naweza kuyajibu bila hofu yoyote kutokana na jinsi nilivyomfahamu huyu bwana mdogo, Ruge Mutahaba.

Siwezi kuelezea yale mambo makubwa ya ndani ya familia lakini ninachoweza kumuelezea ni mambo ya utumishi katika jamii na watu aliowaongoza. Ruge alikuwa kiongozi aliyejua maana ya kuongoza watu wa rika, elimu na tabia mbalimbali, wapo ambao watajiuliza, kwanini kawaliza wafanyakazi wenzake wengi? Nadhani wamelia, kwa sababu walijua ameondoka huku wakiwa wanadaiwa naye mema mengi aliyowatendea.

Kwenye msiba hakuna kasoro za hapa na pale, pia marehemu hakuwa malaika alikuwa ni binadamu mwenye moyo wa nyama lakini ni binadamu mwenye roho ya utu, nimesikia wanaomlaumu lakini wengi wao ni wale akili nusu, duniani wanatafutwa na ahera hawajafika, mapepe.

Nimeamua kuandika waraka huu kwa kuwa najua Ruge kafungua ukurasa mpya sasa wa fursa kwa wakubwa,  kwa maana ya viongozi wengine kujifunza kwanini kiongozi mwenzao anaweza kuliliwa kiasi hicho na wao wakiwa wanaishi na watumishi kama Ruge lakini kila siku ni kama anaombewa ama afukuzwe kazi au atangulie mbele ya haki.

Kifo cha Ruge kimeonewa gere sana na viongozi mbalimbali, si wafanyakazi, viongozi wengine wameona wivu kuhusu kifo kile kiasi cha kujiuliza, hivi na wao wakitwaliwa kama mwenzao huku nyuma watu watalia kama walivyolia kwa mwenzao? Baadhi yao wanaona makandokando mengi yakiwahukumu pasi na ukweli wa tabia zao.

Wapo wanaoona jinsi ambavyo wamewafukuza kazi watumishi wasio na hatia na jinsi ambavyo wanateseka na familia zao, wapo ambao wanaona damu ya rushwa inavyobubujika katika viganja vyao huku wakipoteza haki na kuuza haki za watu wanyonge waliopaswa kuwasaidia.

Wapo ambao wanaona jinsi ambavyo wamejitenga na kundi wanaloliongoza huku wakiamini wanaowaongoza ni wanyama, si binadamu kama wao, fursa ya kuwa kiongozi inaweza kumtokea mtu yeyote yule, hivyo ni bora kuyatumia madaraka huku ukihesabu mema yako baada ya maisha, baada ya kazi. Ruge angeliweza kuwa kiongozi hata baada ya maisha ya uongozi, aliyaangalia maisha baada ya uongozi.

Naandika waraka huu nikiwa naamini kabisa kwamba kazi kubwa aliyoifanya Ruge kuwaelimisha watu wenye madaraka na vipato imetimia, hakuwa mtu wa kukwaza wengine, hakuwa mtu wa kutafuta umaarufu au kutaka kujulikana kwa madaraka aliyokuwa nayo.

Ruge alitumia alichokuwa nacho kwa faida ya wengine, alikataa maisha ya kuiga na alikuwa yeye mpaka pale alipotwaliwa, kama mema yanafuta maovu, naamini mema alikuwa nayo mengi kuliko maovu.

Lengo la waraka wangu si kumsemea Ruge, la hasha! Ni kuwasemea viongozi wengine mliobaki na kujisahau, viongozi ambao mnajenga chuki kwa walio chini yenu, viongozi mnaoamini katika ubinafsi na si haki, viongozi mnaodhani mna haki kuliko wengine, viongozi ambao mnadhani ni bora kujilimbikizia mali badala ya kuitumia na wasio na uwezo, viongozi mliojaliwa dharau kwa walio chini yenu.

Kama kuna kitu mnapaswa kujifunza kutoka kwa Ruge ni kwamba uongozi bora si kutisha, ni kuwa mshauri mwema kwa unaowaongoza, ni kutumia bakaa yako kwa wasio na uwezo badala ya kujilimbikizia mali ambayo kamwe hautakwenda nayo, mnatakiwa kujifunza kwamba kuwatatulia matatizo wengine ni moja ya sadaka kubwa duniani.

Mimi sina cheo chochote, lakini nimemuonea wivu Ruge kwa jinsi alivyozikwa, najua ni mtoto mdogo aliyeishi miongo michache, lakini ameishi miongo mingi kiutumishi na kuwasaidia watu, leo wanamlilia wengi.

Sijui wale wanyapara wangu wa enzi hizo wanajisikiaje leo pamoja na hivyo vyeti vyao walivyotumia kuwanyanyasa waliokuwa chini yao, sijui kama wana muda wa kuomba nafasi tena ili watende aliyotenda mwenzao.

Mwisho, walioko madarakani wameanzaje kubadilika na kujifunza kutoka kwa mwenzao aliyefariki dunia akiwa na amani huku nyuma? Mema yake yamemzika, na wengine watazikwa na waliyoyatenda.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

By Jamhuri