Mimi naamini mazungumzo yoyote kati ya mtu na mtu (au watu) yana maana na madhumuni yake. Yanapata uimara na thamani ya maana yanapojengewa maswali yenye nguvu ya hoja na kupata majibu yaliyosheheni ukweli na usahihi.

Mazungumzo, maswali na majibu hayana budi kulandana kukidhi hoja husika kati ya mtu na mtu (au watu). Mazungumzo yasipopatiwa ustahamilivu na ukweli hayawezi kutimiza lengo na madhumuni yaliyokusudiwa. Yanapokosekana mambo haya, mazungumzo huwa hayana maafikiano au mwisho mwema.

Mkamilishaji wa mazungumzo ni mzungumzaji mwenyewe. Mathalani, hoja fulani inapowasilishwa barazani au mkutanoni, mtoa hoja hana budi kusema ukweli. Na awe fasaha katika kujibu na kufafanua hoja za baraza au mkutano. Anapofanya hivi hupata sifa ya uzungumzaji na hoja yake kukubaliwa. Baraza au mkutano hupata mafanikio.

Kadhalika mtu anayeshiriki mazungumzo awe na uwezo wa kuuliza swali na kujibu hoja. Lakini baadhi ya mazungumzo huwa hayapati matokeo mazuri kutokana na aina ya swali na majadiliano ya hoja au mada inayozungumziwa. Katika hali kama hii waandaaji wa mkutano huwa shakani na kupata hasara. Na mazungumzo yanapoteza maana.

Utaratibu mzuri wa mazungumzo unapatikana kama vile mahakamani, hospitalini au kituo cha usalama. Hata hivyo katika sehemu hizo endapo muhojiwa hatakuwa mkweli, na hakimu, daktari au inspekta hatakuwa makini, tiba ya mazungumzo haitapatikana. Ni dhahiri mazungumzo yamekosa uhai na kuwa mfu.

Usahihi wa jambo au mazungumzo yoyote yanahitaji nidhamu, uvumilivu, ukweli na dhamira sahihi na endelevu. Watu au mataifa yaliyoendelea duniani yanatumia vigezo hivi. Ingawa baadhi ya watu au mataifa yasiyo na uaminifu yamepenyeza kisirisiri (rushwa, dhuluma) kupata maendeleo yao, huku wakiwaumiza watu wanyonge, walalahoi.

Wakati mwingine mazungumzo hayafaulu kutokana na maswali na majibu ndani ya mijadala yalivyowasilishwa. Mara kadhaa nimeshuhudia kwenye vikao wajumbe wakifokeana, wakipigana na wakitimuana, sababu ni maswali na majibu.

Binafsi, naamini ziko aina tatu za swali. Swali elekevu, swali jinga na swali pumbavu. Swali elekevu limesheheni nguvu ya hoja, mwelekeo, uhalisia na ukweli ambao hutoa majibu yenye ufafanuzi, mwanga na toshelezi la moyo. Mazungumzo hunoga na kukubalika.

Swali la kijinga msingi wake ni purukushani ya jambo. Muulizaji anaelewa madhumuni ya mazungumzo, lakini anajifanya haelewi akiwa na nia ya kupotosha au kuleta mzaha, akidhani yeye ni mjanja na mwelevu zaidi ya watu wengine. Kumbe anajiharibu na ana haribu mambo mazuri na kuwa mabaya kwa faida ya wajanja na kwa hasara ya wajinga waliwao.

Swali la kipumbavu chanzo chake ni uzuzu. Mtu hana ajualo lakini atauliza tu ili aonekane anajua na ameuliza. Hatambui kwamba swali lake halina maana katika mjadala au mazungumzo. Na hapa huchafua hali ya hewa na watu kuwa na mshikemshike, huku wakitazamana na kushangaana. Kulikoni?

Ninazungumza haya kutokana na tabia au mwenendo unaofanywa na baadhi yetu Watanzania, kupitia kwenye vikao vya siasa, vikao vya maendeleo na uchumi na vikao vya maadili na usuluhishi kupata majibu machafu. Msingi wa majibu machafu ni namna ya kuwasilisha mada na maswali. Tukitumia kinga ya uhuru wa kuzungumza.

Fujo na sintofahamu zinazopatikana kwenye mitandao ya kijamii hazina kifani. Niliamini mitandao ya kijamii ingetoa mazungumzo bambam kuvuta watu wengi mno kutazama na kujadili mambo murua kwa faida ya wananchi wote nchini. Nilitarajia kupokea mijadala na maswali elekevu, lakini sivyo. Badala yake napokea majadiliano na maswali yenye majibu tatanishi.

Angalia picha na maelezo ya uasherati, sikiliza kauli za dharau na kiburi na malumbano yenye hoja dhaifu ya kufarakanisha watu katika mambo ya kijamii na kisiasa. Kadiri mambo yanavyofanyika ndivyo nchi yetu inavyozama polepole kwenye lindi la uchafu na uhayawani. Si hivyo tu, hata utulivu na amani vimo shakani. Itakuwa hasara ya kujitakia.

Ombi langu kwa wenye mitandao ya kijamii ni kuchukua haraka uamuzi wa kuzuia mabaya ili kunusuru nchi kuzama. Vyombo vya maadili, haki na usalama kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya mambo haya. Tukumbuke serikali ni watu, ni wananchi, ni nchi. Watu wenyewe ni sisi. Tuache kuhadaika na vya mataifa mengine, tuunde vyetu.

Please follow and like us:
Pin Share