Azam imezidi kuonyesha dhamira ya kutetea ubingwa wao baada ya leo kuibuka na ushindi wa mabao 4-0, dhidi ya Jamhuri

Kikosi cha Azam FC, kimezidi kufanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea hapa Zanzibar baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0, dhidi ya timu ya Jamhuri ya Pemba huo ukiwa ni mchezo wa kundi A, uliopigwa majira ya saa 8 mchana uwanja wa Amaan Zanzibar.

Huo ni mchezo wa pili kwa Azam ambao ndiyo mabingwa watetezi na ushindi huo umewafanya kufikisha pointi sita na kuongoza kundi hilo huku wakibakiwa na michezo miwili dhidi ya Simba na URA ya Uganda.

Katika mchezo wa leo Azam walianza kuhesababu bao la kwanza dakika ya 26 mfungaji akiwa ni Benard Arthur aliyeunganisha mpira wa faulo uliopigwa na beki wa kushoto wa timu hiyo Bruce Kangwa.

Bao hilo lilionekana kuwazindua Jamhuri na kucheza soka la kasi na kulisogelea lango la Azam lakini ulinzi wa mabingwa hao watetezi ulikuwa imara kuondoa hatari zote langoni mwao.

Mshambuliaji Mussa Mbarouck alionyesha kuwasumbua sana mabeki Yakub Mohame na Agrey Moris wa Azam lakini hakufanikiwa kufunga bao kutokana na uimara wa kipa Razak Abalora.

Katika dakika ya 38 Jamhuri walilazimika kucheza pungufu baada ya Abduli Mahfudhi kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na nyekundi na kutoka nje kwa kosa la kumchezea rafu mashambuliaji Joseph Mahundi wa Azam.

Azam waliendelea kuliandama lango la Jamhuri lakini hadi filimbi ya mapumziko mabingwa hao watetezi walikwenda mapumziko wakiwa na bao hilo moja lililofungwa Arthur.

Kipindi cha Azam waliingia kwa kasi na kufanikiwa kuandika bao la pili dakika ya 48, kupitia kwa kiungo wake Salmin Hoza, aliyepokea pasi ya Arthur akiwa nje ya eneo la hatari na kupiga shuti kali ambalo lilimshinda kipa Ali Shabani na mpira kutinga nyavuni.

Pamoja na kufungwa mabao hayo Jamhuri hawakuonekana kukata tamaa bali walizidi kupambana kutafuta mabao ya kusawazisha lakini mambo yalikuwa magumu kuipenya ngome ya Azam.

Yahya Zaid aliifungia Azam FC bao la tatu dakika ya 61,  bao ambalo lilitokana na uzembe wa kipa wa Jamhuri Ali Shabani aliyetaka kuudaka mpira wenye nguvu badala ya kuupangua baada ya kosa hilo kipa huyo alitolewa nje na nafasi yake kuchukuliwa na Ali Mrisho.

Badala ya bao hilo kocha wa Azam alionekana kuridhika na matoeo hayo na kuanza kuwapumzisha wachezaji wake wa kikosi cha kwanza kama Arthur, Yakub Mohamed, Yazid na kuwaingiza wachezaji chipukizi Abduli Omary,Abdallah Kher, Shabani Idd na Peter Poul.

Mabadiliko hayo yaliweza kuzaa matunda dakika ya 78 ambapo Peter Poul alifunga bao la nne na la tatu kwake baada ya kazi nzuri iliyofanywa na kiungo Mcameroon Stephen Kingue.

Katika mchezo huo kiungo wa Azam Salmin Hoza alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo kutokana na kuonyesha kiwango bora na kufunga bao la pili kwa timu yake.

By Jamhuri