Shinyanga

Na Antony Sollo

Waziri wa Madini, Dk. Dotto Biteko, ameombwa kufuta leseni ya Kampuni ya El-Hillal Minerals kutokana na walinzi wake kutuhumiwa kumuua kwa risasi mchimbaji mdogo wa madini.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, William Jijimya, amesema Cosmas Kusililwa (25), aliuawa Machi 10, mwaka huu nje ya eneo la El-Hillal Minerals Limited.

“Wachimbaji wadogo (wabeshi) huenda kwenye maeneo hayo kujitafutia riziki kwa kuchimba almasi,” amesema Jijimya.

Kusililwa alikuwa mkazi wa Kijiji cha Igumanghobo, Kata ya Idukilo aliyekuwa akijishughulisha na uchimbaji katika Kijiji cha Mwang’holo.

Pia viongozi kadhaa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamelaani tukio hilo na kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan asitishe leseni ya uwekezaji ya kampuni hiyo kwa kushindwa kuliendeleza eneo alilopewa kwa zaidi ya miaka 15.

Jijimya na Katibu wa CCM wa Wilaya, Peter Mashenji, wamekiita kitendo hicho kuwa ni cha kinyama, wakisema kwa nyakati tofauti kuwa kwa sasa Kishapu hawahitaji mwekezaji mkatili kwa wananchi ambao ndio wapiga kura wao.

“Ni vema Waziri wa Madini (Dk. Dotto Biteko) akamshauri Rais na kuchukua hatua haraka juu ya ukiukwaji huu wa haki za binadamu,” amesema Mashenji.

JAMHURI lina taarifa za ukiukwaji wa haki za binadamu ndani ya mgodi huo jirani na Mgodi wa Williamson, ikidaiwa kuwapo kwa wananchi wengi waliopata ulemavu wa kudumu.

Askari wa kampuni binafsi wanaolinda kampuni hiyo ndio wanaodaiwa kutumia nguvu kupita kiasi na kuwanyanyasa wananchi, hivyo kusababisha takriban watu 71 kupata majeraha ya kudumu.

“Kwa mwaka jana watu hawa ambao ni wakazi wa Mji Mdogo wa Maganzo na vijiji jirani wilayani Kishapu wamelipwa jumla ya Sh bilioni 14 kama fidia kutokana na kuumizwa na kutiwa ulemavu wa kudumu na walinzi wa Mgodi wa Williamson Diamonds Limited,” amesema.

Wadau wa haki za binadamu wanaofanya shughuli zao mkoani Shinyanga wanakiri kuwapo kwa matukio ya ukatili kwa raia na taarifa za mauaji yanayotokea migodini, wakiiomba serikali kuunda tume kuchunguza matukio hayo.

By Jamhuri