Miradi ya kiuchumi inaua lengo la dini?

Imani za kishirikina zimeendelea kushika kasi nchini, kiasi cha watu wengi kuamini kuwa dini zimeweka kando majukumu ya kiroho na kujikita katika miradi ya kiuchumi.

Kitendo cha wazee wawili kuzikwa wakiwa hai katika Wilaya ya Momba mkoani Mbeya, ni miongoni mwa matukio yanayoashiria upungufu wa mafundisho ya dini katika jamii.

 

Ernest Molela (60) na Mizinala Nachela (50) walipigwa hadi kuzirai kabla ya kuzikwa pamoja na marehemu Nongwa Hussein kwenye kaburi moja, baada ya kutuhumiwa kumuua kishirikina. Huo ni ukatili kupindukia!

 

Hussein alifariki baada ya kuugua kwa muda mrefu, lakini baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Karungu waliamini kuwa ameuawa na wazee hao katika mazingira ya kichawi.

 

Imani za kichawi zimeendelea kuchochewa na makundi ya watu wachache waliopachikwa majina ya ‘lambalamba’ na ‘nyaunyau’, yanayolazimisha kujipatia riziki kwa njia haramu miongoni mwa wananchi.

 

Watu hao wamejibandika hadhi za waganga wa jadi wakiilaghai jamii kwamba wana uwezo wa kusafisha nyota, kuleta utajiri na neema nyingine kwa wenye matatizo mbalimbali.

 

Wamejikita katika utapeli wa kupiga ramli, kueneza imani za kichawi, kuchonganisha watu na kupanda chuki katika jamii kwa nia ya kujipatia fedha, mifugo na mali nyingine.

 

Matapeli hao wamekuwa wahamasishaji wakuu wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), kwa kudanganya watu kuwa viungo vya kundi hilo la jamii vinawezesha utajiri wa haraka kupitia shughuli za uchimbaji madini, uvuvi na siasa.

 

Kwa bahati mbaya, watu wengi, pasipokujua kuwa huo ni utapeli tu, wamekuwa na mwitikio mkubwa wa kukumbatia imani za kishirikina katika maisha yao ya kila siku.

 

Kibaya zaidi ‘lambalamba’ na ‘nyaunyau’ hao wamekuwa wakiwatafuta wanawake wa kuwapikia chakula na kufanya nao ngono, hali inayochangia maambukizi ya magonjwa ya zinaa na ukimwi katika jamii.

 

Ni wazi kuwa matapeli hao wanahatarisha usalama, amani, utulivu na afya za watu kama si kusababisha wananchi hasa vikongwe na albino, kuishi kwa hofu na kushindwa kushiriki shughuli za kijamii na ujenzi wa Taifa.

 

Viongozi wengi wa dini wamejikita zaidi katika uhamasishaji wa miradi ya kiuchumi ikiwamo ya elimu kuliko kuijenga jamii katika misingi ya kiroho na maadili.

FIKRA YA HEKIMA inawakumbusha viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini, kutambua kuwa wana changamoto kubwa ya kusaidiana na Serikali kudhibiti imani za kishirikina na matendo ya kikatili katika jamii.


Kasumba inayoendelea kushamiri ya viongozi wa dini kuelekeza nguvu kubwa katika kuhamasisha miradi ya uzalishaji mali, na kupunguza kasi ya kuimarisha mafundisho ya kiroho katika jamii, ni chukizo hata mbele za Mungu.

Wajitambue na kujisahihisha.


By Jamhuri