Polisi mkoani Tanga, wanafanya kila linalowezekana ili gari la askari wa Jeshi hilo lililokamatwa likiwa na wahamiaji haramu 10 liachiwe.

Duru zinaonyesha kuwa polisi wamekuwa kwenye msuguano na Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Tanga, wakitaka gari la mwenzao lisiendelee kushikiliwa na hatimaye litumiwe mahakamani kama kielelezo.

“Polisi wanapambana kuhakikisha gari la mwenzao linaachiwa kwa kigezo kuwa ni la biashara kwa hiyo liachiwe na siku ya kesi lipelekwe mahakamani. Uliona wapi kidhibiti kinaachiwa kabla ya kufikishwa mahakamani? Huo siyo utaratibu. Kwa kawaida gari linapokamatwa likisafirisha wahamiaji haramu linapaswa litumike kama kilelezo.

“Tukipeleka watuhumiwa mahakamani bila gari lililotumika kuwasafirisha hatuwezi kufanikiwa kwenye kesi. Sasa polisi wanataka mwenzao aachiwe ili liendelee na kazi, huo siyo utaratibu hata kidogo.

“Suala hili limeibua msuguano mkali kati ya vyombo hivi  (Polisi na Uhamiaji) kwa sababu hawataki litaifishwe.

“Hivi tunavyozungumza wameshapanga gari hilo liondolewe polisi ambako linashikiliwa. Kwanini magari mengine hayaachiwi, lakini hili liachiwe? Polisi hapa wanakwamisha kazi za Uhamiaji. Tunapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano,” kimesema chanzo chetu cha habari kutoka Tanga.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa gari hilo lenye namba T565AHQ linamilikiwa na Meja Khamis wa Kituo cha Polisi Mabawa, Tanga Mjini.

Lilikamatwa Desemba 6, mwaka jana likiwa na Waethiopia 10 ambao ni Eshetu Leilago (14), Melkamu Abebe (30), Adisu Erkalo (15), Temesgn Almu (22),

Desta Diga (18), Take Abane (13), Efrem Enetros (17),

Arag Belora (18), Muluglet Ansoi (12) na Damo Mane (12).

Pia walikuwamo Watanzania wanne wanaotuhumiwa kujihusisha na usafirishaji wahamiaji hao. Watanzania hao ni Mohamed Musa (32) ambaye ni dreva, Mbezi Omary Kibio (36) – utingo; Swalehe Khamis (18)- utingo na Said Fadhil (18) ambaye pia ni utingo.

Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) Mkoa wa Tanga, Aziz Kimatta, amezungumza na JAMHURI na kusema Mahakama ndiyo yenye uamuzi wa mwisho kuhusu gari linalokamatwa likiwa limepakiwa wahamiaji haramu.

Alipoulizwa kama ni kweli gari lililokamatwa na wahamiaji hao linamilikiwa na askari polisi, Kimatta, hakuwa tayari kujibu swali hilo lakini akasisitiza kuwa Mahakama ndiyo yenye uamuzi.

By Jamhuri