kipandeAliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, Madeni Kipande, ameng’olewa rasmi katika wadhifa huo baada ya uchunguzi wa Serikali kubaini kuwa hana sifa za kuongoza Bandari.
  Kwa mujibu wa Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Kipande amekuwa na mahusiano mabaya kazini, ana uamuzi wa papara na amefifisha uhusiano kati ya Bandari na wateja.
 Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Uchukuzi wiki iliyopita, ilisema:  


“Itakumbukwa kuwa mnano tarehe 16 Februari, 2015, Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Samuel Sitta (Mb), alimsimamisha kazi kwa muda Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, Ndugu Madeni Kipande, kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali dhidi yake.
“Tume aliyoiteua Mheshimiwa Waziri kuchunguza suala hili, ilikamilisha kazi yake mnano tarehe 20 Machi, 2015 na kumkabidhi taarifa ya uchunguzi wao mnamo tarehe 24 Machi, 2015 kwa hatua zaidi.


  “Baada ya kuisoma taarifa ya Tume na hatimaye kushauriana na taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala haya, tumeridhika pasipo mashaka yoyote kwamba isingefaa Ndugu Madeni Kipande kuendelea na kazi ya kuongoza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari.
“Hii ni kutokana na kudhihirika utawala mbovu aliouendesha uliosababisha manung’uniko mengi miongoni mwa wateja na wadau wa Bandari, na mgawanyiko mkubwa wa wafanyakazi.


“Kutokana na hali hiyo, Serikali imeamua kumrejesha Ndugu Madeni Kipande Idara Kuu ya Utumishi ili aweze kupangiwa majukumu mengine. Ndugu Awadh Massawe ataendelea kukaimu nafasi hiyo ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari.
Taarifa hiyo imetolewa na Wizara ya Uchukuzi, 16 Aprili, 2015.


Kipande alisimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa wiki mbili kutokana na tuhuma za kuwa na mahusiano mabaya kazini na wafanyakazi wenzake, kuingilia mchakato wa zabuni na kubughudhi wateja wa Bandari.
Kipande aliyekuwa amesifiwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), chini ya Mwenyekiti wake Zitto Kabwe katika Mkutano wa 18 wa Bunge uliomalizika Dodoma hivi karibuni kuwa ni mtendaji mahiri, alishushiwa rungu na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, kwa alichodai kuwa ni matumizi mabaya ya madaraka.


Sitta aliitisha mkutano na waandishi wa habari Bandarini, kisha akavifahamisha vyombo vya habari ifuatavyo:     
“Nimemsimamisha  kazi kwa muda Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, Ndugu Madeni Kipande, leo hii tarehe 16 Februari, 2015  ili kupisha uchunguzi unaohusu tuhuma mbalimbali zinazomkabili.
“Tuhuma hizo ni pamoja na manung’uniko kuhusiana na ukiukwaji wa taratibu za manunuzi. Hali hii inatokana na kutotabirika kwa taratibu na kukosekana kwa uwazi, pamoja na taratibu hizo kuingiliwa na Mamlaka.


“Aidha, tuhuma nyingine ni mahusiano yasiyoridhisha kati ya uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari na wadau wake muhimu na mahusiano mabaya sehemu ya kazi.
“Kufuatia hali hii, nimeteua Tume ya kuchunguza suala hili na nimeipa muda wa wiki mbili kukamilisha kazi hii na kunipatia taarifa. Majina ya wajumbe wa Tume hiyo ni kama ifuatayo: Jaji mstaafu Agusta Bubeshi – Mwenyekiti, Ndugu Ramadhani Mlingwa – Mjumbe, Eng. Samson Luhigo – Mjumbe, Ndugu Happiness Senkoro – Mjumbe, Ndugu Flavian Kinunda – Mjumbe na Ndugu Deogratius Kasinda – Katibu.


“Wakati Ndugu Kipande  akiwa amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi, kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa na Sheria ya Bandari Namba 17 ya mwaka  2004 kifungu cha 34 kifungu  kidogo cha 2, ninamteua Meneja wa Bandari Dar es Salaam, Bwana Awadh Massawe, kukaimu nafasi hiyo kuanzia leo tarehe 16 Februari, 2015.
 Samuel Sitta (Mb), Waziri wa Uchukuzi, 16 Februari  2015.
  Kwa mujibu wa kifungu cha 20 cha Sheria ya Bandari Na. 17 ya mwaka 2004, Waziri mwenye dhamana (Uchukuzi) anaweza kutoa maelekezo yoyote kwa nia ya kulinda usalama wa nchi au mahusiano kati ya Tanzania na nchi nyingine, iwapo watumishi wa Bandari wanafanya matendo yenye kuhatarisha usalama au uhusiano wa Tanzania na nchi nyingine.


  Kifungu cha 34 (2) kinampa Waziri mamlaka ya kuteua mtu mwenye sifa zilizotajwa na sheria kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari baada ya Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (anayoiteua yeye pia) kupendekeza kwake majina matatu. Sitta alitumia kifungu hiki.
Iwapo Tume isingempata na hatia katika makosa aliyotuhumiwa nayo, basi Kipande angerejeshwa kazini, na kwa Tume kumkuta na hatia, kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 9 ya mwaka 2011 kifungu cha 87, mtumishi aliyekutwa na makosa anapaswa kushitakiwa chini ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 au sheria nyingine kudhibiti uhalifu husika.


Kwa upande wake, Kipande alikaririwa na gazeti la Nipashe mwezi uliopita akisema ameonewa na kwamba hakupewa nafasi ya kujitetea kabla ya kusimamishwa kazi, ila akasema anasubiri majibu ya uchunguzi.
Majibu ya uchunguzi yametoka na kumtia hatiani, ambapo sasa anarudishwa Idara ya Utumishi kupangiwa kazi nyingine.

By Jamhuri