Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Bin Shaaban Simba, amevitaka vyombo vya dola kufuatilia kwa makini baadhi ya misikiti inayodaiwa kutumiwa na baadhi ya waumini wake kufanya mazoezi nyakati za usiku.
 Akizungumza na JAMHURI katika mahojiano maalum yaliyofanyika hivi karibuni, Mufti alionesha kushangazwa baada ya kusikia kuwa kuna baadhi ya misikiti nchini imekuwa ikitumika kufanyia mazoezi usiku baada ya ibada.
 Akizungumza kwa umakini, Mufti Simba anasema kuwa hilo ni jambo la ajabu maana hakuna mahali popote katika dini ya Kiislamu inakoelekeza hivyo.


 Anasema hafahamu kama nyumba hizo za ibada zinatumika kwa ajili ya kufanyia mazoezi, lakini siyo sahihi kutumika kwa ajili ya kufanyia mazoezi nyakati za usiku.
  Mufti Issa Bin Shaaban Simba anahoji sababu za waumini hao kufanya mazoezi katika misikiti nyakati za usiku, huku wakijua wazi kuwa hakuna mahali popote vitabu vitakatifu (Quran) vilipoelekeza  kufanya hivyo.


 “Haya mambo hayatokani na taratibu za dini ya Kiislamu, hili jambo siyo sahihi kabisa, hatuna utaratibu huo katika miongozo ya dini yetu, hapa ipo haja ya vyombo vya ulinzi na usalama kutazama na kufuatilia kwa makini hawa wanaofanya hivyo ni kina nani na wana dhamira gani!” anasema Mufti Simba.
 Anabainisha kuwa Waislamu wana shule wanazomiliki, na katika shule hizo hakuna hata moja inayofundisha kufanyika kwa mazoezi katika nyumba za ibada, bali kama wanahitaji kufanya mazoezi ya viungo huyafanya katika viwanja vya wazi na nyakati za mchana na si usiku.
“Mimi binafsi nashindwa kabisa kuliongelea hili kwa undani maana halipo kwenye imani zetu, pia misikiti inayofanya hivyo siifahamu ila ni vyema vyombo vya dola vikawa makini na hili ili kujiridhisha na kuchukua hatua ikibidi,” anasema Mufti.


  Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, anaeleza kuwa ni vyema nyumba za ibada zikatumika kwa shughuli za ibada tu na si vinginevyo.
  Chikawe aliyezungumza na gazeti hili, anasema kuwa msikiti ni nyumba ya kufanyia ibada, ni mahala patakatifu hivyo haiwezekani kuigeuza kuwa nyumba za kufanyia mazoezi (gym) kama ambavyo inafanywa na baadhi ya watu.


  Pia alihoji sababu za kufanyika kwa mazoezi hayo katika nyumba hizo za ibada. “Wanajifunza karate na kupigana ili iweje? Wanataka kupambana na nani hasa? Tena wanafanya kwa kificho, nyakati za usiku ndani ya nyumba za ibada ili itokee nini?”Anasema na kuongeza: “Kama wana nia njema, basi hawana sababu za kufanya mazoezi hayo usiku tena kwenye nyumba za ibada”.
 Hata hivyo, alilitaka gazeti hili kuwasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, ili kupata ufafanuzi wa kina kuhusiana na suala hilo.


  IGP Mangu akizungumzia sakata hilo, anaeleza kuwa jeshi hilo linahusika na makosa ya jinai, hivyo anaomba kupatiwa orodha ya nyumba hizo za ibada zinazojihusisha na kufanya mazoezi hayo ili Jeshi la Polisi liweze kufuatilia.
 “Tuleteeni majina ili tufuatilie tuweze kujua ni mazoezi gani yanayofanywa humo nyakati za usiku, kama ni kosa la jinai tutakuja tuseme, kwa sasa siwezi kukwambia lolote bali nipe majina… inaonekana kuna kitu mnajua zaidi,” anasema Mangu.
  Wiki iliyopita, watu 10 walikamatwa katika msikiti wa Sunni uliopo Kidatu, Wilaya ya Kilombero, wakituhumiwa kuhusika na vitendo vya ugaidi.


  Watu hao walikamatwa baada ya wasamaria wema kuliarifu Jeshi la Polisi kuhusu uwepo wa watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu katika msikiti huo.
  Mmoja wa viongozi wa Msikiti wa Masjid Salah Al-Fajih, Mohamed Manze, anasema kuwa wao kama viongozi na waumini msikitini humo hawakuwa na taarifa zozote za ujio wa watuhumiwa hao, na kwamba wapo vijana wanne tu ambao wamekuwa wakilala na kujisomea msikitini humo.
  Kiongozi huyo anasema kuwa hawakupendezwa na suala hilo na kwamba limewachafua na kuwaharibia sifa waumini wa msikiti huo.


  Katika tukio hilo, Hamadi Makwendo aliuawa kwa kupigwa risasi na askari baada ya kumjeruhi askari kwa kumkata kwa jambia.

By Jamhuri