LONDON

England

Yamebaki mataji matatu yanayoshindaniwa kwa sasa England; timu mbili kubwa, Liverpool na Manchester City zote zinayahitaji. Swali ni nani atashinda nini na kujiandikia historia?

Kiungo wa zamani wa Liverpool, Danny Murphy, anachambua.

Inaonekana kana kwamba wiki chache za mwisho kwa msimu huu zitakuwa na mchuano mkali kati ya Liverpool na Manchester.

Kwa viwango vinavyoonyeshwa na timu hizi katika miaka ya karibuni, ni wazi kuwa hizi ndizo timu bora kwa sasa England zikiziacha nyingine mbali kabisa. 

Uthabiti wao ni wa kushangaza na zote zina vikosi imara – ndiyo maana wote wana nafasi sawa za kushinda mataji matatu yaliyosalia.

Kwa hakika huwezi kujua ni kikosi gani cha Liverpool kitakachoanza mechi fulani, hasa safu ya ushambuliani; wala huwezi kubashiri ni nini bosi wa City, Pep Guardiola, atakachokifanya kuchagua timu ya kwanza.

Hebu tuzitazame mechi zinazozikabili timu hizi, kwa kuwa zitakuwa za nguvu na za kuvutia, hasa pale zenyewe zitakapokutana ndani ya wiki chache zijazo.

Hii itatokea walau mara mbili – kwanza ni Aprili 10 katika Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Etihad – kisha nusu fainali ya Kombe la FA ndani ya Wembley wiki moja baadaye. Lakini pia upo uwezekano wakakutana kwenye fainali ya Kombe la Mabingwa Ulaya, Mei 28.

Inafurahisha sana. Kwa kawaida shabiki wa soka hupenda kutazama timu bora – zenye wachezaji na makocha bora – zikipambana katika hatua kubwa kama sasa, kukiwa na shinikizo kubwa ndani na nje ya uwanja. 

Ni vitu fulani vidogo vidogo ndivyo huamua mambo makubwa pale pande mbili zenye uwezo mkubwa kama Liverpool na City zinapokutana.

Unatamani mechi kama hizi kumalizika kwa kuona vitu vikubwa vikitokea, lakini bado inaweza kuwa ni makosa madogo tu – mtu mmoja amejisahau wakati mpira wa adhabu ndogo unapigwa.

Kwa sasa, Liverpool haionekani kufanya kosa kama hilo. Kikosi cha Jurgen Klopp kinafahamu namna ya kumaliza kazi wakati hakichezi vizuri, kitu ambacho kwa wiki kahaa za sasa City hawana, kutokana na ukweli kwamba siku hizi ‘Reds’ hawafungiki kirahisi. 

Kwa kiasi kikubwa ni kwa sababu ya kuwa ni golikipa imara, Alisson, ambaye yupo katika kiwango cha juu; pamoja na walinzi bora, lakini pia ni kutokana na kuwa na hamu ya ushindi wanapoona kuwa mambo yanawaendea vema.

Ninafahamu jinsi ilivyo pale unapowaona adui zako wakikosa nafasi muhimu; unapata nguvu za kukuwezesha kushinda mchezo huo.

Tumeliona hili likitokea kwenye Kombe la FA kati ya Liverpool na Nottingham Forest, wachezaji walipoona kuwa huo ndio wakati wao. Hivi ndivyo Liverpool inavyoonekana, tofauti na City.

Liverpool tayari wamepata mzuka kwa kupunguza tofauti ya pointi iliyokuwapo kati yao na City kwenye Ligi Kuu kutoka pointi 14 Januari 15, mwaka huu na kubakiza tofauti ya pointi moja; wakiingia nusu fainali ya Kombe la FA huku wakipangwa dhidi ya Benfica katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa. Kujiamini kumeongezeka Anfield.

Nusu fainali ya Kombe la FA haitakuwa na shinikizo kubwa kwa timu zote mbili, lakini kutakuwa na utofauti katika uchaguzi wa vikosi.

Tayari Liverpool wameshachukua kombe moja la nyumbani msimu huu, City wakiwa wameshashinda mataji mengi ya aina hiyo misimu iliyopita. Kwa hiyo ninadhani kwa sasa timu zote zinakubaliana kuwa kwa umuhimu kombe hili ni la mwisho kati ya matatu.

Mengine mawili ndiyo makubwa zaidi, nionavyo mimi kila mmoja atashinda kombe moja.

Sijui ni kwa nini, lakini ninadhani Liverpool watashinda ubingwa wa Ligi Kuu.

Mechi kati yao kwenye Uwanja wa Etihad ni ya muhimu sana kwa kuwa yeyote atakayetoka akiwa anaongoza ligi, itakuwa si rahisi kukamatwa tena – sioni timu hizi zikipoteza pointi nyingi baada ya hapo.

Ni muhimu kwa Liverpool kushinda mechi hiyo, kwa kuwa Kloppp ameshinda mara moja tu kwenye Ligi Kuu hapo Etihad tangu mwaka 2015, lakini nina hisia kwamba ‘Reds’ wataibuka kidedea.

Kwa upande mwingine, ninadhani mwaka huu ni wa City kwenye Ligi ya Mabingwa. Lengo la ujumla unapozungumzia mashindano ya soka, ni kuendeleza au kuukaribia ushindi mara kwa mara.

Fanya kama ambavyo City wanafanya kwenye mashindano ya Ulaya na ipo siku utashinda.

Kama nimekosea na City wakamaliza msimu mikono mitupu au Liverpool wakaambulia Kombe la Carabao pekee, maana yake msimu wao utakuwa hauna maana.

Si upande wangu, hapana. Kwangu msimu mbaya utakuwa pale ambapo Manchester United itaishia kukamata nafasi ya tano hivyo kukosa nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa huku pia ikitoka bila kombe lolote kwa mara nyingine.

Itakuwa mbaya sana kwa hakika, lakini kama City au Liverpool wataishia nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu, Klabu Bingwa ya Ulaya na Kombe la FA, kwangu ni sahihi au karibu kabisa na kuwa sahihi.

Kwa timu hizi mbili, kufika hapo walipo maana yake vikosi vyao vimekuwa na mwendelezo mzuri kabisa kwa msimu mzima, wakicheza sawia soka la ndani na la kimataifa kwa miezi minane.

Kwa hiyo, chochote kitakachotokea baadaye, tayari ulikuwa ni msimu mzuri sana kwa Liverpool na City, lakini unaweza kuwa msimu mzuri zaidi.

By Jamhuri