Mheshimiwa Rais tuwekeze zaidi vijijini 

DAR ES SALAAM

NA DK. FELICIAN B. KILAHAMA 

Ni jambo la kumshukuru Mungu aliye muweza wa yote kwa kutujalia uhai na afya njema baada ya kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. 

Akiwa Makamu wa Rais, aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania kutokana na kifo cha mtangulizi wake, Dk. John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021.

Kulingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais aliye madarakani akifariki dunia; Makamu wake anaapishwa kuliongoza taifa. Hivyo Machi 19, 2021, Samia akaapishwa kuwa Rais wa Sita wa Tanzania. Hali hiyo ilitokea muda mfupi baada ya kumaliza Uchaguzi Mkuu (Oktoba, 2020) na kuanza kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Tano. 

Sasa ni mwaka mmoja tangu Samia aapishwe kuliongoza taifa letu. Tunamshukuru Mungu kwa mabadiliko hayo ya uongozi wa juu kufanyika kwa mujibu wa Katiba bila kulazimika kufanya uchaguzi. 

Nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mungu, muumba wa mbingu na dunia pia mwingi wa rehema, kwa kutujalia kuendeleza vema utawala wa taifa letu kwa utulivu na amani. 

Pili, nampongeza Rais Samia kwa kuiongoza Tanzania kwa ujasiri mkubwa akiwa ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa juu kabisa nchini.

Nimebahatika kusikiliza sehemu ya mahojiano kati ya Rais Samia na Mkurugenzi Mkuu wa TBC (Ayub Rioba). Nilifarijika Rais aliposema kwamba yeye ni sehemu ya Serikali ya Awamu ya Tano na kuongeza kuwa yeye na Magufuli walikuwa wakishirikiana vizuri. 

Akafafanua kuwa walishirikiana katika kupanga mambo muhimu kwa mustakabali wa taifa. Akaongeza kuwa wakati Magufuli akiweka nguvu kwenye masuala ya ndani ya nchi; yeye alikuwa akiwakilisha Tanzania katika masuala ya kimataifa. 

Kwa kufanya hivyo, Magufuli alimsaidia makamu wake kupata uzoefu wa kutosha na kwa mambo mengi ya msingi kwa faida ya taifa.

Baada ya kuapishwa kuwa Rais ndani ya kipindi kilichosalia cha Awamu ya Tano; hakuona shida wapi pa kuanzia maana alikuwa sehemu ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati iliyolenga kuchochea maendeleo endelevu kwa taifa. 

Nilifarijika Rais Samia aliposema miradi mikubwa ni masuala muhimu ya kipaumbele na atahakikisha inakamilishwa kwa wakati. Alisisitiza kuwa miradi na mipango ya maendeleo iliyopitishwa ya Awamu ya Tano atahakikisha inatekelezwa ipasavyo kwa faida ya Watanzania. 

Vilevile, akiwa Rais wa Sita, anaweza kutekeleza miradi mingine ambayo ataona inafaa kuinua hali ya maisha ya Watanzania na maendeleo ya taifa kwa ujumla. Kimsingi ni mwelekeo mzuri aliouonyesha Rais Samia ndani ya mwaka mmoja na inatia moyo; hongera sana Rais. 

Taifa kamili linakuwa na mipaka inayotambulika na ndani yake kuna watu wanaishi wakifanya shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi. 

Tanzania ina vigezo hivyo na Rais wa kwanza, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema: “Ili taifa liendelee tunahitaji vitu muhimu vinne: ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora.” Pamoja na hayo pia aliwahi kusema maadui wakubwa nchini ni: ‘ujinga, umaskini na maradhi’

Watanzania tunaishi mijini na vijijini lakini asilimia zaidi ya 70 wanaishi vijijini ingawa namba inazidi kuongezeka mijini (sensa ya mwaka huu itaainishi hali halisi ilivyo). 

Pamoja na huduma za kijamii kupewa umuhimu, hali bado haijatengemaa vizuri hasa maeneo mengi vijijini. Mwaka jana (Desemba 9, 2021) tuliadhimisha miaka 60 ya uhuru na miaka 58 ya Muungano. 

Hiki si kipindi kifupi lakini kwa uhalisia bado tunajitahidi kutokomeza maadui wa maendeleo yetu.

Namshukuru Mungu kwa kunijalia kupata fursa ya kutembelea sehemu mbalimbali vijijini. Pamoja na kuipongeza serikali kwa juhudi zake za kuimarisha huduma za kijamii hususan katika nyanja za elimu, afya, maji, kilimo/mifugo na miundombinu (barabara, umwagiliaji na umeme) lakini pia nathubutu kusema bado kazi kubwa ipo mbele yetu. 

Sasa Rais Samia kwa dhamira yako njema ya kuwa na miradi mingine mbali na ile ya awali; kwa heshima na taadhima nikuombe uangalie namna ya kuinua hali za maisha vijijini kati ya mwaka huu 2022 na 2025. 

Ushauri wangu ni kutoa kipaumbele cha pekee (kuweka mkazo) ili kuinua zaidi hali ya maisha vijijini. Kwa uzoefu nilionao, bado maeneo mengi vijijini hali ni ngumu kimaisha. 

Masuala ya umaskini na maradhi bado ni changamoto kubwa kwa wengi ingawa tumejitahidi kupigana na ujinga lakini nguvu zaidi inahitajika. Mbinu za kilimo na ufugaji bado duni maana misingi ya kilimo hai na ufugaji kibiashara havizingatiwi vya kutosha. 

Kadhalika, masuala ya miundombinu ya barabara vijijini hali si ya kuridhisha kama ilivyo katika sehemu za miji. Mheshimiwa Rais, ukiwekeza kwenye halmashauri za wilaya takriban 139 katika wilaya 134 kwenye mikoa yote; kwa kujenga barabara ambazo zitapitika mwaka mzima pamoja na miundombinu mingine ya huduma za kijamii na utaalamu wa kuvuna na kuhifadhi maji mengi ya mvua badala ya kuyaacha yapotelee mabondeni vikaimarishwa ipasavyo; na huduma ya umeme ikapatikana karibu vijiji vyote (zaidi ya 12,000); uongozi wako utakuwa umechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo endelevu nchini Tanzania. 

Isitoshe, wataalamu wa kilimo/ufugaji na uhifadhi wa misitu, wanyamapori na utunzaji mazingira wakawepo wa kutosha na wakawezeshwa kutimiza wajibu wao ipasavyo; maendeleo vijijini yatadhihirika ifikapo mwaka 2025 kwa kupata matokeo chanya haraka. 

Kadhalika, TARURA iweke mkazo wilayani na vijijini ili ifikapo mwaka 2025 maeneo mengi vijijini, katika halmashari za wilaya, yawe yanapitika mwaka mzima. 

Nia ni kuwezesha sehemu kubwa ya Tanzania kusambaza pembejeo kwa urahisi na kwa bei rafiki kwa wakulima na wafugaji, lakini pia kufungua fursa nyingi za masoko na biashara kwa mazao mbalimbali ya kilimo na ufugaji. 

Huduma za ugani katika kilimo, ufugaji, misitu, uvuvi, wanyamapori na utunzaji mazingira ziimarishwe ili wakulima/wafugaji watumie ardhi vizuri na kupata mazao mengi bila kuathiri ubora wa mazingira. Juhudi hizo pamoja na kuongeza nguvu kusambaza na kuimarisha huduma za afya, maji na elimu; hakika tutainua hali za maisha kwa wananchi wengi vijijini. 

Angalau hali ya mawasiliano si mbaya kama ilivyokuwa zamani, mathalani mtandao wa Halotel umesambaza huduma zake zaidi vijijini. Mitandao mingine pia hawako nyuma, ingawa wamejiimarisha zaidi maeneo ya mijini. 

Tukiwa na dhamira thabiti, kuweka uzalendo mbele na fedha zinazopatikana zikasimamiwa na kutumika ipasavyo (tukaondokana na roho za ubinafsi na udanganyifu) wakati huohuo, viongozi kwa ngazi zote wakawajibika ipasavyo, hakika tutafanikiwa.