DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Wiki iliyopita Tanzania iliungana na dunia kuadhimisha Wiki ya Maji ambapo maadhimisho hayo yalifanyika Mkoa wa Pwani kwa uzinduzi wa mradi wa maji Mlandizi – Mboga – Chalinze huko Msoga na baadaye kitaifa Dar es Salaam ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alikabidhiwa ripoti za utendaji bora wa baadhi ya Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira (WSSAs).

Mengi yalisemwa na Rais Samia na wadau wengine wa maji, Wizara ya Maji, Dawasa na watoa huduma kuhusu hali ya upatikanaji wa maji nchini, changamoto zake na malengo ya serikali kufikia asilimia 95 ya mijini na 85 vijijini mwaka 2025.

Si lengo la makala hii kurudia yaliyosemwa na Rais Samia bali kuangalia kwa namna gani Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ilivyofanikiwa hadi leo.

Ewura ni moja ya mamlaka za udhibiti nchini iliyoanzishwa mwaka 2006 kwa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ya 2001 (Sura ya 414 ya Sheria za Tanzania). 

 Ewura pia ina majukumu chini ya Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 (Sura ya 392 ya Sheria za Tanzania) kudhibiti shughuli za mkondo wa kati na wa chini wa petroli (mafuta na gesi asilia) Tanzania Bara za kusafisha au kuchakata mafuta ghafi au gesi asilia, kusafirisha, kusambaza na kuuza mafuta na gesi asilia.

Majukumu makubwa ya Ewura ni kutoa leseni za uendeshaji wa shughuli za nishati na maji nchini, mapitio ya ushuru, utendaji wa ufuatiliaji wa viwango, ubora, usalama, afya na mazingira. 

EWURA pia ina wajibu wa kukuza na kuendeleza ushindani wenye tija kiuchumi, kulinda masilahi ya walaji na kuendeleza upatikanaji wa huduma zilizowekwa kwa watumiaji wote, ikiwa wa kipato cha chini, watumiaji wa vijijini na sekta nyingine.

 Je, tangu ianzishwe, Ewura imefanikiwa kwa kiasi gani kudhibiti sekta ya maji, inakabiliwa na changamoto gani na kwa namna gani imeweza kuzitatua na nini matarajio yake yajayo? Makala hii inaeleza kwa uchache mafanikio hayo adhimu.

 Meneja Mawasiliano kwa Umma Ewura, Titus Kaguo, anasema tangu mamlaka ianzishwe mwaka 2006, Ewura imefanikiwa katika mambo mengi, ikiwamo kuziwezesha Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira za mikoa, kitaifa na wilaya (WSSSAs).

Kaguo anasema Ewura imekuwa ikiziwezesha WSSAs kuandaa mipango kazi ya biashara ili kuongeza huduma za maji na ubora kwa kuzishindanisha kwa utendaji bora na mshindi kuzawadiwa.

Anasema kila mwaka Ewura imekuwa ikitaja mamlaka za maji zinazoshinda katika ngazi ya wilaya au mikoa na kitaifa katika ripoti yake ya utendaji ya mwaka, na mwaka huu washindi wa mwaka wa fedha wa 2020/21 walitajwa mbele ya Rais Samia.

Katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Maji kitaifa, jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godfrey Chibulunje, alimkabidhi Rais Samia ripoti za utendaji za Ewura ikiwamo ya utendaji wa mamlaka hizo ili azizindue rasmi.

Mhandisi Chibulunje alizitaja baadhi ya WSSAs zilizofanya vizuri kwa mwaka huo ulioishia Juni 2021 na kuzawadiwa Sh milioni 25 mshindi wa kwanza, Sh milioni 15 kwa mshindi wa pili na Sh milioni 10 kwa mshindi wa tatu kwa makundi mawili ya washindi, WSSA za ngazi ya wilaya na za mikoa na kitaifa.

WSSAs zilizotajwa kufanya vema katika utendaji wake ni pamoja na Moshi, Kahama, Iringa, Makambako, Nzega na Igunga. Fedha hizo zilielekezwa kusaidia uunganishaji huduma za maji shule za sekondari na vituo vya afya vya maeneo yao.

Pia Kaguo anasema EWURA huzipiga msasa WSSAs ziweze kuimarisha utoaji huduma za maji na usafi wa mazingira kwa wananchi, kuzijengea uwezo wa kuhakiki taarifa za utekelezaji wa majukumu ili ziweze kuandaa taarifa ya jumla ya utendaji.

Kaguo anasema Ewura huandaa semina kuhakikisha wadau wote wa sekta ya maji wanapata uelewa kuhusu EWURA inavyoandaa taarifa za utendaji kazi na ushiriki wao na vigezo vinavyotumika kupima utendaji wa Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira.

 Anasema mpango wa upimaji utendaji kazi za WSSAs ni wa uwazi na umelenga kuhakikisha zinaimarisha ukusanyaji mapato, utoaji huduma na kuzingatia viwango vya ubora.

Kwa mfano, Kaguo anasema upimaji wa utendaji wa WSSAs wa mwaka 2019, ulijikita kuangalia pia uwepo wa mkataba wa huduma kwa mteja katika kila mamlaka ambapo zaidi ya wadau 100 kutoka Wizara ya Maji, Ofisi ya Rais – TAMISEMI na watendaji kutoka Mamlaka za Maji za Wilaya, Miji Midogo, Mikoa na Miradi ya Kitaifa walishiriki semina ili kuelimishwa.

Kaguo anasema ni kutokana na kufanya vema kwa WSSAs, Ewura nayo hujikuta ikifanya vema majukumu kama taasisi mama, ikiwa imeweka historia ya kupata hati safi ya ukaguzi wa mahesabu kwa miaka 14 tangu ianzishwe mwaka 2006 hadi mwaka 2020.

Ndiyo maana haikuwa ajabu Rais Samia kuisifia Ewura kwa kazi nzuri inazofanya pale alipozindua ripoti zile mbili za utendaji za mwaka 2020/21 pale Mlimani City. Ni matarajio ya wananchi hata ripoti hiyo itaonyesha mazuri mengi inayoyafanya Ewura. 

Kaguo anasema katika kutekeleza kazi zake, EWURA ina wajibu wa kukuza ustawi wa Watanzania kwa kuhimiza ushindani wenye tija na ufanisi kiuchumi; kulinda masilahi ya walaji na kulinda mitaji ya kifedha ya watoa huduma za maji.

Pia ina wajibu wa kuhimiza upatikanaji wa huduma zinazodhibitiwa kwa makundi yote ya vipato vya chini, maalumu na vijijini; kuimarisha utoaji wa elimu kwa umma na kujenga uelewa kuhusu sekta inazodhibiti haki na wajibu wa watumiaji na watoa huduma hizo na upokeaji na utatuzi wa malalamiko na migogoro ya kazi, wajibu na shughuli zao na kulinda na kutunza mazingira.

Huduma hizo ni za maji ambazo Waziri wa Maji, Jumaa Aweso anaeleza mafanikio ya utekelezaji wa miradi yake Julai, 2020 hadi Machi, 2021 kuwa ni pamoja na kuongezeka kiwango cha upatikanaji wa maji nchini kutoka asilimia 70.1 vijijini na 84 mijini mwaka 2019/20 hadi asilimia 72.3 vijijini na 86 mijini.

Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa maabara za ubora wa maji zenye ithibati kutoka moja ya Mwanza hadi saba, uzinduzi miradi mikubwa ya maji ya Tabora – Igunga – Nzega na Isaka – Kagongwa na utekelezaji wa kihistoria wa miradi 422 ya maji ambapo kati yake, ya vijijini ni miradi 355 na mijini miradi 67.

Kaguo anasema kukamilika kwa miradi mingi ya maji kuna maana kazi yao  ya kudhibiti  WSSAs zilizopo, zinazoanzishwa au zinazoongeza miradi ya maji inaongeza wigo wa kazi na kugeuka changamoto kwao inayowalazimu wajipange kuitatua. 

Kaguo anasema kwa mujibu wa kifungu cha 7 cha Sheria ya EWURA, majukumu yao ni kutekeleza kazi zote zilizoanishwa na sheria ya EWURA na kisekta, kutoa, kuhuisha na kufuta leseni; kuweka na kusimamia viwango vya ubora wa huduma.

Nyingine ni kudurusu na kusimamia bei za huduma, kutunga sheria ndogo na kanuni; kufuatilia maendeleo ya sekta zinazodhibitiwa kwa kuzingatia upatikanaji, ubora wa huduma, gharama ya huduma, ufanisi wa uzalishaji, uwekezaji na usambazaji wa huduma; kusimamia utatuzi wa malalamiko na migogoro; kutoa taarifa za kazi za udhibiti; kupata maoni ya mamlaka nyingine za udhibiti; na kusimamia utekelezaji wa sheria.

Ni katika kutekeleza hayo, Kaguo anasema Ewura imekuwa ikiita wananchi kwenye mikutano yao ya hadhara kujadiliana nao bei za maji au kuzuia upandishaji wa bei za maji kinyume cha sheria unaofanywa na WSSAs ili kusimamia ubora na haki yao.

Hivyo, anasema kuongezeka kwa miradi ya maji kulikoelezwa na Waziri wa Maji na Rais Samia katika kilele cha Wiki ya Maji wamekupokea kama changamoto inayowataka wajipange zaidi  kiutendaji ili wajenge uwezo wa kusimamia WSSAs vizuri zaidi.

Kaguo anasema uwezo huo wanao kwani umejidhihirisha katika ripoti yao ya utendaji ya mwaka 2019/20 ambapo mkurugenzi anasema walifanya vema zaidi mwaka 2019/20 kulinganisha na mwaka wa fedha wa 2018/19 katika maeneo ya kusimamia uzalishaji maji, udhibiti wa majitaka na udhibiti wa upotevu wa maji.

Pia Kaguo anasema mwaka huo walifanikiwa pia kudhibiti WSSAs katika masuala ya huduma za ufungaji mita na huduma kwa wateja wa maji, tija kwa wafanyakazi wa WSSAs na udhibiti wa ukusanyaji wa mapato ya uuzaji maji kwenye WSSAs.

Kaguo anayataja maeneo yaliyopewa kipaumbele kurekebishwa kuwa ni pamoja na bei kubwa ya maji, kupungua uzalishaji wa maji, utendaji usio na tija WSSAs na takwimu zisizo sahihi za maji.

 Kaguo anasema Menejimenti na Bodi  ya Wakurugenzi Ewura inao uwezo mkubwa wa kusimamia mambo yote yanayohitajika ili kwenda na kasi ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali katika sekta ya maji ikiwamo ujenzi wa bwawa kubwa la maji Kidunda, Morogoro, miradi ya maji Kimbiji na Ziwa Victoria. 

By Jamhuri