Rais apokee hizi sifa kwa hadhari 

Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa ziarani mkoani Mara hivi karibuni, miongoni mwa mambo aliyozungumza kwa mkazo ni suala la sifa anazomiminiwa.

Kwa maneno yake mwenyewe alisema hapendi kusifiwa yeye binafsi, bali sifa hizo ziende kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho yeye ndiye amepewa dhima ya kusimamia ilani iliyopelekwa kwa wananchi nao wakaridhia kukipa ushindi.

Hii si mara ya kwanza kwa Rais Samia kutoa kauli ya aina hii, lakini ni wazi kwamba wanaoendelea kumsifu bado hawajabadilika.

Kiongozi au mtu yeyote anapofanya jambo au mambo yenye faida, kusifiwa ni stahiki yake. Kwa muda mfupi alioshirika madaraka ya kuongoza taifa letu, Rais Samia amefanya mambo mengi, makubwa na mazuri. 

Si rahisi kuyaorodhesha mambo mema yote aliyofanya kwa muda mfupi, lakini ni haki tukisema Rais amesaidia kurejesha hali ya Watanzania kujiona wako huru katika taifa lao.

Amefanikiwa kuondoa au kupunguza kwa kiwango kikubwa matumizi ya simu za ‘WhatsApp’ ambazo wapo waliotaka kuzungumza jambo hata kama ni la kukopeshana fedha za mboga, walitumia mfumo huo kwa imani ya kukwepa kuvujisha mazungumzo yao. Ulifika wakati kuzungumza kitu ilionekana kama uhaini. Udukuzi ulikuwa sehemu ya maisha.

Rais Samia amesaidia kupunguza uonevu wa watu kuwekwa rumande kwa kesi zisizo na vichwa wala miguu. Kudaiana kodi kwa ‘mitutu’ ya bunduki, pingu na vitisho kumeondolewa, na kwa namna ya ajabu ni kwamba makusanyo ya nchi yameongezeka. Imani kwa wawekezaji inarudi. Miaka kadhaa iliyopita wawekezaji walikamatwa wakawekwa rumande kwa kudaiwa kodi hewa na wengine wakalipa mabilioni kwa uonevu. Wapo waliougua na hata kupoteza maisha kutokana na mshituko. 

Kunradhi, wakati fulani chombo chetu cha kodi badala ya kuwa Revenue Authority, kikawa Robbery Authority. Leo huo ubabe haupo. Hili ni jambo la kumshukuru Rais wetu na wanaomshauri.

Tulikuwa na viongozi wa ajabu mno walioumiza watu wengi. Nani asiyejua kilichofanywa na watu kama aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Arusha, mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, mkuu wa Wilaya ya Hai na wenzao wa jamii hiyo? 

Hawa walikuwa miungu-watu ambao mikono yao ilijaa dhuluma. Haya kwa Rais Samia yamepungua mno. Rais anaposifiwa kwa mapinduzi mema kama haya, hatuna budi kumsifu na kumshukuru. 

Tukawa na watu wanaoweza kusimama na kuwatukana wazee waliolitumikia taifa letu kwa heshima kubwa. Wakaachwa watambe. Watanzania wanapomshukuru Rais Samia, wanamshukuru kwa kuwaondolewa madhila haya.

Pengine shida yetu Tanzania ni kukosekana kwa mifumo. Kuna dalili za Rais Samia kuanza kujenga mifumo ili kwamba hata ikitokea tumempata mkuu wa mkoa ambaye ni ‘fyatu’, basi mfumo umbane.

Kwa mifumo ilivyo sasa ni vigumu mno Watanzania kubadilika siku moja na wote wakawa malaika. Ukimsikiliza Rais Samia na watangulizi wake – wote wanalalamika. Nchi hii hata kama si mfokaji, ukiwa kiongozi mkuu utafoka tu, maana kuna mambo yatakuwa hayaendi kama unavyotaka. Mambo hayaendi kwa sababu yanakwazwa na kukosekana kwa mifumo.

Malalamiko haya hayatakoma endapo aina ya mifumo ya kiuongozi na ya kitaasisi itabaki kama ilivyo. Kwa mfano, sioni ni kwa namna gani DAS, DED na DC wanaweza kuleta maendeleo ya kweli mahali ambako hapo hapo kuna mwenyekiti au meya wa mji/halmashauri/jiji. Mfumo tulionao ndio unaomfanya rais au waziri muda wote awe msuluhishi wa viongozi hao, maana mgongano walionao ni mkubwa mno.

Matokeo yake ndiyo haya sasa ya kila mmoja kutaka aonekane hodari kwa rais. Nimesema hapo awali kwamba si dhambi hata kidogo kumsifu rais wetu kwa kazi nzuri anazofanya, lakini pamoja na ukweli huo, tutazame kama kweli hizi sifa zinazomwagwa kwa rais wetu zina nia njema nyuma yake.

Sasa imekuwa fasheni kwa kila kiongozi anayesimama, awe wa Chama Cha Mapinduzi, au wa serikali kumsifu Rais wakati mwingine kwa namna ambayo unaona inapita kiasi. Watanzania wamebuni mbinu ya kuishi kwa kusifu, kujipendekeza na kufitinisha. Bila shaka walio madarakani wanajua shehena ya fitina inayosukumwa kwao.

Kila anayesimama hata kuzindua mradi wa madawati, sifa ni kwa Rais moja kwa moja bila hata kutambua nafasi ya wakulima wa miti waliowezesha upatikanaji wa mbao za kutengeneza hayo madawati. Haitashangaza siku moja kumsikia kiongozi akiipongeza serikali kwa kuleta mvua!

Waziri hawezi kusimama kuzungumza bila kumtaja Rais Samia, kana kwamba yeye waziri kwa nafasi na elimu yake hana la maana analoweza kufanya ili baadaye naye asifiwe na Rais. Sifa nyingine zinazomwagwa ni kama ngao tu ya kuhalalisha mambo fulani fulani. Sifa hizi zina faida na athari. Wale wanaoujua mchezo wa ‘darts’ wanaelewa pale mshale unapotakiwa kuingia (bullseye). 

Mawaziri na watendaji wengine wanapofanya kazi zao, wazifanye kama wao ili ikitokea kuna kasoro, Rais apate nafasi yake kama kiongozi mkuu kurekebisha kasoro hizo. Endapo watamfanya Rais aonekane ni yeye anayewatuma kufanya kila kitu, basi ikitokea dosari imeonekana au imetokea, lawama atatwishwa kiongozi mkuu wa nchi kwa sababu wameamua kumfanya ‘bullseye’.

Dosari hii ilionekana wakati wa uongozi wa Dk. John Magufuli. Yeye ndiye aliyeonekana kuagiza kila kitu kifanyike. Ilipotokea waziri akavuruga, ilionekana ni yeye Rais aliyeagiza au kuubariki uvurugaji huo. 

Tunayo mifano hai kama ile tuliyosikia ikitajwa mahakamani. Kuna DC alifanya kazi kwa jina na ‘maagizo’ ya Rais Magufuli. Lakini akili ya kawaida tu inagoma kuamini kuwa Rais anaweza kumwagiza DC aende kutenda ujambazi, au aende kuongoza ubakaji na uporaji. Lakini kwa sababu kila kilichofanywa kilihusishwa na ‘maagizo kutoka juu’, ni vigumu sana kumtenganisha kiongozi mkuu wa nchi wa wakati huo na hata matukio mabaya yaliyofanywa na wasaidizi wake.

Sote tunaona na kusikia namna wale walioimba mapambio ya sifa kwa Rais Magufuli walivyomgeuka na kumponda. Hawa hawa waliomsifu leo wanajitahidi kukomaa mishipa kutuaminisha kuwa Dk. Magufuli alikuwa kiongozi mbaya. 

Bahati mbaya zaidi, hao hao wanaomponda Dk. Magufuli, ndio hawa hawa walio mstari wa mbele kumsifu mno Rais Samia. Hawa ni wanafiki. Kitu gani kitawazuia kumponda Rais wetu huyu akishang’atuka?

Ninayo mapendekezo: Rais Samia aendelee na msimamo wake wa kukataa sifa zisizo na nia njema. Kama alivyosema mwenyewe, sifa ziwe kwa chama chake na serikali. 

Pili, mawaziri na watendaji wengine wa umma wafanye kazi zao bila kuonyesha kuwa wanafanya kwa sababu Rais anataka iwe hivyo. Je, bila kutumwa hawawezi kufanya kazi? Nia njema ya Rais tunaijua iko ndani ya ilani, miongozo na mipango ya nchi, kwa hiyo kinachofanywa ndio wajibu wenyewe huo wa kulitumikia taifa.

Tatu, wale mabingwa wa kusifu sharti wajulikane lengo lao ni lipi, maana isije ikawa kumsifu Rais kunatumika kama koti la kuficha uovu na sanaa zilizo nyuma ya pazia. 

Sisi wengine tukienda vijijini au mitaani kwetu huwa tunakuwa makini – ukiona mtu anakuja na kuanza kukumwagia sifa nyingi za uungwana au mapenzi yako kwa wanakijiji au kwa wana mtaa wenzako, ujue hapo unalainishwa tu, kwani mwishowe utatakiwa ulipie ‘wanzuki’ au kitu kingine. Hakuna anayesifu bila kuwa na ajenda nyuma yake.

Nimeyaandika haya kwa nia njema, kwa kuwa wengi wetu tungependa kumuona Rais wetu akifanikiwa zaidi, maana ameshaonyesha mwelekeo mwema. Tumsaidie kwa kumweleza tunayodhani yana tija kwa uongozi wake na kwa taifa letu. Tusimpe sifa nyingi hata akadhani kila kitu kiko sawa ilhali kuna mahali pa kusawazisha. 

Rais wetu asifanywe ‘bullseye’ ili kwamba mambo yakienda mrama aonekane yeye ni chanzo. Hapana. Wasaidizi wake wawe na ujasiri wa kutekeleza wajibu wao bila kumsukumia kila kitu kwa kujificha nyuma ya sifa. 

Uwajibikaji wa pamoja ni muhimu sana ili hatimaye kama ni sifa iwe kwa serikali yote na kama ni lawama asiachiwe rais mwenyewe. Tunao wajibu wa kumlinda Rais wetu dhidi ya hila zote za vilemba vya ukoka. Mungu ambariki Rais Samia.