Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua thabiti za kukomesha uhalifu wa kimtandao, ikiwemo utapeli unaotumia laini za simu na mifumo ya kidijitali, wakati akihitimisha hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo bungeni jijini Dodoma leo Alhamisi Aprili 30, 2026.
Waziri Kairuki amssema Serikali imeimarisha uchunguzi na usimamizi wa laini za simu zinazotumika katika matukio ya kihalifu, hatua iliyowezesha kufungiwa kwa laini 62,879 zilizobainika kuhusishwa na uhalifu mtandaoni.
Aidha, ameleza kuwa Serikali imechukua hatua za kufunga usajili mpya wa laini mpya za simu kwa kutumia vitambulisho vya taifa, ambapo laini 60,177 zilizokuwa na viashiria vya utapeli au kuhusishwa na matukio ya uhalifu zimefanyiwa uchunguzi na kuchukuliwa hatua stahiki.
Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, hatua hizi ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuimarisha usalama wa mtandao na kulinda wananchi dhidi ya wimbi la utapeli mtandaoni, ambao umeendelea kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi.
Amesema wizara itaendelea kushirikiana na kampuni za simu, vyombo vya dola na taasisi za usimamizi wa TEHAMA ili kuhakikisha mifumo ya mawasiliano inakuwa salama na wananchi wanatumia teknolojia kwa uaminifu na uhakika.


