Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekanusha taarifa inayosambaa katika mitandao ya kijamii ikidai kuwa tukio la Aphelion linalotokea katika mfumo wa Jua litasababisha baridi kali nchini Tanzania kuanzia Agosti 10, 2026.
TMA imesema taarifa hiyo si ya kweli, ikieleza kuwa tukio la Aphelion ni hali ya kawaida katika mzunguko wa Dunia kwenye mfumo wa Jua na hutokea kila mwaka, hivyo haliwezi kuhusishwa moja kwa moja na kuongezeka kwa baridi nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA , tukio hilo linatokea wakati Dunia inapokuwa katika hatua ya kuwa mbali zaidi na Jua katika mzunguko wake, lakini mchango wake katika mwenendo wa hali ya hewa, ikiwemo hali ya baridi, ni mdogo sana.
TMA imeeleza kuwa saa 11:00 alfajiri kwa muda wa saa 27, tukio la Aphelion litashuhudiwa na kwamba tukio hilo litaambatana na msimu mmoja kuwa mdogo na mwingine kuwa mkubwa katika maeneo ya Dunia kutokana na Dunia kuwa karibu au mbali na Jua.
Hata hivyo, TMA imefafanua kuwa hali ya hewa nchini inaendelea kutawaliwa na mifumo ya kawaida ya hali ya hewa ya msimu wa Kipupwe, unaoanzia Juni hadi Agosti kila mwaka.
Kwa mujibu wa utabiri wa msimu wa Kipupwe uliotolewa na TMA Mei 25, 2026, baadhi ya maeneo nchini yanatarajiwa kuendelea kuwa na vipindi vya baridi zaidi kuliko maeneo mengine.
Maeneo hayo ni pamoja na Ukanda wa Pwani ya Kusini, mkoani Dodoma, Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, maeneo ya nchi kavu, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Nyanda za Juu Kusini Magharibi, pamoja na mikoa ya Singida na maeneo mengine.
TMA imesema hali ya joto inayotarajiwa katika kipindi hiki inatofautiana kulingana na eneo, ambapo nyuzi joto kati ya 6°C na 21°C zinatarajiwa katika maeneo ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi, huku maeneo ya Nyanda za Juu Kusini yakitarajiwa kuwa na nyuzi joto kati ya 10°C na 20°C.
Kwa maeneo ya Kandaya Kusini, joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi 10°C na 25°C, wakati maeneo mengine ya nchi yanaweza kuwa na joto kati ya nyuzi 10°C na 22°C.
TMA imeongeza kuwa hali ya baridi inaweza kuendelea kujitokeza katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na mifumo ya hali ya hewa inayotawala katika kipindi cha Kipupwe, lakini hali hiyo haihusiani na tukio la Aphelion kama inavyodaiwa katika taarifa inayosambaa mitandaoni.
“Taarifa hii ni potofu, kwani tukio la Aphelion ni hali ya kawaida katika mzunguko wa Dunia kwenye mfumo wa Jua ambayo hutokea kila mwaka ikihusisha tukio la Dunia na Ikweta. Hata hivyo, mchango wake katika mwenendo wa hali ya baridi ni mdogo sana,” TMA imeeleza.
TMA imeonya kuwa taarifa zisizo sahihi kuhusu hali ya hewa zinaweza kuleta hofu na mkanganyiko kwa wananchi, ikiwemo madai kwamba baridi kali inaweza kusababisha matatizo ya kiafya kama mafua, kikohozi na matatizo ya kupumua.
Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa ndiyo taasisi yenye jukumu na mamlaka ya kutoa na kusambaza taarifa rasmi za utabiri na tahadhari za hali ya hewa nchini.
TMA imewakumbusha wananchi kutumia taarifa rasmi kutoka mamlaka hiyo na kuepuka kusambaza taarifa za utabiri wa hali ya hewa ambazo hazijatolewa na taasisi yenye mamlaka.
Aidha, TMA imeeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019, pamoja na vifungu vya 27(5) na 46(1), ni kosa kisheria kutoa au kusambaza taarifa zisizo rasmi za utabiri na tahadhari za hali ya hewa kwa umma.


