Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mufindi

Serikali wilayani Mafinga imetoa wito kwa maofisa kwa viongozi wa vijiji, dini, Serikali pamoja na wananchi wilayani humo wa kuhamasishana na kujitokeza kwa wingi katika zoezi la usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa na vifo linalotekelezwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mafinga, Dkt. Linda Salekwa wakati wa uzinduzi wa kampeni ya usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa na vifo uliofanyika katika Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Lufana, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, ambapo amesisitiza kuwa vyeti hivyo ni nyaraka muhimu katika kumtambulisha mwananchi na kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii.

Alisema cheti cha kuzaliwa ni nyaraka muhimu inayobeba taarifa za msingi za mtu na kuthibitisha utambulisho pamoja na uraia wake, hivyo kila mwananchi anapaswa kuhakikisha anakuwa nacho na kukitunza kwa ajili ya matumizi ya sasa na ya baadaye.

Kwa mujibu wa Dkt. Salekwa, baadhi ya wananchi, hususan wanaoishi vijijini, wamekuwa wakikosa nyaraka hizo kutokana na kutofuatilia kwa wakati taarifa na huduma zinazotolewa na Serikali, jambo ambalo huwasababishia changamoto pale wanapohitaji kuzitumia katika kupata huduma nyingine muhimu.

“Tumekuwa tukitoa taarifa za mambo mbalimbali, lakini wananchi hawatilii maanani. Ndiyo maana wanapitwa na mambo muhimu. Huduma hizi za RITA zinahitaji kila mwananchi awe nazo, kwani ni nyaraka muhimu zitakazomsaidia katika upatikanaji wa huduma nyingi za kijamii,” alisema Dkt. Salekwa.

Alisema kuwa kuwa na cheti cha kuzaliwa kunaweza kumsaidia mwananchi katika mazingira mbalimbali, ikiwemo pale anapopata ajali, anapofariki, anapopotea au anapokumbana na mazingira mengine yanayohitaji kuthibitisha utambulisho wake.

Alisisitiza kuwa nyaraka hizo ni sehemu ya ulinzi na utambulisho wa mwananchi, kwa kuwa zinatoa taarifa zinazoweza kusaidia kumtambua mtu na kuwezesha ndugu, Serikali au taasisi husika kuchukua hatua stahiki wakati wa changamoto.

“Vyeti hivi vitakuwa zaidi ya ulinzi kwetu sisi wote, kwani vinatupa nafasi kubwa ya kutambulika katika maeneo tofauti. Hata inapotokea shida, ni rahisi watu kujua sisi ni nani na namna wanavyoweza kusogeza msaada kwa karibu zaidi,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Mafinga, Dkt. Linda Salekwa akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa kampeni ya usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa na vifo uliofanyika katika Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Lufana, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa kampeni iliyoandaliwa na Wakala wa Usajili,Ufilisi na Udhamini (RITA) jana.

Aidha, Dkt. Salekwa aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kampeni hiyo ili kuhakikisha wananchi wote wenye uhitaji wa huduma za RITA wanapata huduma hizo kwa wakati kabla ya kukamilika kwa siku zilizopangwa.

Alisema ushiriki wa viongozi wa Serikali, viongozi wa dini na viongozi wa jamii ni muhimu katika kuhakikisha taarifa za kampeni hiyo zinawafikia wananchi wengi zaidi, hususan wale ambao bado hawajapata vyeti vya kuzaliwa au vifo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mtwango, Bw. Monte Kilambia, aliipongeza RITA kwa kusogeza huduma hizo karibu na wananchi, akisema hatua hiyo itapunguza usumbufu, gharama na muda ambao wananchi wamekuwa wakitumia kusafiri kwenda mjini kufuatilia huduma hizo.

Alisema huduma zinazotolewa katika kampeni hiyo, zikiwemo usajili na upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa na vifo pamoja na huduma zinazohusiana na udhamini na mirathi, zina umuhimu mkubwa katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Kwa mujibu wa Kilambia, vijana ni miongoni mwa kundi litakalonufaika kwa kiasi kikubwa na upatikanaji wa huduma hizo, hasa wakati wa kuomba ufadhili wa masomo, mikopo ya elimu ya juu na fursa nyingine zinazohitaji nyaraka za utambulisho.

Amesema baadhi ya vijana wamekuwa wakipitia changamoto wakati wa kutafuta udhamini wa masomo au kuomba mikopo kutokana na kukosa nyaraka muhimu za utambulisho, hali ambayo imekuwa ikiwalazimu kutumia muda na gharama zaidi kufuatilia huduma hizo katika maeneo ya mijini.

“Kuna wakati vijana wanataka kuomba mikopo ya elimu ya juu, lakini wanajikuta wakikwama kutokana na kukosa cheti cha kuzaliwa ambacho ni miongoni mwa nyaraka muhimu zinazowapa uhalali wa kukamilisha mchakato huo,” alisema Kilambia.

Alisema kusogezwa kwa huduma za RITA karibu na wananchi ni hatua muhimu kwa sababu kutawasaidia wananchi kupata nyaraka hizo kwa urahisi na hivyo kuongeza uwezekano wa kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali na taasisi nyingine.

Kwa upande wake, mwananchi wa Kata ya Mponda, Bw. Clayson Samwel, alisema upatikanaji wa huduma hizo katika maeneo ya karibu na wananchi utasaidia kutatua changamoto ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikiwakabili wakazi wa maeneo ya vijijini.

Alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakikumbana na usumbufu mkubwa wakati wa kufuatilia mafao ya mifuko ya hifadhi ya jamii, ikiwemo pale ambapo mwananchi anahitaji nyaraka za kuthibitisha utambulisho, kuzaliwa au kifo cha ndugu yake.

Kwa mujibu wa Samwel, wakazi wengi wa eneo hilo wanajishughulisha na shughuli za uvunaji wa chai katika mashamba makubwa, na wakati mwingine hukutana na changamoto ya kukosa cheti cha kuzaliwa wanapotaka kuomba ajira.

Mkuu wa Wilaya ya Mafinga, Dkt. Linda Salekwa akimkabidhi mwananchi cheti cha kuzaliwa mala baada ya kusajiliwa wakati wa uzinduzi wa kampeni ya usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa na vifo uliofanyika katika Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Lufana, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa kampeni iliyoandaliwa na Wakala wa Usajili,Ufilisi na Udhamini (RITA) jana

Alisema hali hiyo imekuwa ikiwafanya baadhi ya wananchi kukosa fursa za ajira kwa sababu ya kutokuwa na nyaraka muhimu zinazohitajika katika mchakato wa kuajiriwa.

“Changamoto ni nyingi. Wapo ambao wamekuwa wakifuatilia mafao ya ndugu zao waliofariki na wanahitajika kuwa na cheti cha kifo au cheti cha kuzaliwa. Sasa wanapovikosa, wanajikuta wanakosa huduma kwa wakati,” alisema Samwel.

Aliongeza kuwa kusogezwa kwa huduma hizo katika maeneo ya wananchi kutasaidia kupunguza safari zisizo za lazima kwenda mjini na kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa wakati huku wakipunguza gharama za usafiri na muda wanaotumia kufuatilia nyaraka hizo.

Kampeni hiyo ya RITA inatarajiwa kuwawezesha wananchi wa Mufindi kupata huduma za usajili na upatikanaji wa nyaraka muhimu kwa urahisi zaidi, huku viongozi wa Serikali wakitoa wito kwa wananchi kutumia fursa hiyo kuhakikisha taarifa zao za msingi za kiraia zimesajiliwa na nyaraka husika zinapatikana.