Na Mwandishi Maalumu , Dodoma

Wazazi na walezi nchini wametakiwa kuwapeleka watoto wao wa kike wenye umri wa miaka 9 hadi 14 kupata chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi ili kuwakinga dhidi ya ugonjwa huo unaoongoza kwa vifo miongoni mwa saratani za uzazi kwa wanawake.

Rai hiyo imetolewa leo na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Frank Rutachunzibwa, wakati akitoa mada ya uelimishaji kuhusu saratani kwa watumishi wa Wizara ya Fedha, Mtumba jijini Dodoma.

Dkt.Rutachunzibwa alisema chanjo hiyo hufanya kazi vizuri zaidi kwa watoto ambao bado hawajaanza kujamiiana kwani huwapa kinga dhidi ya maambukizi yanayoweza kusababisha saratani ya mlango wa kizazi baadaye katika maishani yao.

Alibainisha kuwa kila mwaka maelfu ya wanawake hupoteza maisha kutokana na saratani hiyo huku sababu kubwa ikiwa ni kuchelewa kugundua ugonjwa huo.

“Kati ya wagonjwa wengi tunaowaona, idadi kubwa hufika hospitalini wakiwa katika hatua za mwisho” alisema.

Dkt. Frank Rutachunzibwa aliongeza kuwa pamoja na saratani ya mlango wa kizazi, zipo pia saratani nyingine zinazowaathiri watanzania wengi ikiwemo saratani ya matiti, tezi dume na mfumo wa chakula.

Daktati huyo Bingwa wa Magonjwa ya Saratani alisisitiza umuhimu wa kujichunguza mapema na kufika hospitalini mara kwa mara kwa uchunguzi huku akionya kuwa watu wengi bado wanakimbilia tiba mbadala badala ya matibabu ya kisasa.

“Saratani inatibika kama magonjwa mengine. Ni muhimu kujipenda, kujichunguza na kutafuta matibabu sahihi bila kuchelewa lakini bado kuna imani potofu na mwitikio mdogo wa huduma za kinga, hali inayochangia wagonjwa wengi kugundulika katika hatua za mwisho za ugonjwa”, alisisitiza.

Alitaja baadhi ya vihatarishi vya saratani kuwa ni pamoja na mtindo usiofaa wa maisha, uvutaji wa sigara, pamoja na sababu za kinasaba. Pia alibainisha kuwa wanaume wanaweza kupata saratani ya matiti ingawa ni kwa kiwango kidogo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mali za Serikali, Choto Sendo aliishukuru Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) kwa kutoa elimu ya magonjwa ya saratani na yasiyo ya kuambukiza kwa watumishi wa Wizara hiyo na kusema kuwa elimu waliyoipata pamoja na upimaji watakaofanyiwa utawasaidia kujua hali za afya zao.

“Ninaishauri ORCI kuendelea kufanya tafiti ili kubaini sababu za ongezeko la saratani katika baadhi ya maeneo ya nchi, ikiwemo Kanda ya kaskazini ,Nyanda za juu kusini, Kanda ya Ziwa na Dar es Salaam, ni muhimu kuelewa chanzo cha tatizo ili kuweka mikakati madhubuti ya kinga badala ya kuendelea kutoa matibabu pekee”, alisema Sendo.

Saratani ya mlango wa kizazi ni miongoni mwa saratani zinazoongoza kwa vifo vya wanawake nchini, huku changamoto kubwa ikiwa ni uelewa mdogo na kuchelewa kwa uchunguzi na matibabu. Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, chanjo kwa watoto wa umri wa miaka 9 hadi 14 ni njia muhimu ya kinga dhidi ya ugonjwa huo sambamba na uchunguzi wa mara kwa mara kwa watu wazima.