Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kiteto
MKUU wa Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, Remidius Mwema, amekabidhiwa rasmi jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kiteto na Mkuu wa Mkoa Queen Sendiga, lenye thamani ya Shilingi bilioni 1.7 lililopo Mtaa wa Msakasaka, Kata ya Bwagamoyo, Tarafa ya Kibaya Wilayani Kiteto.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Sendiga amekabidhi jengo hilo baada ya kukagua na kujiridhisha na hatua ya ukamilishaji wa mradi huo wenye vyumba 35 na ukumbi wa mikutano ambao umetekelezwa kwa mfumo wa force akaunti tangu kuanza kwake tarehe 30 Machi, 2023.
“Nawapongeza wataalamu na mafundi wote walioshiriki kufanikisha ujenzi huu, uzuri wa jengo hili ni lazima uende sambamba na utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kutoa tafsiri halisi ya uwajibikaji na utendaji kazi na huduma kwa wananchi” amesema Sendiga.
Hata hivyo, DC Mwema ameishukuru Serikali kwa kufanikisha mradi huo mkubwa na kuahidi kutekeleza kikamilifu maelekezo yote ya RC Sendiga kuhusu mradi pamoja na kuendelea kuifanya ofisi hiyo kuwa kimbilio la kila mwananchi wilayani Kiteto.
“Ni kweli jengo linapendeza sana kwa muonekano wake, ahadi yetu ni kuongeza furaha mioyoni mwa wananchi kwa usikivu na huduma kwa makundi yote ya wananchi, bahati nzuri miundombinu ya ofisi hizi inawezesha na watu wote wenye mahitaji maalum kuhudumiwa,” DC Mwema.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Msakasaka kata ya Bwagamoyo Mwangao Sadick Mpalila amesema mradi huo umesogeza karibu huduma kwa wananchi na kwamba uwepo wa jengo la utawala la Wilaya katika mtaa huo pia itasaidia wananchi wengi zaidi sasa kupata huduma kwa haraka na wakati mmoja.


