Na Do Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma
Hatua ya kuimarisha uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma imechukua sura mpya baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuanza kuwahoji viongozi wa halmashauri 39 kutoka mikoa 15 kuhusu hoja zilizobainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), huku ikisisitiza ufuatiliaji wa utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa ili kuziba mianya ya ubadhirifu.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ado Shaibu Ado, ambaye pia ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini, amesema hatua hiyo imewezekana baada ya Spika wa Bunge kutoa kibali kwa kamati kuendelea na uchambuzi wa hoja za ukaguzi, ambapo awali wakati wa Bunge la Bajeti ilizihoji halmashauri nane na sasa imepewa nafasi ya kuzihoji halmashauri 39 kutoka mikoa 15.
Akizungumza bungeni Leo Agosti 4,2026 Dodoma ,mesema katika zoezi hilo, kamati inawahoji Wakurugenzi wa Halmashauri ambao ni Maafisa Masuuli pamoja na timu zao za menejimenti ili kujibu hoja zote zilizobainishwa na CAG katika halmashauri husika.
Ado amesema pamoja na kusikiliza maelezo ya viongozi hao, kamati pia inafuatilia utekelezaji wa maagizo iliyowahi kuyatoa pamoja na mapendekezo ya CAG ili kujiridhisha kama dosari zilizobainishwa zimefanyiwa kazi.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 14 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, LAAC ina majukumu matatu makuu. Jukumu la kwanza ni kuchunguza maeneo yote yenye matumizi mabaya ya fedha za Serikali za Mitaa yaliyoainishwa katika ripoti ya CAG kwa kuwahoji Maafisa Masuuli, kusikiliza utetezi wao na kutoa maelekezo ya awali pale inapobaini kuna ulazima wa kufanya hivyo.
Jukumu la pili ni kufuatilia utekelezaji wa maagizo na mapendekezo yaliyowahi kutolewa na kamati pamoja na yale yaliyotolewa na CAG, kwa lengo la kuhakikisha mapungufu yaliyojitokeza yanarekebishwa na hayajirudii katika halmashauri.
Amesema jukumu la tatu ni kuishauri Serikali na Serikali za Mitaa kuhusu hatua za kuboresha usimamizi wa fedha za umma na kuimarisha uwajibikaji, ili kupunguza matumizi mabaya ya fedha za Serikali na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ado amesema baada ya kukamilisha zoezi la kuhoji halmashauri zote, kamati itaandaa taarifa na mapendekezo ambayo yatawasilishwa bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa kuwa maazimio yatakayokuwa maelekezo rasmi kwa Serikali.










