Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Nzega

MWENGE wa uhuru umemaliza mbio zake kwenye Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora kwa kuridhia miradi yote 11 ya thamani ya shilingi Bilioni 4.1 hivyo kuendelea na mbio hizo Wilaya ya Igunga.

Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Naitapwaki Lemea Tukai, amemkabidhi mwenge wa uhuru Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo, kwenye viwanja vya shule ya sekondari Ziba.

DC Tukai amesema mwenge wa uhuru mwaka 2026 umeridhia na kuipitisha miradi 11 ya maendeleo ya thamani ya shilingi Bilioni 4.1 kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Nzega na Mji wa Nzega.

Amesema kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Nzega mwenge umeridhia na kupitisha miradi ya ujenzi wa shule ya sekondari Ndala, kuzindua duka la dawa muhimu za binadamu Kichima na mradi wa vijana Ukombozi.

“Miradi mingine ni wodi ya wagonjwa kituo cha afya Busondo, jiwe la msingi barabara ya Mwambaha – Lubisu na kuweka jiwe la msingi shule ya sekondari Mwabangu,” amesema DC Tukai.

Amesema Septemba 19, mwaka 2026 mwenge wa uhuru umeridhia na kupitisha miradi ya maendeleo ya Halmashauri ya Mji wa Nzega ambayo ni ofisi ya kijiji cha Kitangiri na Nkuba hotel.

Amesema umezindua vyumba viwili vya madarasa ya shule ya sekondari Hussein Bashe, mradi wa zahanati ya Nyasa na upanuzi wa mfumo wa kusafisha na kutibu maji Nzega.

“Pia mwenge wa uhuru umezindua barabara ya kiwango cha lami ya Lumambo – Kitongo tunashukuru sana, kwaherini wakimbiza mwenge wa uhuru wote wa kitaifa tunawaribisha tena,” amesema DC Tukai.

Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2026 Wazo Michael Mwang’onda amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Nzega kwa kuukimbiza mwenye wa uhuru kwa siku mbili mfululizo.

“Tunawapongeza Nzega kwa kuutendea haki mwenge wa uhuru 2026 kwani viongozi na wananchi kila mmoja amejitoa kwa nafasi yake hongereni sana,” amesema Mwang’onda.

Kauli mbiu ya mwenge wa uhuru mwaka 2026 ni ‘Tanzania ni yetu sote, Tushikamane kwa pamoja kuleta Maendeleo,